IFAD na wadau waepusha mizozano kati ya wakimbizi na wafugaji Niger

27 Aprili 2020

Nchini Niger, mfuko wa maendeleo ya kilimo, IFAD na wadau wake wamesaidia ujenzi wa mradi wa maji uliosaidia kupunguza mzozano kati ya wakimbizi wa ndani, wafugaji na familia zinazohamahama.

Nchini Niger, mfuko wa maendeleo ya kilimo, IFAD na wadau wake wamesaidia ujenzi wa mradi wa maji uliosaidia kupunguza mzozano kati ya wakimbizi wa ndani, wafugaji na familia zinazohamahama.

Mradi huo katika eneo la Diffa lililopo kusini-mashariki mwa Niger unatokana na ukweli kwamba idadi ya watu wanaokimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya Boko Haram sambamba na kusaka maji imeongezeka katika eneo hilo la ukanda wa Sahel.

Wakimbizi hao wa ndani na wenyeji wao sasa wanaishi kwenye vibanda walivyojitengenezea wenyewe huku wakikumbuka kilichowafurusha makwao.

Miongoni mwao ni Ambotcha Malam Dalo, mkimbizi wa ndani ambaye ni miongoni mwa wakimbizi wa ndani 250,000 nchini Niger na anasema kuwa, “ilikuwa yapata saa moja usiku, giza lilishaingia na wanaume wote kijijini walikuwa wameenda msikitini. Watu wenye silaha walikuja na kuuawa wanakijiji 12. Tulihofia sana. Tuliwazika wanaume wale 12 na kukimbia kijiji chetu.”

Bi. Dalo anasema kuwa walitembea kwa muda wa wiki moja hadi kufika Waragou, ambako walielezwa kuwa angalau kuna usalama.

Waragou ni makazi ya zaidi ya wakimbizi wa ndani 7,000 ambao pamoja na kusaka usalama kwenye eneo hilo bado wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji kutokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyochochea kuenea kwa jangwa.

Visima vya asili havikuwa na uwezo wa kutoa kiwango kikubwa cha maji kukidhi mahitaji na ndipo IFAD kwa ushirikiano na serikali ya Niger na Norway wakajenga mtambo wa kusukuma maji kwa kutumia nishati ya jua.

Mtambo huo unasukuma lita 15,000 za maji kwa saa, ambapo maji yanatoka umbali wa mita 62 chini ya ardhi.

Saleh Mahmadou, mchungaji wa ng’ombe anasema mradi huo umekuwa mkombozi kwa sababu, “mifugo ilikuwa ni mingi mno kiasi kwamba tulikesha usiku mzima kuwanywesha maji. Lakini kuwepo kwa mtambo huu, hata kama ni kunywesha maji mifugo mingi, unamaliza hata kama giza halijaingia. Tunafurahia sana kuwepo kwa kituo hiki.”

Ili kupunguza msuguano katika matumizi ya rasilimali hiyo adhimu ya maji, IFAD imesaidia wakazi wa Waragou kuunda kamati ya usimamizi wa matumizi ya maji ili kuepusha tatizo lolote linalotokea.

Walam Gori ni Chifu wa kijiji na anasema kuwa, “sasa maji ni mengi kwa ajili ya kila mtu wakiwemo wakimbizi, wachungaji wa kuhamahama na wanyama. Tunashukuru Mungu hakuna tena mwenye kiu. Bila mradi huu, tungalikuwa na mizozano, kwa sababu tusingalikuwa na maji ya kutosha kila mtu.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud