Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO ina dhima muhimu sana katika kutokomeza COVID-19- Guterres

Timu ya WHO yawasili Tehran ili kuisaidia Iran kupambana na COVID-19
WHO
Timu ya WHO yawasili Tehran ili kuisaidia Iran kupambana na COVID-19

WHO ina dhima muhimu sana katika kutokomeza COVID-19- Guterres

Afya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema shirika la afya la umoja huo, WHO linapaswa kuungwa mkono duniani kote, akisema kuwa chombo hicho kimekuwa muhimu sana kikichukua msimamo wa kimataifa kukabiliana na mlipuko wa janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19.

Katika taarifa yake aliyoitoa leo kupitia msemaji wake jijini New York, Marekani, Guterres amesema, “janga la COVID-19 ni moja ya changamoto za hatari zadi ambazo dunia hii imewahi kukabiliana nazo. Na zaidi ya yote ni janga kubwa la kibinadamu lenye madhara kijamii na kiuchumi.”

Katibu Mkuu amegusia kuwa maelfu ya wafanyakazi wa WHO wako mashinani wanapambana na virusi hivyo mstari wa mbele, wakisaidia nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na kuhudumia watu walio hatarini zaidi huku wakiwapatia mwongozi, mafunzo, vifaa na hata misaada ya kuokoa maisha.

Ametoa mfano akisema kuwa, “nilishuhudia ujasiri na utayari wa wafanyakazi wa WHO nilipotembelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC mwaka jana ambapo wafanyakazi wa WHO wanafanya kazi katika mazingira magumu kwenye maeneo ya ndani zaidi wakikabiliana na Ebola.” Akitambua kuwa kuwa hakuna mgonjwa mpya wa Ebola aliyebainika katika miezi kadhaa, Katibu Mkuu amesema kuwa hayo ni mafanikio makubwa.

Virusi visivyokuwa vya kawaida

Virusi vya sasa si vya kawaida kabisa katika zama zetu na vinahitaji hatua za aina yake,”  amesema Guterres.

Amefafanua kuwa suala kwamba ukweli kuhusu virusi umetafsiriwa tofauti na vyombo mbalimbali, baada ya muda kupita na janga kumalizika, kutakuwepo na muda wa kutathimini na kubonga bongo kufahamu na kuelewa jinsi gani ugonjwa huo uliibuka na kuenea na kusababisha madhara makubwa duniani kote, na ni kwa jinsi gani wale wote waliohusika katika kushughulikia janga hilo walichukua hatua.

“Kile kitakachokuwa somo kutokana na janga hili kitakuwa muhimu sana katika kushughulikia majanga mengine kama hayo siku za usoni,”  amesema Katibu Mkuu huku akitamatisha taarifa yake akisema kuwa, “sasa si wakati huo wa tathmini bali ni wakati wa mshikamano, wakati wa jamii ya kimataifa kufanya kazi pamoja ili kukomesha hivi virusi na madhara yake.”

Tusiingize siasa kwenye COVID-19- Dkt. Tedros

Mapema akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video mjini Geneva, Uswisi, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus ametaka watu waache kuingiza siasa kwenye suala la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Amesema kuwa. "sijali nani anasema nini kuhusu mimi. Ningalipenda tujikite katika kuokoa maisha. Hakuna muda wa kupoteza. Tukiwa na Umoja na mshikamano katika ngazi ya taifa na kimataifa, rasilimali hazitakuwa tatizo. Tunaomba muweke karantiki suala la kuingiza siasa kwenye janga hili. Tunaomba mshikamano wa dhati. Kwa hiyo rasilimali? Zitatoka kwa wote.”