Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ondoeni vikwazo kusaidia COVID-19, madaktari wasemao ukweli msiwaadhibu- Bachelet

Madaktari wakifurahi baada ya mgonjwa kupona kutoka hali mahututi kufuatia maambukizi ya ugonjwa wa corona.
Department of Critical Care Medicine, Affiliated Hospital of Guangdong Medical University
Madaktari wakifurahi baada ya mgonjwa kupona kutoka hali mahututi kufuatia maambukizi ya ugonjwa wa corona.

Ondoeni vikwazo kusaidia COVID-19, madaktari wasemao ukweli msiwaadhibu- Bachelet

Haki za binadamu

Wakati idadi ya wagonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19 ulimwenguni ikizidi kupaa na kuwa zaidi ya 330,000 huku vifo vikifikia 14,652 Kamishna Mkuu wa haki za binadamu, Michelle Bachelet ametaka vikwazo vya kisekta duniani viondolewe ili mataifa yaweza kukabiliana na mlipuko wa virusi hivyo.

Taarifa iliyotolewa leo mjni Geneva, Uswisi na ofisi yake, imemnukuu Kamishna Mkuu Bachelet akisema kuwa vikwazo hususan katika sekta ya afya vinaweza kusababisha maambukizi na vifo zaidi na hata kusambaratisha mifumo ya afya.

“Misingi ya kibinadamu inapaswa kuzingatiwa kwenye vikwazo hivyo haraka hususan kwenye vifaa vya matibabu na dawa,”  amesema Bi. Bachelet akitolea mfano Iran ambako amesema watu wapatao 1,800 wameshafariki dunia kutokana na COVID-19 kwa sababu vikwazo vinakwamisha wao kupatiwa vifaa kama vile vivutia hewa na vifaa vya  kusaidia wahudumu wa afya kujikinga dhidi ya virusi.

Bi. Bachelet amesema zaidi ya madaktari 50 wamefariki dunia nchini Iran tangu wagonjwa wa awali wathibitishwe nchini humo wiki 5 zilizopita, “janga la Corona linasambaa nchi jirani na litakuwa na madhara kwenye mifumo ya afya kwa nchi za Pakistani na Afghanistan.”

Amegusia kuwa vikwazo vya aina mbalimbali vinaweza pia kukwamisha huduma za kitabibu dhidi ya Corona huko Cuba, Korea Kaskazini, Venezuela na Zimbabwe ambako amesema baadhi yao tayari mifumo ya afya ni dhaifu.

 Amekumbusha kuwa ni muhimu kulinda afya za watoa huduma na kwamba madaktari hawapaswi kuadhibiwa kwa kubainisha udhaifu wanaokumbana nao wanapokabiliana na janga la Corona kwa kwa wao wako mstari wa mbele kumlinda kila mtu,

Bi. Bachelet ametoa wito kwa viongozi duniani kuwa kitu kimoja akisema mshikamano wa kimaitafa ni muhimu wakati wote katika kusongesha haki za binadamu na kwamba ni muhimu katika kusongesha maslahi ya kila taifa katika kipindi cha sasa.

COVID-19 imethibitishwa katika mataifa 189.