Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaondoa hofu kuhusu chanjo ya AstraZeneca na kuidhinisha ya Jonhson & Jonson

Cambodia ikipokea dozi 324,000 za AstraZeneca dhidi ya COVID-19 kupitia mkakati wa chanjo wa COVAX
© UNICEF/Antoine Raab
Cambodia ikipokea dozi 324,000 za AstraZeneca dhidi ya COVID-19 kupitia mkakati wa chanjo wa COVAX

WHO yaondoa hofu kuhusu chanjo ya AstraZeneca na kuidhinisha ya Jonhson & Jonson

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO limesema leo kwamba linajua kuhusu hofu ya damu kuganda inayohusishwa na kundi maalum la chanjo ya AstraZeneca-Oxford dhidi ya gonjwa la corona au COVID-19, lakini inashikilia kuwa hadi sasa, hakuna mtu aliyekufa kutokana na chanjo yoyote dhidi ya  virusi vya corona .

Hatua hiyo imekuja baada ya nchi kadhaa za Ulaya kusitisha kutolewa kwa chanjo hiyo ya AstraZeneca-Oxfork kama tahadhari.

“Tangu tarehe 9 Machi, kumekuwa na dozi zaidi ya milioni 268 za chanjo zilizosambazwa tangu kuzuka kwa janga hilo, na kulingana na takwimu zilizoripotiwa kwa WHO na serikali zamataifa mbalimbali hakuna sababu za kifo zilizopatikana au zilizosababishwa na chanjo ya COVID Chanjo -19 hadi sasa ”, kwa mujibu wa msemaji wa WHO Dkt. Margaret Harris.

Akizungumza kwa njia ya video huko Geneva Uswis , Dkt Harris ametanabaisha kwamba bodi ya ushauri ya wataalamu wa kimataifa ya WHO, SAGE, kwa sasa inatathmini ripoti juu ya chanjo ya AstraZeneca na kwamba matokeo hayo yatawekwa wazi mara tu yatakapopatikana.

Chanjo ya AstraZeneca/Oxford dhidi ya COVID-19 inatengenezwa nchini India chini ya leseni maalum.
© UNICEF/Dhiraj Singh
Chanjo ya AstraZeneca/Oxford dhidi ya COVID-19 inatengenezwa nchini India chini ya leseni maalum.

Hakuna kinachounganisha tatizo na chanjo

Dkt. Harris amesema vitendo vya damu kuganda miongoni mwa watu ni vya kawaida "kwa hivyo haijulikani endapi hii ilikuwa ni kitu ambacho kingetokea au ikiwa chanjo hiyo inawajibika kwa tatizo hilo. Hakuna uhusiano uliodhihirika baina ya mambo hayo mawili.”

Pia amesisitiza kwamba kamati ya tathmini ya hatari ya mashirika ya tiba ya Muungano wa Ulaya, Pharmacovigilance, pia imeamua kuwa faida za chanjo hiyo zimeendelea kuwa nyingi kuzidi hatari.

"Jopo hilo limechukua msimamo kwamba chanjo hiyo inapaswa kuendelea kiutumika wakati uchunguzi wa visa vya ghafla vya damu kuganda unaendelea.” Amesisitiza Dkt. Harris.

Nchi ambazo zimearifiwa kusitisha kmapeni za chanjo hiyo ya AstraZeneca ni pamoja na Austria, Denmark, Estonia, Lithuania, Norway, Iceland na Thailand.

UNICEF imeanza kusambaza mabomba ya sindano kwa ajili ya kampeni ya chanjo dhidi ya COVID-19 duniani kote chini ya mkakati wa COVAX
© UNICEF/Charles Asamoah
UNICEF imeanza kusambaza mabomba ya sindano kwa ajili ya kampeni ya chanjo dhidi ya COVID-19 duniani kote chini ya mkakati wa COVAX

Mamia ya uwezekano wa aina za chanjo

Kulingana na kitengo cha WHO cha ufuatiliaji wa chanjo dhidi ya  coronavirus">COVID-19, kuna chanjo aina 81 ambazo ziko katika awamu ya uzalishaji na zaidi ya 180 katika awamu ya awalim ya tathimini kabla ya kutengenezwa.

Hadi kufikia sasa, WHO imeidhinisha chanjo mbili za matumizi ya dharura dhidi ya COVID-19: chanjo ya Pfizer / BioNTech iliyoidhinishwa mnamo 31 Desemba 2020 na matoleo mawili ya chanjo ya AstraZeneca-Oxford, mnamo 15 Februari 2021.

Chanjo ya Wachina ya Sinovac kwa sasa iko katika hatua ya mwisho ya tathmini ya kliniki na inaweza kuidhinishwa kutumiwa mwishoni mwa mwezi, amesema Dkt. Harris.

"Kwa kweli, tunaangalia chanjo ya Wachina na kuna chanjo ya Johnson & Johnson ya kuzingatia, na tunaangalia nyingine kadhaa," ameongeza.

Idhini ya kutumia chanjo ya Johnson & Johnson

Takriban dozi bilioni 2 za chanjo dhidio ya Corona zinatarajiwa kusambazwa duniani ifikapo mwisho wa mwaka huu wa 2021
© UNICEF/Dhiraj Singh
Takriban dozi bilioni 2 za chanjo dhidio ya Corona zinatarajiwa kusambazwa duniani ifikapo mwisho wa mwaka huu wa 2021

Wakati huohuo WHO  leo pia imetangaza kutoa kibali kwa chanjo iliyotengenezwa na Janssen (Johnson & Johnson), kwa matumizi ya dharura katika nchi zote na kwa juhudi za kimataifa zinazosimamiwa na Umoja wa Mataifa kupitia mkakati wa kimataifa wa chanjo kote duniani wa COVAX.

Uamuzi huo umekuja baada ya idhini ya wakala wa dawa za Ulaya (EMA), kutangaza kuanza matumizi ya chanjo hiyo jana Alhamisi.

"Kila nyenzo mpya, salama na madhubuti dhidi ya COVID-19 ni hatua nyingine muhimu ya kukaribia kudhibiti janga hilo,", amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Ameongeza kuwa "Lakini matumaini yanayotolewa na nyenzo hizi hayatatekelezeka hadi pale yatakapopatikana kwa watu wote katika nchi zote. Ninazisihi serikali na kampuni zitimize ahadi zao na watumie suluhisho zote wanazoweza kuongeza uzalishaji ili vifaa hivi viwe bidhaa za umma ulimwenguni kote na kupatikana kwa wote, ikiwa ni suluhisho la pamoja kwa janga hili la kimataifa. "

Chanjo kutoka Janssen ni ya kwanza kuorodheshwa na WHO kama chanjo ya dozi moja, ambapo shirika hilo litasaidia katika masuala ya kiufundi ya  kuwezesha chanjo hiyo katika nchi zote. 

Utoaji wa chanjo dhidi ya COVID-19 nchini Kenya.
WHO Video
Utoaji wa chanjo dhidi ya COVID-19 nchini Kenya.

"Takwimu za kutosha za majaribio makubwa ya kliniki zilizotolewa  na kampuni hiyo pia zinaonyesha kwamba chanjo hiyo ni nzuri Zaidi kwa wazee", limesema shirika hilo katika taarifa yake kwa waandishi wa habari.

Takwimu za hivi karibuni

Kufikia leo Ijumaa 12 Machi, kumekuwa na wagonjwa 118,058,503 waliothibitishwa kuwambukizwa COVID-19, pamoja na vifo 2,621,046, vilivyoripotiwa kwa shirika la afya la Umoja wa Mastaifa.

Idadi kubwa zaidi ya visa vya maambukizi ya COVID-19 yaliyothibitishwa inaendelea kuwa Amerika ambayo ina wagonjwa 52,386,995, ikifuatiwa na Ulaya (40,438,291), Asia ya Kusini Mashariki (13,819,871), Mashariki mwa Mediterania (6,793,641), Afrika (2,924,244) na Pasifiki ya Magharibi (1,694,716).