Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huu si wakati wa kusitisha ufadhili kwa WHO- Guterres

Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus wakipata taarifa kuhusu kituo cha operesheni za kimkakati dhidi ya virusi vya Corona huko Geneva, USwisi.
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus wakipata taarifa kuhusu kituo cha operesheni za kimkakati dhidi ya virusi vya Corona huko Geneva, USwisi.

Huu si wakati wa kusitisha ufadhili kwa WHO- Guterres

Afya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema huu si wakati wa kupunguza rasilimali za kufanikisha operesheni za shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO ambalo linakabiliana na janga la virusi vya Corona au COVID-19.

Bwana Guterres amesema hayo leo katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake jijini New York, Marekani akisema kuwa siyo tu kwa WHO bali pia si wakati wa kupunguza rasilimali kwa shirika lolote lile la kibinadamu linalopambana hivi sasa na ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19.

Kauli ya Katibu Mkuu imekuja saa chache kufuatia tangazo la leo Jumanne la Rais wa Marekani Donald Trump la kusitisha fedha kwa WHO, hadi baada ya tathmini ya hatua za shirika hilo dhidi ya mlipuko wa COVID-19.
 
Katibu Mkuu amesema, “kama nilivyosema tarehe 8 mwezi Aprili, janga la COVID-19 ni moja ya changamoto kubwa kuwahi kukumba dunia yetu sasa. Ni janga kubwa zaidi la kibinadamu lenye madhara makubwa kijamii na kiuchumi.”
Ukurasa kuhusu virusi vya Corona & Taarifa mpya

Amesema WHO, na maelfu ya wafanyakazi wake walio mstari wa mbele wakisaidia nchi wanachama na jamii zao hususan wale walio hatarini zaidi ambapo baadhi yao wanawapatia mafunzo, mwongozo, vifaa na huduma muhimu za kuokoa maisha huku wakikabili na virusi.

“Ni imani yangu kuwa WHO inapaswa kuungwa mkono kwa sababu bila shaka ni muhimu sana katika juhudi za dunia za kupambana na COVID-19,”  amesema Katibu Mkuu.

Ufadhili uendelee

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesema huu ni wakati wa mshikamano na kwamba, “kama nilivyosema awali, huu ni wakati wa umoja na jamii ya kimataifa kushirikiana na kukomesha hivi virusi na madhara yake.”

Bofya hapa kufahamu dondoo 5 juu ya umuhimu wa WHO katika kusongesha harakati za kimataifa dhidi ya COVID-19.

Hadi leo Jumanne, ramani ya kuenea kwa COVID-19 inayosimamiwa na WHO inaonesha kuwa zaidi ya watu zaidi ya watu milioni 1.8 katika mataifa 213 wamethibitishwa kuwa na virusi vya Corona na kati yao hao watu 117,000 wamefariki dunia.

Kwa nchi za Afrika Mashariki COVID-19 imethibitishwa Uganda, Kenya, Tanzania, Rwanda, Burundi,  Sudan Kusini ambapo hii leo Uganda na Tanzania zimeongeza muda wa hatua mbalimbali za kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo ikiwemo shule na vyuo kuendelea kufungwa.