Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19: Sasa ni wakati wa busara si kupagawa na sayansi na si unyanyapaa - Guterres

Hofu ya kuenea kwa virusi vya Corona vimesababisha bidhaa madukani kununuliwa kwa kasi kubwa watu wakijiandaa kusalia nyumbani.  Pichani ni kwenye duka moja kubwa jijini New York, Marekani.
UN News/Beatriz Barral
Hofu ya kuenea kwa virusi vya Corona vimesababisha bidhaa madukani kununuliwa kwa kasi kubwa watu wakijiandaa kusalia nyumbani. Pichani ni kwenye duka moja kubwa jijini New York, Marekani.

COVID-19: Sasa ni wakati wa busara si kupagawa na sayansi na si unyanyapaa - Guterres

Afya

Shaka na shuku zikiendelea kugonga vichwa vya wakazi wa dunia hii wakati  huu wa kusambaa kwa virusi vya Corona, au COVID-19, Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema huu ni wakati wa busara na sio kupagawa, wakati wa sayansi na sio unyanyapaa na zaidi ya yote ni wakati wa ukweli na si hofu.

Guterres amesema hayo leo kupitia ujumbe wake aliotoa kwa njia ya video kwa wakazi wa dunia hii akisema kuwa “tunakabiliwa na tishio lisilo la kawaida la kiafya tofauti na lingine lolote katika wakati wetu. Wakati huohuo virusi vinasambaa, hatari inaongezeka na mifumo yetu ya afya, uchumi na maisha yetu ya kila siku yako katika majaribu makubwa.

Katibu Mkuu amesema walio hatarini zaidi ndio wanaoathiriwa zaidi akitaja wazee na wale walio tayari na matatizo ya kiafya, wale wasio na huduma bora za afya na wale walio kwenye umasikini au wanaoishi pembezoni.

Amesema athari za kijamii na kiuchumi kutokana na mchanganyiko wa janga la mlipuko na kudorora kwa uchimi vitaathiri watu wengi kwa miezi kadhaa, lakini kusambaa kwa virusi kutashika kasi na uchumi nao baadaye utatengamaa.

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema kuwa “ijapokuwa hali hii imeelezwa kama janga la kimataifa , ni hali ambayo tunaweza kuidhibiti. Tunaweza kuzuia kasi ya kusambaa, kuzia maambukizi na kuokoa maisha.Lakini hiyo itahihaji hatua madhubuti binafsi, za kitaifa na kimataifa. Tunatakiwa kutangaza vita dhidi ya virusi hivi.”

Amefafanua kuwa tamko hilo linamaanisha kuwa nchi zina wajibu wa kujipanga, kuongeza juhudi na kuzidisha hatua na zaidi ya yote ni kwa kutekeleza mikakati madhubuti ya kuvidhibiti na kwa kuzindua na kuboresha mifumo ya kukabiliana na dharura.

Halikadhalika amesema vita dhidi ya COVID-19 vifanyike “kwa kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa upimaji na kuhudumia wagonjwa, kwa kuweka mazingira bora hospitali, kuhakikisha zina nafasi, vifaa na wahudumu wanaohitajika na kwa kuanzisha hatua za kitabibu za kuokoa maisha.

Mkazi wa jiji la New York, nchini Marekani akiwa amevaa barakoa kujikinga dhidi ya virusi vya Corona, COVID-19.
UN Photo/Loey Felipe
Mkazi wa jiji la New York, nchini Marekani akiwa amevaa barakoa kujikinga dhidi ya virusi vya Corona, COVID-19.

Kila mtu ana wajibu

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema hata hivoy, “nasi sote tuna wajibu wa kutimiza. Kwa kuzingatia ushauri wa kitabibu na kuchukua hatua. Hatua rahisi za zilizopendekezwa na mamlaka za afya.”

Si afya tu bali pia uchumi  umetikiswa; COVID-19 kugharimu dunia dola trilioni 1

Guterres amegeukia pia uchumi akisema kuwa mbali ya COVID-19 kuwa ni mgogoro wa afya ya umma , virusi vinaathiri pia uchumi wa dunia kwa kuwa, “masoko ya fedha duniani yameporomoka vibaya na hali ya sintofahamu. Mnyororo wa usambazaji duniani umeathirika.  Uwekezaji na mahitaji ya watumiaji vimeathirika huku kukiwa na hatari bayana ya kutumbukia kwenye mdororo wa uchumi ulimwenguni.”

Amesema kuwa wachumi wa Umoja wa Mataifa wanakadiria kwamba virusi hivyo vinaweza kugharimu uchumi wa ulimwengu angalau dola trilioni 1 mwaka huu na pengine zaidi.

Mshikamano unahitajika sasa

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa hakuna nchi inayoweza kukabili hili peke yake.

“Sasa kuliko wakati mwingine wowote serikali zinapaswa kushirikiana kufufua uchumi , kupanua wigo wa uwekezaji wa umma, kukuza biashara na kuhakikisha msaada unaolengwa kwa wat una jamii zilizoathiriwa zaidina ugonjwa huu au zilizo katika hatari zaidi ya athari mbaya za kiuchumi wakiwemo wanawake ambao mara nyingi hubeba mzigo mkubwa wa kazi ngumu ya kutoa huduma,” amesema Bwana Guterres.

Amesisitiza kuwa janga la virusi vya Corona “linarejesha nyumbani umoja wetu ambao ni muhimu katika familia ya ubinadamu wetu.Kuzuia kuenea zaidi kwa COVID-19 ni jukumu letu zote kwa pamoja.

Kwa  upande wa chombo anachoongoza Katibu Mkuu Guterres amesema, “Umoja wa Mataifa likiwemo shirika la afya duniani umejipanga kikamilifu. Kama sehemu ya familia yetu ya kibinadamu tunafanyakazi saa 24/7 na serikali ili kutoa muongozo wa kimataifa kuusaidia ulimwengu kuchukua hatua za kukabili tishio hili.Tuko pamoja nawe katika mshikamano huu.  Tuko pamoja katika hili, na tutalikabili hili kwa pamoja.