Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za dharura dhidi ya COVID-19 zisitumike kubinya haki za binadamu: UN

Migahawa na maeneo ya burudani jijini New York zimeagizwa kufungwa kwa ajili ya kudhibiti mlipuko wa virusi vya corona.
UN News/Daniel Dickinson
Migahawa na maeneo ya burudani jijini New York zimeagizwa kufungwa kwa ajili ya kudhibiti mlipuko wa virusi vya corona.

Hatua za dharura dhidi ya COVID-19 zisitumike kubinya haki za binadamu: UN

Haki za binadamu

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamezitaka nchi kuhakikisha kwamba hawazitumii vibaya hatua za dharura za kukabiliana na mlipuko wa virusi vya Corona, COVID-19 kwa kubinya haki za binadamu.

Katika taarifa yao iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi wataalamu hao wamezitaka nchi kuepuka hatua za usalama za kubana kupindukia katika kukabiliana na milipuko wa virusi vya corona na kuwakumbusha kwamba nguvu za dharura hazipaswi kutumiwa kukandamiza haki na umoja.

“Wakati tunatambua hali mbaya na ukubwa wa mgogoro wa kiafya uliopo sasa na kutambua kwamba nguvu za dharura zinaruhisiwa na sheria za kimataifa kukabiliana na tishio kubwa kama hili, pia tunazikumbusha haraka nchi kwamba hatua zozote za dharura kukabiliana na virusi vya Corona ziende sanjari na haki za binadamu na zisiwe za nguvu kupindukia, ziwe tu zile za lazima na zisizobagua “ wameongeza wataalam hao.

Wito wao wa leo unasisitiza wito uliotolewa hivi karibuni na Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet akizitaka nchi zote kuweka hali za binadamu katika kitovu cha vita dhidi ya COVID-19 na kuhakikisha kila anayestahili kulindwa na kuhudumiwa anapata huduma hiyo bila kujali ni nani na yuko wapi.

Mlipuko wa COVID-19 ambao ulianzia China sasa umesambaa katika nchi nyingi duniani, na kukatili maisha ya maelfu ya watu.