Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila nchi lazima ifanye kila iwezalo kujiandaa dhidi ya COVID19:UN

Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus wakipata taarifa kuhusu kituo cha operesheni za kimkakati dhidi ya virusi vya Corona huko Geneva, USwisi.
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus wakipata taarifa kuhusu kituo cha operesheni za kimkakati dhidi ya virusi vya Corona huko Geneva, USwisi.

Kila nchi lazima ifanye kila iwezalo kujiandaa dhidi ya COVID19:UN

Afya

Umoja wa Mataifa umeitaka kila nchi kote duniani kufanya kila liwezekanalo ili kujiandaa endapo mlipuko wa virusi vya Corona COVID19 utazuka.

Akizungumza kwenye mkutano wa pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema huu ni wakati wa kila nchi kuchukua hatua kujiandaa na mlipuko wa ugonjwa wa Corona ambao kwas asa umekuwa ni “dharura ya kimataifa ya afya ya umma” .

Dkt Tedros amesisitiza kwamba “Kila nchi lazima ifanye tathimini yake binafsi ya hatari, WHO pia inaendelea kufanya tathimini yake ya hatari na inafuatilia mwenendo wa mlipuko huo kila saa. Lakini kuna vipumbele vitatu mosi kila nchi lazima itoe kipaumbele katika kuwalinda wahudumu wa afya, pili ni lazima tushirikishe watu na jamii hususani walio katika hatari ya mlipuko wa magonjwa hususani wazee na watu walio na maradhi mengine tayari na tatu ni lazima tuzilindew nchi ambazo hazijiwezi kwa kuhakikisha tunazisaidia kukabiliana na mlipuko”

Amesisitiza kuwa huu ni wakati kwa nchi, jamii , familia na watu binafsi kujikita katika kujiandaa,”hatuishi katika dunia ambayo iko wazi kwa kila kitu, na si ama hili au lile, ni lazima tujikite na kuudhibiti huku tukifanya kila tuwezalo kujiandaa na uwezekano wa zahma kubwa.”

Na katika maandalizi hayo amesema hakuna mtazamo mmoja ambao utaweza kuwa suluhu kwa wote.

 Je hili ni zahma ya kimataifa ama la ?

Kuhusu endapo mlipuko huu wa COVID19 ambao mkuu huyo wa WHO amesema kwa China pekee kufikia asubuhi ya leo umesababisha visa 77,362 na vifo 2618 na nje ya China visa 274 na vifo 23 katika nchi 28 ,kuwa ni zahma ya kimataifa ama la, Dkt. Tedross amesema bado haujafikia kiwango cha kuwa zahma ya kimataifa kwani hadi ugonjwa kufikia hatua hiyo ni lazima uwe umesambaa kwa kiasi kikubwa duniani kote na kwa kasi, hivyo mesisitiza kwamba kwa sasa ni ‘’dharura ya kimataifa ya afya ya umma’’ japo ameongeza kuwa uwezekano wa mlipuko huo kuwa zahma ya kimataifa upo. ‘’uamuzi wetu umetokana na tathimini inayoendelea ya kusambaa kwa mlipuko huu katika maeneo mbalimbali , ukubwa wa ugonjwa huo na athari unazosababisha kwa jamii nzima. Kwas asa hatushuhudii kusambaa kimataifa ambako hakuwezo kudhibitiwa na hatushuhudii kiwango kikubwa cha ugonjwa huo na vifo ‘’

Matumaini ya kudhibiti COVID19

Dkt. Tedros amesema kuna matumaini kwamba mlipuko huo unaweza kudhibitiwa kwani kwa sasa idadi ya visa inaendelea kushuka hasa nchini China. Pia amesema jopo la wataalam wa WHO na China limekamilisha  ziara na kuwasilisha ripoti ya kile ilichokibaini nchini humo kuhusu ukubwa wa ugonjwa huo, athari zake na hatua zinazochukuliwa ikiwemo katika jimbo la Wuhan na kutoa mapendekezo kadhaa.

Timu hiyo imebaini kwamba maambukizi makubwa na hali mbaya ilikuwa kati ya Januari 23 na Februari Pili na tangu hapo kasi ya maambukizi inashuka. Pia timu imebaini kwamba hakuna mabadiliko makubwa katika viasili nasaba (DNA) vya virusi hivyo, na kwamba kiwango cha vifo Wuhan ni kati ya asilimia 2 na 4 na asilimia 0.7 nje ya Wuhan.

Timu hiyo imebaini pia kwamba kwa watu ambao hawajaathirika sana na ugonjwa huo muda wa kupona ni takribani wiki mbili na wale walio mahtuti ni kati ya wiki tatu hadi sita.

Timu hiyo ambayo imetoa mapendekezo 22 pia inakadiria kwamba hatua zilizochukuliwa na Uchina zimesaidia kuepusha idadi kubwa ya visa.

Utakuwa ni upuuzi mkubwa kutofadhi WHO

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akisistiza katika maandalizi amesema ni muhimu kusema kwamba nchi zote na sio Uchina pekee yake akimaanisha nchi zote ‘’zinapaswa kufanya kila liwezekanalo kujiandaa huku zikiheshini kanuni za kutokubagua , unyanyapaa na kuheshimu haki za binadamu  na kufanya kila wawezalo kudhibiti ugonjwa huo, kwani bado inawezeka kuudhibiti hugonjwa huo, lakini endapo baadhi watashindwa basi mlipuko huu unauwezekano wa kuwa janga kubwa lenye athari mbaya kwa afya ya kimataifa na uchumi wa kimataifa. ‘’

Hivyo ametoa wito na kusisitiza nchi zote duniani kutimiza wajibu wao katika hili wakitambua kwamba wanaweza kuitegemea WHO kuwasaidia katika juhudi hizo.

 Ufadhili wa kukabiliana na mlipuko wa COVID 19

Na alipoulizwa kuhusu kusuasua kwa ufadhili na umuhimu wa ufadhili huo kwa WHO ili kukabiliana na mlipuko wa virusi hivyo vya Corona Guterres amesema ‘’kama kuna jambo la upuuzi zaidi la kufanya katika dunia ya sasa ni kutofadhili kikamilifu maombi ya WHO, kwa sababu maombi ya WHO ni muhimu katika kusaidia nchi wanachama ili kuepuka magonja ambayo ni makubwa ya mlipuko kuwa jinamizi la kimataifa. Ombi langu kwa wahisani wote ni kuhakikisha ombi la WHo kuhusu mlipuko huu na mingineyo yanafadhiliwa kikamilifu.