Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mladenov apongeza ushirikiano wa Israel na Palestian kukabili COVID-19

Nickolay Mladenov, mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kwa aliji ya mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati akitoa taarifa kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
UN Photo/Eskinder Debebe)
Nickolay Mladenov, mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kwa aliji ya mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati akitoa taarifa kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Mladenov apongeza ushirikiano wa Israel na Palestian kukabili COVID-19

Afya

Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa katika mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati Nikolay Mladenov amepongeza ushirika baina ya mamlaka ya Palestina na Israel katika kukabiliana na mlipuko wa virusi vya Corona, COVID-19.

Bwana Mladenov ametoa pongezi hizo wakati wa mazungumzo kwa njia ya sim una wajumbe wengine wa kundi la pande nne la upatanishi Mashariki ya Kati lijulikanalo kama Quartet.

Kundi hilo linajumuisha Muungano wa Ulaya, Urusi, Marekani na Umoja wa Mataifa .

Katika mazungumzo hayo kwa njia ya simu yaliyofanyika alhamisi Mladenov alitoa maelezo ya kina kuhusu mpango wa Umoja wa Mataifa dhidi ya COVID-19 ukijikita Zaidi Gaza ambako kuna hatari kubwa ya kusambaa kwa ugonjwa huo.

Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa uratibu na ushirikiano ulioanzishwa baina ya Israel na Palestina kuhusu kukabiliana na COVID-19 umeelezwa kuwa ni mzuri sana.

Israel na Palestina wanaendelea kuratibu hatua zao za pamoja kwa karibu na kwa nia njema taarifa hiyo ilisema, kitu ambacho ni suala kubwa katika mafanikio ya kudhubiti ugonjwa huo hadi sasa.

Serikali ya Israel imearifu kuhusu hatua zilizoidhinishwa kudhibiti watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine na biashara, ikiwemo kufungwa kwa shule na kupiga marufuku mikusanyiko , huku waziri mkuu wa Palestina akiripotiwa kuamuru kutotembea na kutoka nje Jumapili usiku.

Takwimu za karibuni za shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO zinaonyesha kuwa kuna watu Zaidi ya 3,300 waliothibitishwa kuwa na Corona nchini Israel na Zaidi ya watu 80 kwenye eneo linalokaliwa la Palestina.

Tangu kuzuka kwa COVID-19 Israel imeruhusu kuingia kwa vifaa na bidhaa muhimu Gaza kwa mfano vifaa vya kukusanya vipimo kwa ajili ya kubaini COVID-19 na vifaa vingine vya maabara vinavyohitajika kwa ajili ya upimaji , na vifaa vya kujikinga kwa ajili ya wahudumu wa afya.

Taarifa hiyo pia imeelezea ushirikiano wa Israel katika kuruhusu wahudumu wa afya na watu wengine wanaohusika katika kukabiliana na COVID-19 kuuingia na kutoka Ukingo wa Magharibi na Gaza.