Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres akiwa Niger: Rasilimali zaidi zinahitajika kukabili mashambulizi ya kigaidi Sahel

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akilakiwa na Rais wa Niger Mohamed Bazoum kwenye mji mkuu Niamey
UN /Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akilakiwa na Rais wa Niger Mohamed Bazoum kwenye mji mkuu Niamey

Guterres akiwa Niger: Rasilimali zaidi zinahitajika kukabili mashambulizi ya kigaidi Sahel

Amani na Usalama

Idadi ya mashambulizi ya kigaidi kwenye ukanda wa Sahel barani Afrika inazidi kuongezeka, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ambaye amewasili kwenye mji mkuu wa Niger, Niamey hii leo Jumatatu ikiwa ni kituo cha pili cha ziara yake Afrika Magharibi wakati huu wa hitimisho la mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Akizungumza baada ya kukutana na Rais wa Niger, Mohamed Bazoum, Bwana Guterres amesema, “jamii ya kimataifa inapaswa” kutambua kuwa ugaidi “sio tu jambo la kikanda au la Afrika pekee, bali ni jambo linalotishia dunia nzima.” Amesisitiza wito wake wa kuelekezwa kwa rasilimali nyingi zaidi ili kutatua suala hilo akisema, “amani, utulivu na ustawi wa Niger na katika ukanda wote wa Sahel vinasalia kuwa kipaumbele cha Umoja wa Mataifa.”

Rais Mohamed Bazaoum akitambua azma ya Bwana Guterres ya kusaka suluhu ya tatizo la ugaidi amesema “tatizo linasonga na linabadilika na tunahitaji majawabu yanayoendana na hali ya sasa.”
Wakati huo huo, Rais wa zamani wa Niger, Mahamadou Issoufou,  amekubali ombi la Muungano wa Afrika, AU,  la kumtaka aongoze jopo la pamoja la muungano huo na Umoja wa Mataifa, AU-UN la kutathmini hali ya usalama ukanda wa Sahel likijikita katika mapendekezo ya maendeleo ya jinsi ya kuimarisha hatua za kimataifa za utatuzi wa janga la usalama Sahel.

Tathmini hiyo itafanyika kwa mashauriano na Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS na Sekretarieti ya kundi la nchi Tano, G5 la ukanda wa Sahel.

Raia ndio waathirika

Umoja wa Mataifa unasema ukosefu wa usalama Niger unachochewa na pande mbalimbali ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema mara nyingi raia ndio wanaoathirika pindi ghasia zinapoibuka.

Takwimu zinaonesha kuwa takribani waathirika 8 kati ya 10 wa mashambulizi ni raia.
Vikundi mbalimbali vyenye misimamo mikali vinaendesha shughuli zao hasa katika majimbo ya Tillabéri, Tahoua na Diffa huko Kaskazini-maghairbi, kusini na kusini-mashariki mwa Niger.

Huko jimbo la Maradi, ukanda wa kusini, vikundi vilivyojihami mara kwa mara vinaendesha operesheni zao kutokea Nigeria, halikadhalika waporaji ndani ya Niger nao ni tishio kubwa.
 
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akiwasili mji mkuu wa Niger, Niamey ikiwa sehemu ya ziara yake ya mataifa matatu barani Afrika
UN /Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akiwasili mji mkuu wa Niger, Niamey ikiwa sehemu ya ziara yake ya mataifa matatu barani Afrika

Mwaka 2021, kipimo cha ugaidi duniani, kilisema vifo 588 nchini Niger vilitokana na ugaidi, ikiwa ni idad ikubwa zaidi ya vifo visababishwavyo na ugaidi katika muongo uliopita. Katika jimbo la Tillabéri, idadi ya vifo imeongezeka maradufu kati yam waka 2020 na 2021.

Ukosefu wa usalama ni moja tu ya sehemu ya kile alichosema Katibu Mkuu kama janga la pande tofauti lililo na kipimo cha kupindukia. Ametaja majanga mengine kuwa ni mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa uhakika wa kupata chakula, bei ya juu ya vyakula inayochochewa na vita nchini Ukraine akisema vyote hivyo vimechochea ongezeko kubwa la mahitaji ya kibinadamu.

Umoja wa Mataifa unasema idadi ya watu ambao wako na mahitaji makubwa zaidi ya chakula imeongezeka maradufu tangu mwaka 2020, na inakadiriwa kuwa asilimia 15 ya wananchi milioni 25 wa Niger watahitaji msaada wa kibinadamu mwaka huu wa 2022 

Katika nchi ambayo asilimia 80 ya wananchi wake wanategemea kilimo kama njia ya kujipatia kipato, ukosefu wa usalama na mabadiliko ya tabianchi vimechangia katika kupunguza uwezo wa familia kujilisha.

Wanawake nchini Niger wakiandaa mashamba tayari wa msimu wa mvua kama sehemu ya kukabiliana na kuenea kwa jangwa.
© FAO/Giulio Napolitano
Wanawake nchini Niger wakiandaa mashamba tayari wa msimu wa mvua kama sehemu ya kukabiliana na kuenea kwa jangwa.

Ripoti ya mwaka 2019 ya kipimdo cha maendeleo ya binadamu, HDI, ambayo inapima umri wa mtu kuishi, elimu na mapato iliiweka Niger kama nchi ya chini kabisa kwenye orodha ya mataifa 189 duniani yanayoendelea.

Matumaini kwa siku za usoni

Licha ya changamoto kubwa ambazo Niger inakabiliana nazo, Katibu Mkuu wa UN amewaeleza waandishi wa habari kuwa “bado kuna matumaini na kwamba Umoja wa Mataifa lazima usimamia azma yake ya kusaidia vijana wa Niger hususan wanawake, na waweze kupata fursa za kujenga mustakabali bora.

Umoja wa Mataifa unahitaji hatua zaidi ili kufanikisha matamanio na matumaini ya wananchi wa Niger
© UNICEF/Frank Dejongh
Umoja wa Mataifa unahitaji hatua zaidi ili kufanikisha matamanio na matumaini ya wananchi wa Niger

Amesema, “kipindi chanya kwa Niger” kinaweza kuleta mzunguko bora zaidi wa mabadiliko ukanda mzima.

Kesho  Jumanne, Guterres anaelekea Nigeria na tayari alizuru Senegal siku ya Jumapili.