Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Palestina inahitaji dola milioni 350 kushughulikia misaada ya kibinadamu: OCHA

Mkimbizi wa Palestina akiishi kwenye makazi ya UNRWA katika Kambi ya Khan Dunoun, Syria.
UNRWA/Taghrid Mohammad
Mkimbizi wa Palestina akiishi kwenye makazi ya UNRWA katika Kambi ya Khan Dunoun, Syria.

Palestina inahitaji dola milioni 350 kushughulikia misaada ya kibinadamu: OCHA

Msaada wa Kibinadamu

Mpango mkakati wa msaada wa kibinadamu HRP wa mwaka 2019 umetoa ombi la dola milioni 350  ili kutoa huduma za msingi kama chakula, ulinzi, huduma za afya, malazi, maji na usafi kwa Wapalestina milioni 1.4 ambao wamebainika kuwa na mahitaji makubwa ya kibinadamu kwenye Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Maghariki likiwemo eneo la Jerusalem Mashariki.

Ombi hilo limezinduliwa leo mjini Ramallah na waziri wa maendeleo ya kijamii wa taifa la Palestina Dr Ibrahim Al-Shaer pamoja na  mratibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu ,OCHA wa eneo hilo Bw Jamie McGoldrick.

Waziri Al Shaer amesema  hali ya kibinadamu katika eneo hilo, inazidi kuzorota kutokana na kuendelea kukaliwa na Israel kinyume cha sheria na katika wakati ambao kuna upungufu mkubwa wa  rasilimali huku msaada wa kibinadamu ukipungua kutokana na kuingiza siasa katika masuala hayo ya misaada. Ameongeza kuwa, “ tunawasiwasi mkubwa kuhusu haki na huduma kwa watu maskini wanaohitaji msaada wa huduma za  kibinadamu.”

Kwa upande wake Bw McGoldrick, amesema hali inaendelea kuzorota katika maeneo yanayokaliwa ya wapalestina na hivyo kuwazuia  wapalestina kupata huduma za afya, maji safi pamoja, maisha ya kawaida na mahitaji mengi mengine. Ameongeza kuwa kwa wakati huo wale watoao misaada wanakabiliwa na changamoto kubwa ikiwa ni pamoja na kiwango kidogo cha ufadhili na ongezeko la mashambulizi  ili kuharamisha shughuli hizo za misaada

Kuhusu mpango huu mpya McGoldrick amesema , “Mpango wa mwaka huu ni mwelekeo mpya  ukitafakari kile ambacho tunaweza kufikia katika mazingira ya msaada finyu uliopo. Tunatambua kuwa msaada zaidi unahitajika, lakini tunahitaji kuungwa mkono na jamii ya kimataifa.”

Mpango huo wa mwaka 2019, kwa mujibu wa taarifa ya OCHA, unajumulisha miradi 203 ambayo inapashwa kutekelezwa  na mashirika 88 , yakiwemo  kitaifa 38, Mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali 37, na mashirika ya Umoja wa Mataifa 13. Pesa zinazotakiwa asilimia 77 ni kwa ajili ya Gaza. Hii ni kutokana na hali kuwa mbaya  kuanzia Machi 30 mwaka 2018 iliyosababishwa na ongezeko la idadi ya majeruhi waliyopata Wapalestina wakati wa maandamano sehemu za Gaza. Pia kuzingirwa na Israel kumezidisha adha kwa wapalestina , mgawanyiko wa kisiasa baina ya Wapalestina na ongezeko la uhasama. Kwa upande wa  Ukingo wa Magharibi, msaada  utamulika  familia zinazohitaji msaada  katika eneo la C, Jerusalem Mashariki na  eneo la H2 mjini Hebron.

 

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.