Mchakato umekwama Mashariki ya Kati, ghasia zashamiri, amani mashakani- Mladenov

27 Agosti 2019

Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa kwenye mchakato wa amani Mashariki ya Kati, Nickolay Mladenov ameonya kuwa hatua za haraka zinahitajika ili kurejesha mchakato wa amani kwenye eneo hilo kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa huku akitoa wito kwa viongozi wa pande zote za Israel na Palestina kuchukulia hatua makundi yenye misimamo mikali.

Bwana Mladenov amesema hayo wakati wa hotuba yake ya kila mwezi kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo jijini New York, Marekani wakati huu ambapo kipindi cha mwezi mmoja uliopita kimeshuhudia mvutano mkubwa kwenye Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan na Ukanda wa Gaza.

“Nina wasiwasi kwamba ni lazima nianze hotuba yangu kwa kujikita katika ongezekola ghasia kwenye Ukanda wa Gaza na Ukingo wa magharibi wa mto Jordan na tishio lake kwenye kuzorota kwa usalama katika ukanda huo wa Mashariki ya Kati.Vyote vinatokea huku mchakato wa kisiasa ukiwa umekwama na hakuna mwelekeo wa kufufua,” amesema Bwana Mladenov.

Akifafanua mivutano hiyo, Bwana Mladenov ametaja masuala ya ubomoaji wa makazi, ujenzi wa makazi mapya, ghasia na kudorora kwa huduma za afya akisema hali inakuwa mbaya kila uchao.

Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan hali si shwari

“Tarehe 8 Agosti, raia wa Israeli mwenye umri wa miaka 19 aliuawa Ukingo wa Magharibi baada ya kuchomwa kisu karibu na makazi ya Migdal Oz. Watuhumiwa wawili wa kipalestina walikamatwa baadaye na jeshi la Israeli. Tarehe 15 Agosti, watoto wawili wa kipalestina walimchoma kisu afisa wa polisi wa Israe mjini Yerusalem. Mmoja wao watoto hao alipigwa risasi na kufariki dunia,” amesema Mladenov.

Amesema kwa ujumla mwezi uliopita huko Ukingo wa Magharibi na Yerusalem Mashariki, wapalestina wawili na waisraeli wawili waliuawa na takribani wapalestina 102 walijeruhiwa huku kwa upande wa Israel majeruhi ni 7.

“Kwa dhahiri kabisa, nalaani mashambulio dhidi ya wapalestina na waisraeli. Mashambulizi ya aina hii ni ya kiuoga na hatari na yananufaisha wale tu wanaotaka amani izidi kuzorota,” amesema mratibu huyo maalum.

Nickolay Mladenov, Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa katika mchakato wa amani Mashariki ya Kati akihutubia Baraza la Usalama kwa njia ya video kuhusu hali kwenye ukanda huo. (27th August 2019)
UN Photo/Eskinder Debebe)
Nickolay Mladenov, Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa katika mchakato wa amani Mashariki ya Kati akihutubia Baraza la Usalama kwa njia ya video kuhusu hali kwenye ukanda huo. (27th August 2019)

Ukanda wa Gaza nako japo kuna utulivu lakini si salama

Bwana Mladenov amesema kwa upande wa Gaza, kwa miezi miwili iliyopita kumekuwepo na utulivu kiasi licha ya matukio ya ghasia kuendelea.

“Katika kipindi hiki tunachoripoti, hali imeendelea kuwa tete ambapo maroketi mawili na makombora yalirushwa kutoka Gaza na kuelekzwa Israeli. Takribani yote yalikingwa na mawili yalitua kwenye mji wa Sderot nchini Israel tarehe 17 na 25 ya mwezi huu wa Agosti’” ameema Mladenov.

Mratibu huyo amesema makombora hayo yalisababisha uharibifu na “kutokana na hali hiyo, jana Israel iliamua kupunguza kwa muda kwa asilimia 50 upelekaji wa mafuta huko Gaza. Uamuzi huu tayari umesababisha uhaba wa nishati hiyo ya mafuta Gaza.”

Kuhusu urushaji wa vishada vyenye moto na Maputo kutoka Gaza kuelekea upande wa pili, Bwana Mladenov amesema kulikuwepo na matukio 7, ingawa ametoa wito kwa Israel kuacha kutumia silaha za moto akisema silaha hizo zitumike tu pale ambapo hakuna njia nyingine.

Halikadhalika ametaka kikundi cha Hamas nacho kiache urushaji holela wa makombora kuelekea Israel akisema ni lazika kihakikishe kuwa maandamano yoyote yanayofanyika kwenye uzio Gaza yanakuwa ya amani na hayana uchochezi wowote.

Akihitimisha hotuba yake, Mladenov amerejelea wito wake kuwa, “hatua za dhati zinawezekana, na lazima zichukuliwe kubadili mwelekeo wa hali ya sasa wa mvutano kati ya Israel na Palestina.”

Amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake umeazimia kusaidia wapalestina na waisrael kutatua mzozo kati yao kwa msingi wa sheria za kimataifa, mazimio ya Umoja wa Mataifa na makubaliano ya awali na kufanikisha dira ya kuwepo kwa mataifa mawili ya Israeli na Palestina yanayoishi kwa amani.

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter