Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna mtoto wala mama anayestahili kufa wakati wa kujifungua:UNFPA 

Masita Lemorin mwenye umri wa miaka 26 akimyonyesha mwanae mwenye umri wa miezi 4 huko Port au Prince nchini Haiti
UNICEF/Marco Dormino
Masita Lemorin mwenye umri wa miaka 26 akimyonyesha mwanae mwenye umri wa miezi 4 huko Port au Prince nchini Haiti

Hakuna mtoto wala mama anayestahili kufa wakati wa kujifungua:UNFPA 

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani UNFPA limesema hakuna mtoto wala mama anayestahili kupoteza maisha wakati wa kujifungua nchini Haiti na ndio maana limeamua kulivalia njuga tatizo hilo. 

Huyo ni mmoja wa ndugu wa binti aliyepoteza maisha wakati wa kujifungua mjini Port-au Prince nchini Haiti akisema binamu yake aliyekuwa mjamzito alifia hospitali wakati anajifungua na mwanaye mchanga alikufa pia.

Kwa mujibu wa shirika la UNFPA Haiti ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya vifo vya wakati wa kujifungua vya watoto na kina mama kutokana na sababu mbalimbali lakini kubwa zaidi ni uhaba wa wauguzi na wakunga wenye ujuzi unaohitajika.

Zaidi ya kina mama 500 kati 100,000 hupoteza maisha wakati wakijifungua nchini humo na takriban theluthi mbili hujifungua bila msaada wowote wa muuguzi au mkunga. Stefani Roche ni mkunga katika moja ya hospitani mjini Port-au-Prince,“Kuwa na fursa ya kumpata muuguzi na mkunga mwenye ujuzi bado ni changamoto kubwa kwetu kwa sasa. Tunachokitaka ni kwa wanawake kujifungua katika mazingira salama bila hatari.”

Eloniese Vilise ni miongoni mwa kina mama ambaye wakati wa ujauzito wake alihuduria kliniki kwa mkunga Roche katika hospitali hii kila wiki kupata ushauri kuhusu afya yake na lishe na akajifungua salama mtoto wa kike.“Ninamambo mazuri tu ya kusema kuhusu mkunga Stefani Roche kutokana na jinsi anavyohudumia na kusaidia watu, nilihisi ni kama rafiki yangu na ndio maana namshukuru sana.”

Kwa kutambua changamoto wa waugunzi na wakunga  na mahitaji nchini Haiti sasa UNFPA inashirikiana na wadau kutatua changamoto hiyo ikisema kupatikana kwa wakunga waliofuzu kunaweza kuokoa maisha ya kina mama 28,000 wakati wa kujifungua kila mwaka.

Miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na shirika hilo ni kutoa mafunzo kwa wauguzi na wakunga, vifaa, kutoa elimu kwa kina mama wajawazito na kuwekeza katika kuongeza idadi ya wahudumu hao muhimu wa afya katika hospitali zikiwemo  vijijini.