Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wengi wakosa chanjo hata kabla ya COVID-19- UNICEF

Muuguzi akiandaa chanjo ya kuchanja mtoto katika kliniki Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© UNICEF/Thomas Nybo
Muuguzi akiandaa chanjo ya kuchanja mtoto katika kliniki Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Watoto wengi wakosa chanjo hata kabla ya COVID-19- UNICEF

Afya

Wiki ya chanjo ikiendelea duniani kote, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na wadau wake, linatoa wito kwa serikali na wahisani kuchukua hatua kuhakikisha watoto wanapata chanjo zao wakati huu ambapo kasi imeelekezwa zaidi kwenye kusaka chanjo dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

 

 Wiki ya chanjo ikiendelea duniani kote, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na wadau wake, linatoa wito kwa serikali na wahisani kuchukua hatua kuhakikisha watoto wanapata chanjo zao wakati huu ambapo kasi imeelekezwa zaidi kwenye kusaka chanjo dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Wito huo wa UNICEF unakutaja wakati ambapo takwimu mpya za shirika hilo zinaonesha kwamba takribani watoto milioni 182 duniani kote walikosa chanjo ya kwanza dhidi ya surua kati yam waka 2010 hadi 2018 ikimaanisha watoto milioni 20.3 kila mwaka.

UNICEF inasema kuwa kwa wastani, kiwango cha chanjo ya surua duniani ni asilimia 86, kiwango ambacho ni chini ya asilimia 95 inayotakiwa ili kuzuia mlipuko.

 

Mtu akipatiwa chanjo (Maktaba)
PAHO.WHO.Jane Dempster
Mtu akipatiwa chanjo (Maktaba)

Shirika hilo linasema ongezeko la watoto wasiopatiwa chanjo lilisababisha milipuko ya ugonjwa wa surua mwaka 2019 kwenye nchi za vipato vya juu kama vile Marekani, Uingereza na Ufaransa.

Nchi za kipato cha chini nazo hali ilikuwa si shwari hata kabla ya janga la COVID-19 ambapo kati yam waka 2010 na 2018, Ethiopia ilikuwa na idadi kubwa ya watoto walio na umri wa chini ya mwaka mmoja ambao hawakupatiwa chanjo ya surua.

Idadi kwa Ethiopia ilikuwa ni watoto milioni 10.9 ikifuatiwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, watoto 6.2 million, Afghanistan watoto milioni 3.8 million, Chad, Madagascar na Uganda kila moja ikiwa na watoto milioni 2.7 waliokosa chanjo ya Surua.

Akizungumzia sababu za DR Congo kuwa miongoni mwa nchi zilizokumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa Surua, Dkt.Jean Jacques Muyembe, mratibu wa vita dhidi ya Ebola nchini humo amesema kuwa, “tunaona aibu kwamba bado idadi kubwa ya vifo kutokana na surua. Ni kwa sababu Ebola ilitumia fedha zote ambazo zingalitumika kukabiliana na magonjwa mengine. Ebola imetumia kila kitu, mwitikio na rasilimali watu ambavyo vingalitumiwa kupambana na magonjwa mengine. Hii imedhoofisha mfumo wa afya. Hili ni fundisho kubwa kutokana na magonjwa hayo, kufahamu kuwa pindi kuna Ebola, tunachotakiwa ni mawasiliano bora na elimu bora kwa wananchi.

Hata hivyo Dkt. Muyembe amekumbusha kuwa surua ni ugonjwa unaoweza kuzuilika, kwa sababu kuna chanjo yenye ufanisi na kwamba virusi vya surua havibadiliki lakini ugonjwa huo unarudia mara kwa mara kwa sababu “utaratibu wa utoaji chanjo haufuatwi ipasavyo. Na kwangu mimi kufuata utaratibu wa chanjo ndio kila kitu. Na ni suala la mama, wazazi ambao wanapaswa kuwa na utashi wa kupeleka watoto wao wapatiwe chanjo. Na iwapo tutapanga vyema kampeni zetu za chanjo, kampeni ya chanjo haitakuwa kubwa. Kwa hiyo elimu kwa mwanamke, elimu kwa mama ndio msingi wa kila kitu kwenye chanjo.”

Serikali zifanye nini sasa?

UNICEF inataka serikali ziendeleze huduma za chanjo huku zikihakikisha usalama wa jamii na wahudumu wa afya. Pia zianze kupanga huduma za chanjo pindi janga la COVID-19 litakapomalizika, na pia ziwezesha ubia wa chanjo duniani GAVI ili uweze kusaidia kampeni zijazo za chanjona zihakikishe kuwa chanjo ya COVID-19 inapatikana na inafikia wale wanaoihitaji zaidi.