Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CERF yatoa dola milioni 3 kusaidia waathirika wa mafuko Kenya:UN

Mafuriko makubwa katika eneo la pembe ya Afrika na Kenya yamesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ikiwemo barabara.
UN Photos
Mafuriko makubwa katika eneo la pembe ya Afrika na Kenya yamesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ikiwemo barabara.

CERF yatoa dola milioni 3 kusaidia waathirika wa mafuko Kenya:UN

Msaada wa Kibinadamu

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA, Mark Lowcock leo ametangaza kwamba mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF umetenga dola milioni 3 kama mchango wa kuwasaidia waathirika wa mafuriko, maporomoko ya ardhi na maporomoko ya udongo nchini Kenya.

Kwa mujibu wa mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya Siddharth Chatterjee, fedha hizo zimetengwa kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchi nzima Kenya tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba na kusababisha mafuriko yaliyoleta madhara makubwa na kwamba

"Fedha hizi zitaruhusu mashirikika ya misaada ya kibinadamu kupeleka haraka msaada wamuhinmu wa chakula na mahitaji mengine ya maisha, malazi, na huduma za afya kwa wasiojiweza kwenye maeneo yaliyoathirika zaidi, wakiwemo watoto, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.”

Miongoni mwa uharibifu uliosababishwa na mafuriko hayo ni pamoja na kusambaratisha miundombonu ikiwemo nyumba, vituo vya afya na shule, kuwatawanya idadi kubwa isiyojulikana ya watu na kuvuruga huduma za msingi katika kauti 32 kati ya 47 za nchi hiyo.

Barabara na madaraja pia vimeharibiwa na hivyo kusababisha changamoto kubwa kwa juhudi za wahudumu wa misaada ya kibinadamu kufika katika maeneo yaliyoathirika.

Bwana Chatterjee amesema “Mvua hizo kubwa pia zimeharibu maelfu ya ekari za rdhi ya kilimo ukizingatia kwamba nchi hii tayari ilikuwa inakabiliwa ongezeko la njaa, ikikadiriwa kuwa watu milioni 3.1 watakuwa katika mgogoro mkubwa wa kutokuwa na uhakika wa chakula. Tunaishukuru sana CERF kwa mchango huu muhimu na uliokuja wakati muafaka  na nawaomba wahisani wengine kusaidia shughuli hizi’ pia’.

Mbali ya kutoa msaada wa chakula, malazi, msaada wa kiufundi fedha hizo zitatumika kuboresha fursa ya upatikanaji wa maji salama ya kunywa , kwa kukarabati mifumo ya maji iliyoharibiwa na mafuriko  na kwa kuchagiza kaya kuweka dawa kwenye maji  na kuyahifadhi, pamoja na kuchagiza kampeni za usafi ili kuzuia magonjwa ya mlipuko yatokanayo na maji machafu.

Kenya imekuwa ikikabiliwa na milipuko ya magonjwa mbalimbali mwaka huu wa 2019 ikiwemo kipindupindu, homa ya dengue na homa ya bonde la ufa. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayopokea fedha hizo ni pamoja na la chakula na kilimo FAO, la uhamiaji, IOM, la kuhudumia Watoto UNICEF, la mpango wa chakula WFP, la afya WHO na la idadi ya watu duniani UNFPA.