Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaingiwa hofu na mwenendo wa maambukizi ya virusi vya Corona, COVID-19

Maafisa huko Shenzhen nchini China wakiwa katika majukumu  yao ya kawaida ya kufuatilia wagonjwa wa virusi vya Corona
Man Yi
Maafisa huko Shenzhen nchini China wakiwa katika majukumu yao ya kawaida ya kufuatilia wagonjwa wa virusi vya Corona

WHO yaingiwa hofu na mwenendo wa maambukizi ya virusi vya Corona, COVID-19

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO, limesema hofya yake hivi sasa juu ya kuenea kwa virusi vya Corona, COVID-19 ni kutokuwa na taarifa za wazi kuhusu uhusiano wa kuenea kwa virusi hivyo, kama vile historia ya mtu kusafiri China au kuwa na mawasiliano na mtu aliyethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema hayo leo akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi wakati huu inapoelezwa kuwa taifa lenye wagonjwa wengi zaidi wa virusi vya Corona baada ya China ni Korea Kusini.

Dkt. Tedros amesema zaidi ya meli ya kifahari ya abiria ya Diamond Princess iliyopita Korea Kusini, taifa hilo sasa lina idadi kubwa ya wagonjwa kando ya China, na hivyo wanashirikiana na serikali ya taifa hilo kuelewa mzunguko wa maambukizi uliosababisha ongezeko la maambukizi.

“Tuna wasiwasi pia juu ya ongezeko la wagonjwa wa Corona nchini Iran ambako sasa kuna wagonjwa 18 huku wengine wanne wamefariki dunia katika siku mbili tu zilizopita,”  amesema Dkt. Tedros.

Kwa  upande wake Sylvie Briand wa WHO amesisitiza kuwa, “ni kweli tunaona hali inavyokuwa. Si tu kwamba idadi ya wagonjwa inaongezeka bali pia tunashuhudia mwelekeo tofauti wa njia za maambukizi katika maeneo mbalimbali.”

Kuhusu mgonjwa aliyebainika Lebanon, afisa wa WHO, Jaouad Mahjour amesema mgonjwa huyo aligundulika kwenye uwanja wa ndege kwa sababu walikuwa wanachunguza wasafiri kutoka Iran iwapo wana dalili za virusi vya Corona na ndipo mgonjwa akagundulika.

Nayo ofisi ya WHO mjini Cairo, Misri hivi sasa ina mawasiliano na Iran na Lebanon kutathmini hali ilivoy na kisha kubaini aina ya msaada unaohitajika iwapo nchi hizo zitahitaji.

Kwa  mantiki hiyo Dkt. Tedros amesema wanachoamini kuna fursa ya kuchukua hatua, lakini fursa hiyo inazidi kuwa finyu na ndio maana, “tunatoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua. Na ndio maana nilieleza jana kuwa, na nawaeleza ninyi, jamii ya kimataifa ichukue hatua  haraka, ikiwemo kutoa fedha ambazo sasa hivi naona hazipo.”