Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yatoa dola milioni 15 za kimarekani kukabiliana na COVID-19

Hapa ni nchini China, mhudumu akiacha kifurushi nje ya nyumba kwa kuwa hawaruhusiwi kuingia kwenye majengo kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona nchini humo.
Man Yi
Hapa ni nchini China, mhudumu akiacha kifurushi nje ya nyumba kwa kuwa hawaruhusiwi kuingia kwenye majengo kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona nchini humo.

UN yatoa dola milioni 15 za kimarekani kukabiliana na COVID-19

Afya

Umoja wa Mataifa kupitia ofisi yake ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA umetoa dola milioni 15 za kimarekani kutoka katika mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF ili zisaidie juhudi za ulimwengu kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa wa COVID-19, hususani katika nchi zenye mfumo duni wa huduma za afya.

Umoja wa mataifa katika taarifa yake iliyotolewa leo jumapili umesema kuwa fedha hizo zitatumiwa na shirika la afya duniani WHO na lile la kuhudumia watoto UNICEF ili kufanya shughuli muhimu kama vile kufuatilia kusambaa kwa virusi, kufuatilia visa na kuendesha maabara za taifa katika mataifa mbalimbali.

Bado tunayo nafasi ya kuvidhibiti virusi

Vile vile kupitia taarifa hiyo, mratibu wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa Mark Lowcock amesema dunia haijachelewa kuudhibiti ugonjwa wa COVID-19“hatuoni ushahidi bado kuwa virusi hivi vinaweza kusambaa tu hewani. Bado tunayo nafasi ya kuudhibiti ugonjwa huu.”

Hata hivyo bwana Lowcock ametahadharisha kuwa “hatua madhubuti zinatakiwa kuchukuliwa kutambua mapema visa vipya” na akaongeza, “kuwaweka wagonjwa mahali na kuwahudumia kisha kufuatilia waliokutana nao. Tunatakiwa kuchukua hatua hivi sasa kuzuia virusi hivi visiendelee kuyaweka maisha zaidi hatarini.”

Mamilioni ya maisha yanaweza kuokolewa

Mchango huo wa dharura utazisaidia nchi ambazo zina mifumo tete ya kiafya ili kuongeza nguvu za kutambua na kuchukua hatua, amesema Bwana Lowcock akifafanua kuwa fedha hizo zinaweza kuokoa maisha ya mamilioni ya watu walioko hatarini.

Tweet URL

 

Uwezekano wa kusambaa kwa virusi katika nchi ambazo zina mifumo duni ya afya ni moja ya mambo ya msingi ambayo WHO inayaangalia kwa jicho la karibu hivi sasa.

Akiukaribisha mchango huo, mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghereyesus, kupitia mtandao wa Twitter amesema, watasaidia nchi zilizoko hatarini kuwalinda wafanyakazi walioko mstari wa mbele na pia kuwatibu kwa dhati wagonjwa. WHO bado inatoa wito wa kupata dola milioni 675 ili kukabiliana na mapambano dhidi ya virusi vya corona.

Tweet URL

 

Kwa upande wa UNICEF, itatumia mgao itakaoupata katika kuwaelimisha watoto, wajawazito na familia kuhusu namna ya kujikinga, ameeleza Mkuu wa shirika hilo Bi Henrietta Fore akisisitiza kuwa, “katika wakati huu muhimu, kila juhudi inatakiwa kufanywa ili kuudhibiti mlipuko wa ugonjwa.”

Nchi tano mpya zimetangazwa kukumbwa na corona

Azerbaijan, Ecuador, Ireland, Monaco na Qatar zimetangazwa kupitia katika ripoti ya kila siku ya WHO kuhusu virusi vya corona kuwa nazo zimeathirika na ugonjwa huo na hivyo kuzifanya nchi zilizokumbwa na COVID-19 kufikia 58 kote ulimwenguni. Duniani kote, katika siku mbili za jumamosi na jumapili hii vimeripotiwa visa vipya 1739.