Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanahabari wanapolengwa, jamii kwa ujumla ndiyo inalipia gharama-Guterres

Picha ya makataba ikiwaonesha wanahabari wakipiga picha za video katika Makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani.
UN Photo/Ariana Lindquist
Picha ya makataba ikiwaonesha wanahabari wakipiga picha za video katika Makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani.

Wanahabari wanapolengwa, jamii kwa ujumla ndiyo inalipia gharama-Guterres

Haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia Ujumbe wake alioutoa hii leo mjini New York Marekani kuhusu siku  ya leo ya kimataifa ya kutokomeza ukwepaji wa sheria ya uhalifu dhidi ya wanahabari, amesema katika siku ya mwaka huu, dunia vikiwemo vyombo vya habari, juu ya changamoto nyingine, vimekabiliwa na changamoto mpya kabisa ambayo ni COVID-19. 

Bwana Guterres amesema, janga la COVID-19 limeonesha hatari mpya kwa waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari, hata idadi ya mashambulio juu ya usalama wao wa mwili yameongezeka. Kulikuwa na mashambulio yasiyopungua 21 kwa waandishi wa habari walioshughulikia maandamano katika nusu ya kwanza ya mwaka huu 2020 ambayo ni sawa na idadi ya mashambulio kama hayo katika mwaka mzima wa 2017. Pia kumekuwa na vikwazo vya ziada kwa kazi ya waandishi wa habari, pamoja na vitisho vya mashtaka, kukamatwa, kufungwa, kunyimwa upatikanaji wa uandishi wa habari na kushindwa kuchunguza na kushtaki uhalifu dhidi yao. 

 “Wanahabari wanapolengwa, jamii kwa ujumla inalipia gharama. Ikiwa hatutawalinda waandishi wa habari, uwezo wetu wa kukaa na habari na kufanya maamuzi yanayotegemea ushahidi utakuwa umezuiliwa sana. Wakati waandishi wa habari hawawezi kufanya kazi zao kwa usalama, tunapoteza ulinzi muhimu dhidi ya janga la habari potofu na habari mbaya ambazo zimeenea mtandaoni.” Amenukuliwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa 

Bwana Guterres amesema habari zinazoegemea ukweli na uchambuzi hutegemea ulinzi na usalama wa waandishi wa habari wanaofanya ripoti huru, iliyojikita katika kanuni ya msingi: "uandishi wa habari bila woga au upendeleo". 

Wakati ulimwengu unapambana na janga la COVID-19, narudia wito wangu wa kuwa na vyombo vya habari huru ambavyo vinaweza kuchukua jukumu muhimu katika amani, haki, maendeleo endelevu na haki za binadamu. 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa shrika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO, Audrey Azoulay, amesema kutokana na hali hiyo dhidi ya vyombo vya habari, Mataifa yana jukumu la kuwalinda wanahabari  na kuhakikisha kuwa watekelezaji wa uhalifu dhidi ya waandishi wa habari wanawajibishwa.   

Bwana Azoulay amesema jukumu moja muhimu la waandishi wa habari ni kufichua ukweli. Kwa waandishi wa habari wengi sana, hata hivyo, kusema ukweli huja na gharama. Ukweli na mamlaka haviendani kila wakati huku akitoa takwimu zinazoonesha kati ya mwaka 2010 na 2019, karibu waandishi wa habari 900 waliuawa wakati wakifanya kazi yao, zaidi ya 150 katika miaka miwili iliyopita pekee. Wengi wamepoteza maisha yao wakati wa kufuatilia mizozo, lakini zaidi wanauawa nje ya mazingira ya mizozo, wakati wakichunguza masuala kama ufisadi, usafirishaji haramu, makosa ya kisiasa, ukiukaji wa haki za binadamu na masuala ya mazingira.