Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali acheni wanahabari wafanye kazi yao bila uoga wala upendeleo – Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na vyombo vya habari mjini Benghazi.
UN Libya
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na vyombo vya habari mjini Benghazi.

Serikali acheni wanahabari wafanye kazi yao bila uoga wala upendeleo – Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kuelekea siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani tarehe 3 mwezi huu wa Mei, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema wanahabari na wafanyakazi katika vyombo vya habari ni muhimu katika kusaidia ulimwenguni kupitisha maamuzi sahihi kuhusu ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Kupitia ujumbe wake wa siku hiyo yenye maudhui, uandishi wa habari bila uoga wala upendeleo, Bwana Guterres amesema katika vita dhidi ya virusi vya Corona, maamuzi ya aina hiyo yanaweza kuleta tofauti kubwa kati ya uhai na kifo.

Ni kwa mantiki hiyo anatoa wito kwa serikali, na wengineo kuwahakikishia wanahabari kuwa wanaweza kufanya kazi yao wakati huu wa janga la COVID-19 na hata baada ya hapo.

Guterres amekumbusha kuwa waandishi kuwezeshwa kufanya kazi zao kwa uhuru na bila uoga ni jawabu mujarabu kwa kuwa wakati huu ambapo janga linazidi kusambaa, kunaibuka kwa kasi kubwa janga jipya la taarifa potofu, kuanzia ushauri hatari wa kiafya na nadharia zisizo na ukweli wowote.

“Vyombo vya habari vinatoa tiba: habari na uchambuzi uliothibitishwa, wa kisayansi  na wenye ukweli. Cha ajabu ni kwamba tangu kuanza kwa janga la Corona, waandishi wengi wa habari wanakabiliwa na vizuizi vya kuandika habari na hata kuadhibiwa pale wanapofanya kazi zao.”

Katibu Mkuu ameenda mbali akisema kuwa,

“Vizuizi vya muda mfupi katika kukabili mienendo ni muhimu katika kutokomeza COVID-19, lakini havipaswi kutumiwa vibaya kama mbinu ya kuzuia uwezo wa wanahabari kufanya kazi zao.”

Amevishukuru vyombo vya habari vinavyoendelea kuandika habari za ukweli na zenye uchambuzi yakinifu ,huku wakiwawajibisha viongozi katika kila sekta na kueleza ukweli viongozi.

Katibu Mkuu amesema anatambua kipekee wale ambao wanatekeleza majukumu yao ya kuandika habari kuhusu afya ya umma na kutoa wito pia kwa serikali kulinda wanahabari, na kuimarisha na kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari ambao amesema ni muhimu kwa mustakabali wa amani, haki na haki za binadamu kwa wote.