Magereza na rumande zipunguze mirundikano kuepusha kusambaa COVID-19

25 Machi 2020

Ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 umeanza kusambaa kwenye magereza, vituo vya ushikiliaji wahamiaji wasio na nyaraka na hivyo serikali lazima zichukue hatua kulinda afya za wanaoshikiliwa kwenye maeneo hayo, amesema Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet.

Kuptia taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Bi. Bachelet amesema kuwa katika mataifa mengi, vituo vya kushikilia wahalifu au rumande zimejaa kupita kiasi huku mazingira ya kiafya yakiwa ni duni na huduma za afya ni kidogo au hazipo kabisa.

“Katika mazingira kama hayo, mtu kusema anajiweka mbali na mwenzake au anajitenga,haiwezekani kabisa. Serikali zinakabiliwa na mahitaij makubwa ya rasilimali zama za sasa na zinakabiliwa pia na maamuzi magumu ya kufanya,” amesema Kamishna Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu.

Hata hivyo amesema pamoja na kukumbwa na maamuzi magumu, wasisahau wale walioko gerezani au wale wanaoshikiliwa kweye vituo vya afya kutokana na matatizo ya akili, vituo vya malezi kwa wazee na yatima akisema kuwa, “madhara ya kusahau makundi hayo ni janga kubwa.”

Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa serikali kuhakikisha kuwa katika vikao vyao ya kupanga jinsi ya kushughulikia COVID-19, lazima wanajumuisha watu walio korokoroni na magerezani il kulinda kundi hilo pamoja na wafanyakazi wa taasisi hizo na wageni wao na jamii nzima kwa jumla.

Bi. Bachelet amesema kuwa, mlipuko huo wa COVID-19 ukiendelea kuenea na idadi ya vifo ikiongezeka na tayari magereza yameripoti vifo, “mamlaka lazima zichukue hatua kuzuia vifo zaidi miongoni mwa wafungwa, mahabusu na wafanyakazi.”

Kamishna huyo mkuu wa haki za binadamu amesema kuwa pindi wafungwa wanapoachiwa huru, wanapaswa kupimwa afya zao na hatua zichukuliwe kuhakikisha iwapo wanahitaji huduma au kufuatiliwa ikiwemo kufuatilia afya zao.

Ofisi ya haki za binadamu imesema kuwa kwa walio mahabusu, serikali zinapaswa kulinda afya zao kimwili na kiakili kwa mujibu wa kanuni za Umoja wa Mataifa za kuhudumia wafungwa zijulikanazo pia kama kanuni za Nelson Mandela

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter