Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa maji wa IFAD Niger waua ndege wawili kwa jiwe moja

Wakazi nchini Niger
IOM/Monica Chiria
Wakazi nchini Niger

Mradi wa maji wa IFAD Niger waua ndege wawili kwa jiwe moja

Amani na Usalama

Mfuko wa maendeleo ya kilimo duniani, IFAD kwa kushirikiana na serikali ya Norway wameanzisha mradi wa kusukuma maji katika eneo kame la Waragou nchini Niger na hivyo kusaidia wafugaji wa eneo hilo na idadi kubwa ya watu wanaofurushwa kufuatia mapigano. 

Hapa ni kijiji cha Waragou nchini Niger, ambako kupitia video ya IFAD tunaona taswira kutoka angani ya nyumba za wanakijiji. Kwenye bomba la maji kuna foleni kubwa. Wanawake kwa wasichana wameweka mitungi kwenye foleni ili kujaza maji.

Moja ya familia ambazo zimekimbilia kijiji hiki ni ile ya Ambotcha Malam Dalo ambaye ni mkimbizi wa ndani akisimulia kilichosababisha wakimbie.

(Sauti ya Malam)

“Ilikuwa ni giza. Wanaume wote kutoka kijiji chetu walikuwa msikitini. Watu waliokuwa wamejihami waliwasili. Waliwaua wanakijiji 12. Tuliogopa sana. Tulizika wanaume hao 12 na tukakimbia.Tulitembea hadi pale tulipofika, tulipita vijiji vingine. Tulisikia kwamba Waragou ni pazuri na tukaendelea kutembea hadi tulipowasili hapa.”

Familia ya Malam ni miongoni mwa kaya 150,000 zilizofurushwa nchini Niger. Waliziacha nyumba zao na mashamba yao ili kupata hifadhi. Licha ya kwamba wanatamani kurejea nyumbani lakini katika eneo hilo la jangwa, wengi wamekimbia kwa ajili ya usalama lakini hakuna usalama bila maji.

Mabadiliko ya tabianchi, Sahel yanasababisha ukame wa muda mrefu na watu walilazimika kuchimba chini zaidi kwa ajili ya visima vya maji. Lakini mradi wa IFAD unaotegmea kawi au umeme wa paneli za sola unasukuma lita 15,000 za maji.

Raslimali finyu kwa kawaida ni chanzo cha migogoro kati ya wakulima na wafugaji na mradi kama huu unahakiksha kwamba mashine zinafanya kazi vizuri na kwamba ugomvi unatatuliwa kwa utaratibu kila unapozuka. Boukar Walam Gori, ni chifu Kijiji cha Waragou

(Sauti ya Walam)

« Sasa maji yapo mengi kwa ajili ya kila mtu ikiwemo wakimbizi na wafugaji na wanyama. Tunashukuru Mungu, hamna mtu mwenye kiu sasa. Iwapo kituo hakingalikuwepo tungalikuwa na mizozo kwa sababu hatuna ya kutosha. »

Miradi kama hii inalenga kukabiliana na changamoto zitokanazo na ukosefu wa maji na kuleta suluhu za amani kwa watu wenye kiu.