Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifo vya corona vyazidi 1000, WHO yaitisha jukwaa la utafiti na ubunifu

Wafanyakazi wakichunugza joto ya mwili ya wateja kwenye duka la bidhaa Yangon, Myanmar.
Man Yi
Wafanyakazi wakichunugza joto ya mwili ya wateja kwenye duka la bidhaa Yangon, Myanmar.

Vifo vya corona vyazidi 1000, WHO yaitisha jukwaa la utafiti na ubunifu

Afya

Shirika la afya duniani WHO linaendesha jukwaa la utafiti na ubunifu ili kuchukua hatua za kimataifa kushughulikia ,mlipuko wa virusi vya corona yaani COVID-2019 ambapo hadi sasa watu 42,000 wameambukizwa na tayari vifo vimefikia zaidi ya 1000.

“Ni vigumu kuamini kuwa miezi miwili iliyopita, virusi hivi ambavyo vimeteka vyombo vya habari, masoko ya uchumi na viongozi wa kisiasa, tulikuwa hatufifahamu kabisa.” Ameeleza Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus katika hotuba yake ya ufunguzi.

Jukwaa hilo ambalo linafanyika kwa siku mbili kuanzia leo tarehe 11 na kesho 12 mwezi huu wa Februari mjini Geniva Uswisi, limeandaliwa kwa ushirikiano wa muungano wa taasisi ya GloPID-R ambao ni wafadhili wa tafiti kuhusu utayari wa magonjwa ya kuambukiza.

Jukwaa hilo litawaleta pamoja wadau muhimu wakiwemo wanasayansi nguli pamoja na taasisi zaa afya ya jamii, mawaziri wa afya na wafadhili wa tafiti wanaofuatilia ugonjwaa wa corona, afya ya Wanyama na afya ya umma pamoja na maendeleo ya chanjo, tiba na utambuzi wa magonjwa, miongoni mwa uvumbuzi mwingine.

Washiriki watajadili maeneo kadhaa ya utafiti ikiwemo kutambua chanzo cha virusi hivi, pia kupeana taarifa za sampuli za kibailojia na mienendo ya viasili nasaba au maumbile.

“Huu siyo mkutano kuhusu siasa na pesa. Huu ni mkutano kuhusu sayansi. Tunahitaji uelewa wa pamoja, mtazamo na uzoefu, kujibu maswali ambayo hatuna majibu yake, na kutambua maaswali ambayo tunaweza hata tusitambue kuwa tunahitaji kuuliza.” Amesema Dkt Tedros.

Wataalamu wataanzia kwenye utafiti uliopo kuhusu milipuko mingine kama ya ugonjwa wa SARS na MERS na kuona mapungufu na vipaumbele vya utafiti ili kusongesha taarifa za kisayansi na matokeo ya kitabibu ambayo yanahitajika sana kupunguza athari za mlipuko wa sasa wa corona.

Mkutano huo unatarajiwa kutoa ajenda ya utafiti wa kimataifa kwa ajili ya  virusi vya corona, kuweka vipaumbele na mfumo ambao unaweza kuongoza ni miradi gani inatakiwa kutekelezwa mwanzo kabla ya mingine.

"Tunatumai kuwa moja ya matokeo ya mkutano huu itakuwa namna iliyokubaliwa kufanya utafiti ambao watafiti na wafadhili wataungana. Jambo la msingi ni mshikamano, mshikamano, mshikamano." Amesisitiza Dkt Tedros.