Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde tusiwasahau wakimbizi wa ndani wakati wa COVID-19:UN

Watoto wakisafisha mikono kwa sabuni katika kituo cha elimu kinachofadhiliwa na UNICEF katika kambi ya wakimbizi wa Rohingya, Cox's Bazar, Bangladesh
© UNICEF/Suman Paul Himu
Watoto wakisafisha mikono kwa sabuni katika kituo cha elimu kinachofadhiliwa na UNICEF katika kambi ya wakimbizi wa Rohingya, Cox's Bazar, Bangladesh

Chonde chonde tusiwasahau wakimbizi wa ndani wakati wa COVID-19:UN

Haki za binadamu

Serikali zinapaswa kuongeza juhudi za hatua zake ili kuwalinda wakimbizi wa ndani milioni 40 kote duniani dhidi ya tishio la virusi vya Corona, COVIDI-19.

Wito huo umetolewa leo na Cecilia Jimenez-Damary mtaalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi wa ndani. Katika wito huo Bi. Jimenez-Damary amesema “Wakimbizi wa ndani wako katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya COVID-19 kutokana na fursa ndogo waliyonayo ya kupata huduma za afya, maji, usafi, chakula na makazi bora na mara nyingi wanakabiliwa na ubaguzi. Ni miongoni mwa watu wasiojiweza na wanapaswa kutosahaulika na serikali katika vita vyao dhidi  ya ugonjwa huu.”

Ameongeza kuwa wakimbizi wa ndani wale walio katika makambi au kuishi katika makazi ya pamoja hujikuta katika mrundikano mkubwa na makazi yao ya muda hayakidhi haja ya kupambana na maambukizi ya COVIDI-19, na hatari yao inaongezwa na migogoro ya vita.

Mtaalam huyo ameelezea kwamba mazingira ya watu waliotawanywa yanaweza kuongeza hatari ambayo tayari ilikuwepo kwa watu kama wazee na wenye maradhi ya muda mrefu katika kupata maambukizi ya COVID-19.

Watu waliotawanywa wenye ulemavu au kutoka kwenye makundi ya walio wachache au jamii za watu wa asili wanaweza kukabiliwa na vikwazo zaidi katika kupata huduma muhimu na huduma za afya. 

Hivyo amesisitiza “Serikali lazima zihakikishe kwamba wakimbizi wote wa ndani wana fursa ya maji, usafi, mahali pa kujisafi, makazi yanayojitosheleza na chakula. Pia watu hawa wanapaswa kupewa taarifa kuhusu hatari za ugonjwa huu, kinga na matibabu. Na kwa wale wanaohitaji matibabu kwa ajili ya COVID-19 lazima wapate fursa ya huduma muafaka za afya kwa wakati na bila ubaguzi.”

Mtaalam huyo wa haki za binadamu pia ametoa wito kwa serikali kujumuisha wakimbizi wa ndani katika mchakato wao wa maamuzi “wakimbizi wa ndani wanatambua vyema changamoto zinazowakabili , hivyo ushiriki wao katika kubaini changamoto hizi na kusaka suluhu muafaka za kukabiliana na COVID-19 ni muhimu."

Pia amesisitiza kwamba katika makambi hatua za kuzuia na kupambana na virusi hivi vya Corona lazina zichukuliwe kwa kuzingatia tathimini ya hatari inayohusiana na idadi ya watu kambini. 

Amri za kutotembea huenda zikahitajika lakini ni muhimu kuhakikisha pia kwamba kujitenga hakusababishi watu hawa kukosa msaada muhimu wanaouhitaji.

Ametoa wito kwamba “Nchi ni lazima ziongeze msaada wa kibinadamu kwa wakimbizi wa ndani kwa sababu ya janga hili huku zikichukua hatua muafaka kuzuia maambukizi ya COVID-19 na kuwalinda wahudumu wa misaada ya kibinadamu. Ni muhimu kwamba wakimbizi wa ndani hawatelekezwi katika janga hili na nazitaka nchi kutimiza wajibu wao kwa kuwalinda watu hawa.Pia naichagiza jumuiya ya kimataifa na wahisani kuhakikisha mshikamano na wale wasiojiweza duniani.”