Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 25 walikosa chanjo wakati wa COVID-19 ni wakati wa kuziba pengo hilo:WHO

Mvulana akipokea chanjo ya surua katika kituo cha afya katika jimbo la Tigray la Ehtiopia. (Maktaba)
© UNICEF/Hema Balasundaram
Mvulana akipokea chanjo ya surua katika kituo cha afya katika jimbo la Tigray la Ehtiopia. (Maktaba)

Watoto milioni 25 walikosa chanjo wakati wa COVID-19 ni wakati wa kuziba pengo hilo:WHO

Afya

Wiki ya chanjo ya shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani WHO, inaanza leo ikichagiza juhudi kubwa kufanyika ili kuziba pengo la chanjo duniani kote.

Wiki hiyo itakayo kamilika Aprili 30 huadhinmishwa kila wiki ya mwisho ya mwezi Aprili lengo likiwa ni kuainisha juhudi za pamoja zinazohitajika ili kuwalinda watu dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

Katika wiki hii ambayo imebeba kaulimbiu “The Big Catch-Up” ikisisitiza juhudi kubwa zinazohitajika katika kibarua kilichopo kuziba pengo na kufikia lengo la chanjo, WHO inashirikiana na wadau mbalimbali kuzisaidia nchi kurejea katika msitari unaotakiwa kuhusu chanjo ili kuhakikisha watu wengi zaidi wanalindwa dhidi ya magonjwa yanayozuilika.

Hata hivyo shirika hilo linasema mila na imani kwa kiasi imechangia katika baadhi ya jamii watu kutopata chanjo na kusisitiza elimu na kampeni kuanzia ngazi ya mashinani . Hawa Amza ni mkimbizi katika kambi ya Dar es salaam inayosimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR katika eneo la Baga Sola nchini Chad, wakati wa COVID-19 mwanzo alikataa kupata chanjo kutokana na taarifa potofu zilizozagaa kuhusu chanjo lakini baada ya kuelimishwa akakubali kuchanjwa “Nimekubali kuchanjwa baada ya kuuliza waliochanjwa na hakuna hata mmoja aliyechangwa anayelalamika kusu matatizo ya kiafya. Nilipopata dozi ya kwanza sikupata madhara yoyote na sasa nimepata dozi ya pili nikiwa na ujauzito katika mieazi ya awali na najihisi vizuri tu.”

WHO inasisitiza kwamba “Tunahitaji kuchukua hatua sasa ili ili kuwafikia mamilioni ya Watoto ambao walikosa chanjo wakati wa janga la COVID-19, kurejesha usambazaji wa chanjo muhimu kwa kiwango cha angalau mwaka 2019 na kuimarisha huduma za msingi za afya ili kuweza kutoa chanjo.”

Twakwimu za WHO zinaonyesha kuwa “mwaka 2021 pekee Watoto milioni 25 walikosa angalau chanjo moja muhimu.”

Mwaka huu wiki hii ya chanjo itajikita na haja ya kuwafikia mamilioni ya watoto hao waliokosa chanjo wakati wa COVID-19 na pia kutanabaisha mafanikio ya baadhi yan chi ambazo tayari ziko mbioni kujikwamua na pengo la chanjo.

Kwa mujibu wa WHO lengo kubwa la wiki hii ya chanjo duniani ni kuhakikisha watoto wengi, watu wazima na jamii zao wanalindwa dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo, kuwaruhusu kuishi kwa furaha na kuwa na maisha yenye afya.