Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yagawa mashine 32 za Oksijeni DRC kupambana na COVID-19

Ndege ya mshikamano ya UN ikitokea Addis Ababa, Ethiopia itawasilisha vifaa tiba nchi kadhaa barani Afrika.
WFP/Edward Johnson
Ndege ya mshikamano ya UN ikitokea Addis Ababa, Ethiopia itawasilisha vifaa tiba nchi kadhaa barani Afrika.

UNICEF yagawa mashine 32 za Oksijeni DRC kupambana na COVID-19

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia latoto UNICEF limesambaza mashine 32 za hewa ya Oksijeni ili kusaidia wagonjwa mahututi katika vita dhidi ya janga la virusi vya Corona au COVID-19 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC

  Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia latoto UNICEF limesambaza mashine 32 za hewa ya Oksijeni ili kusaidia wagonjwa mahututi katika vita dhidi ya janga la virusi vya Corona au COVID-19 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Mashine hizo zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye kituo cha kuhifadhi vifaa cha UNICEF mjini Kinshasa zinagawanywa kwenye vituo 6 vya afya mjini Kinshasa  na kwenye majimbo mengine kama sehemu ya msaada wa shirika hilo katika utekelezaji wa mapambano dhidi ya COVID-19.

Akizungumzia maandalizi ya usambazaji wa mashine hizo ambazo zzimeanzwa kusambazwa leo Jumatatu Christophe Mwanambwana mkuu wa masuala ya kiufundi wa UNICEF mjini Kinshasa amesema

“Hapa katika kituo cha kuhifadhi vifaa cha UNICEF tunaandaa usafirishaji wa mashine hizi ambazo tutazitoa katika vituo 6 vya afya vinapokea wagonjwa wa COVID-19 kwa sasa . Vituo hivyo ni Hospitali ya Monkole, St Joseph Alimete, hospitali ya Sino N’djili, klinini ya vijana , kliniki ya chuo kikuu na kliniki ya Ngaliema.”

Mwakilishi wa UNICEF DRC bwana Edourd Beigbeder amesema mashine hizi za Oksijeni zitawasaidia wagonjwa mahututi wa Corona ambao wanashindwa kupumua wenyewe ili waweze kuvuka kipindi kigumu kabla ya kupata ahuweni na kwamba shirika hilo litaendelea kuisaidia DRC kupambana na janga la corona.

“Hii ni awamu ya kwanza ambayo ndio imewasili, tunatumai kwamba itaokoa maisha kadhaa ya watu na tutaendelea kuleta vifaa zaidi katika hospitali.”

Mbali ya kusaidia kupambana na COVID-19 nchini DRC UNICEF pia inasaidia kukabiliana na Ebola, kipindupindu, surua na utapiamlo.