Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Unyonyeshaji kwa ajili ya dunia enye afya:UNICEF/WHO

Kikundi cha wanawake cha kuonyeshana mshikamano katika unyonyeshaji wa watoto wao.
UN
Kikundi cha wanawake cha kuonyeshana mshikamano katika unyonyeshaji wa watoto wao.

Unyonyeshaji kwa ajili ya dunia enye afya:UNICEF/WHO

Afya

Wiki ya unyonyeshaji duniani imeanza Agosti Mosi huku Umoja wa Mataifa ukizitaka jamii zote kila mahali “kuunga mkono unyonyeshaji kwa ajili ya kuwa na dunia yenye afya.” 

Mashirika ya Umoja wa Mataifa la afya duniani WHO na lile la kuhudumia watoto UNICEF yametoa wito wa Pamoja kwa serikali kulinda na kuchagiza fursa za kupata ushauri nasaha kuhusu unyonyeshaji ambao ni kiungo muhimu cha msaada katika unyonyeshaji. 

Umoja wa Mataifa kwa muda mrefu umekuwa ukipigia upatu faida za unyonyeshaji ambazo zinaleta afya, lishe na faida za kihisia kwa Watoto na kina mama. Pia unyonyeshaji unasaidia mfumo endelevu wa chakula kwa watoto. 

“Wakati unyonyeshaji ni mchakato wa asili lakini sio rahisi wakati wote” amesema mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore, na mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus katika taarifa hiyo ya pamoja ameongeza kuwa “Kina mama wanahitaji msaada ili kuanza kunyonyesha na katika kunedelea kunyonyesha.” 

Unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa watoto huokoa uhai wa watoto 820,000 kila mwaka wenye umri wa chini ya miaka 5
UN
Unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa watoto huokoa uhai wa watoto 820,000 kila mwaka wenye umri wa chini ya miaka 5

Huduma za ushauri nasaha 

Viongozi hao wawili wamesema kwamba huduma za kitaalam za ushauri nasaha zinaweza kuhakikisha kina mama pamoja na familia wanapata msaada, taarifa, ushauri na hakikisho wanalohitaji kuwanawirisha watoto wao kwa njia bora. 

Viongozi hao wameongeza kuwa “Ushauri nasaha katika suala la unyonyeshaji unaweza kuwasaidia kina mama kujiamini huku wakiheshimu mazingira yao na chaguo lao. Ushauri nasaha unaweza kuwawezesha wanawake kukabili changamoto na kuzuia ulishaji na hulka ambazo zinaweza kuingilia unyonyeshaji wa matoto wao, mfano kuwapa vyakula vya majimaji visivyo vya lazima, chakula cha kawaida na mbadala wa maziwa ya mama kwa watoto wachanga na watoto wadogo.” 

Wamesisitiza kwamba kuboresha fursa za ushauri nasaha wa kitaalam kunaweza pia kuongeza muda wa kunyonyesha Watoto na kuchagiza unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee ambao una faida kuwa kwa watoto, familia na uchumi. 

Mama akimnyonyesha mwanae huko Ukraine wakati wa warsha mahsusi ya unyonyeshaji watoto wakati wa dharura, warsha iliyoandaliwa na UNICEF. (2015)
UNICEF/Zavalnyuk
Mama akimnyonyesha mwanae huko Ukraine wakati wa warsha mahsusi ya unyonyeshaji watoto wakati wa dharura, warsha iliyoandaliwa na UNICEF. (2015)

Maisha 820,000ya watoto yaweza kuokolewa 

Kwa mujibu wa UNICEF na WHO “Tathimini inaonyesha kwamba ongezeko la kiwango cha unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee linaweza kuokoa maisha ya watoto 820,000 kila mwakana na hivyo kuzalisha pato zaidi la dola bilioni 302.” 

Yamesema aina mbalimbali za wataalam wa afya wanaweza kutoa msaada wa kitaalm unaohitajika kama vile washauri wa unyonyeshaji katika mazingira ya kliniki au kwa kuwatembelea kina mama majumbani au kuwa program za jamii zitakazowasaidia watu moja kwa moja au kwa nia ya mtandao. 

Ubunifu wakati wa janga la COVID-19 

UNICEF na WHO yamesema wakati wa janga la COVID-19 ni muhimu hata zaidi kusaka suluhu bunifu ili kuhakikisha kwamba fursa ya kupata huduma hizi muhimu haiingiliwi na kwamba familia zinaendelea kupata ushauri nasaha kuhusu unyonyeshaji ambao zinauhitaji. 

Lucy Atokoru, 28 ananyonyesha mtoto wake nyumbani kwake Omugo, Wilaya ya Arua.
© UNICEF/Zahara Abdul
Lucy Atokoru, 28 ananyonyesha mtoto wake nyumbani kwake Omugo, Wilaya ya Arua.

Wakati huu wa janga la COVID-19 UNICEF na WHO kwa muji wa sera za kuchukua hatua za kimataifa kwa ajili ya kuchagiza unyonyeshaji wanatoa wito kwa serikali : 

KUWEKEZA: ili kuhakikisha kuna wataalam wa utoaji ushauri nasaha kuhusu unyonyeshaji na wanapatokana kwa kila mwanamke. Na hilo linahitaji kuongeza ufadhili wa program za unyonyeshaji  na kuboresha mfumo wa ufuatiliaji na utekelezaji wa sera , mipango na huduma. 

MAFUNZO: Kuwapa mafunzo wahudumu wa afya wakiwemi wakunga na wauguzi ili waweze kutoa ushauri nasaha wa kilaam kuhusu unyonyeshaji kwa kina mama na familia. 

Mwanamke akimnyonyesha mtoto wake mchanga katika hospitali mjini Belgrade Serbia
UNICEF/NYHQ2011-1166/Holt
Mwanamke akimnyonyesha mtoto wake mchanga katika hospitali mjini Belgrade Serbia

KUHAKIKISHA: Kwamba ushauri nasaa unapatikana kama sehemu ya utaratibu wa kila siku wa huduma za afya na lishe ambazo zinapatikana kwa utahisi. 

UBIA: Na ushirikiano na asasi za kiraia  na jumuiya za wataalam wa afya , kujenga mifumo imara ya ushirikiano kwa ajili ya kutoa ushauri nasaha unaostahili. 

KULINDA: wahudumu wa afya dhidi ya ushawishi wa sekta ya vyakula vya watoto. 

Bi. Fore na Dkt. Tedros wamehitimisha ujumbe wao kwa wito maalum wa kuungana kuchukua hatua kwa niaba ya kina mama na watoto, “Kwa Pamoja kupitia ahadi, hatua za pamoja na ushirikiano tunaweza kuhakikisha kwamba kila mama ana fursa ya kupata ushauri nasaha wa kitaalam, kumwezesha ili kumpa mtoto wake mwanzo bora zaidi wa maisha.”