Huu ni wakati wa majadiliano, maridhiano na kutafakari:Guterres

11 Februari 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  leo amesema huu ni wakati wa majadiliano, maridhiano na kutafakari , huku akizitaka pande zote viongozi wa Israel na Palestina kuonyesha ari inayohitajika kusongesha mbele lengo la kuhakikisha amani ya kudumu, lengo ambalo jumuiya ya kimataifa lazima iliunge mkono.

Antonio Guterres ametoa wito huo leo kwenye mkutano maalum wa Baraza la Usalama kuhusu Mashariki ya Kati hususani kujadili mpango wa amani ulioainishwa na Marekani.

“Mvutano na hatari katika Ghuba imeongezeka kwa viwango vya kutatanisha. Na baada ya kuona maendeleo kadhaa ya kutia matumaini mwaka jana, leo tunashuhudia kuongezeka tena kwa machafuko huko Yemen, Syria, na hata Libya.”

Hali hii tata inasisitiza tu haja ya suluhisho la kisiasa kwa mzozo wa Israeli na Palestina, ambao umedumu kwa muda mrefu sana, na ambao unabaki kuwa muhimu kwa amani endelevu ya Mashariki ya Kati.

Msimamo wa Umoja wa Mataifa

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kusaidia katika mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati” Umoja wa Mataifa bado umeazimia kusaidia Wapalestina na Israel kusuluhisha mzozo huo kwa msingi wa maazimio husika ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na makubaliano ya nchi mbili na kutimiza maono ya kuwa nchi mbili, Israeli na Palestina kuishi pamoja kwa amani na usalama ndani ya mipaka inayotambuliwa kwa kuzingatia kwa msingi wa mistari ya kabla ya 1967.”

Mpango wa amani wa Marekani

Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati Nikolai Mladenov, ametangaza kwamba mnamo Januari 28, Marekani iliwasilisha mpango ambao Washington inaamini kuwa ndio unapaswa kuwa msingi wa mazungumzo zaidi kati ya pande hizo.

Kwa mujibu wa Bwana. Mladenov, Israeli ilikubali mpango huo, na serikali ya Palestina iliukataa. Umoja wa Mataifa ya Kiarabu, Shirika la Ushirikiano wa w anchi za  Kiislamu, na wanachama kadhaa wa Muungano wa Afrika pia walikataa kuunga mkono mpango huo wa Marekani.

Wawakilishi wa Muungano wa Ulaya walisema kwamba mpango wa Washington haufikii "vigezo vilivyoidhinishwa na jumuiya ya kimataifa".

Kulingana na Mladenov, baada ya Marekanikuweka bayana mpango wake, vurugu zilizuka katika maeneo yanayokaliwa na Ukingo wa Magharibi , pamoja na Yerusalemu ya Mashariki na Gaza.

UN Photo/Eskinder Debebe
Nickolay Mladenov, mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kwa aliji ya mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati akitoa taarifa kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

"Kuongezeka zaidi kwa machafuko na uchochezi kunaweza kuzidisha hali kuwa mbayá zaidi” amesema  mratibu huyo maalum wa Umoja wa Mataifa akiongeza kwamba "Pande zote lazima zijizuiena zilaani waziwazi  wazi vurugu, popote zinapotokea."

Hatua zisizo za busara hazitasaidia kumaliza mzozo, lakini wale ambao wanakataa mpango wa Marekani, kwa upande wao, hawapaswi kugeukia vurugu-Mladenov

Kwa mujibu wa Bwana. Mladenovu maafisa wa Israel katika kipindi hicho hicho walianza kuongea juu ya kutengwa kwa sehemu moja ya Ukingo wa Magharibi, pamoja na makazi yote ya Israeli na bonde la Jordan.

Marekani kwa mujibu wa mratibu huyo wa amani ya Mashariki ya Kati ilitangaza kuunda tume ya pamoja na Israeli kufanya kazi katika ramani iliyo na dhana zaidi ya kijiografia ambayo itaonyesha kiini cha mpango wa Marekani. "Hii itaruhusu Marekani kutambua uamuzi wa Israeli kutokana na sheria za Israeli katika maeneo fulani ya Ukingo wa Magharibi kuwa halali,"

Amekumbusha kwamba Katibu Mkuu amekua akipinga mara kwa mara hatua zisizo na nia njema na zinazoegemea upande mmoja . Kuhodhi maeneo zaidi amesema Bwana Mladenov, kutaathiri vibaya matarajio ya kutatuliwa kwa msingi wa uamuzi wa kuwa na suluhu ya mataifa mawili mawili.

Hatua za ubinafsi hazitasaidia kumaliza mzozo, lakini wale ambao wanakataa mpango wa Marekani, kwa upande wao, hawapaswi kugeukia vurugu, " mratibu maalum amesisitiza.

Pia amesema matumaini yake ni kuwa "Baraza la Usalama litajiunga na wito wa Katibu Mkuu kwa suluhisho linalokubaliwa kwa pande zote katika mzozo na mazungumzo kati ya pande hizo mbili."

UN Photo/Eskinder Debebe
Mahmoud Abbas, Rais wa Palestina akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa mkutano kuhusu Mashariki ya Kati.

Palestina

Kwa upande wake Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, amesema katika hotuba yake kwamba kukataliwa kwa kwa kiasi kikubwa kwa mpango huu ni kwa sababu ya hatua zisizo na haki zilizomo na "ukiukwaji wake wa wazi wa uhalali wa kimataifa, na kwa sababu unakataa madai ya Wapalestina ya haki yao halali ya uhuru na kujitawala katika taifa lao, na kuhalalisha kisicho halali  kuanzia makazi ya walowezi, na uporaji wa ardhi na kuhodhi ardhi ya Palestina. "

Ameongeza kuwa mpango wa Marekani ni kupora makazi zaidi na utawala wa ubaguzi wa zamani.

UN Photo/Evan Schneider
Balozi wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa Danny Danon akihutubia Baraza la Usalama wakati wa kikao kuhusu Mashariki ya Kati

Israel

Naye Balozi wa Isarel katika Umoja wa Mataifa Danny Danon  katika hotuba yake kwa Baraza la Usalama, amesema kuwa mpango huo wa Marekani unakuwa ni mwanzo wa mazungumzo na unachukuliwa kuwa msingi wa mazungumzo. Danon amemshutumu Rais wa Palestina kwa kukataa kujadili, akisema, "Abbas anakataa kujadili na hafurahii suluhisho la kweli la mzozo huo. Maendeleo kuelekea amani hayatapatikana endapo Rais Abbas atabaki madarakani. Wakati Rais Abbas ataondoka madarakani. , watu wa mataifa haya mawili wanaweza kusonga mbele. "

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud