Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto zaidi ya 6,500 walazimika kukimbia kila siku Syria:UNICEF

Watoto nchini Syria wakijihifadhi katika gofu wakati mashambulizi ya risasi na anga yakishika kasi katika mjin wa Idlib
UNICEF/NYHQ2012-0218/Romenzi
Watoto nchini Syria wakijihifadhi katika gofu wakati mashambulizi ya risasi na anga yakishika kasi katika mjin wa Idlib

Watoto zaidi ya 6,500 walazimika kukimbia kila siku Syria:UNICEF

Amani na Usalama

Shiriika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limetoa wito wa kusitisha mapigani mara moja ili kuwalinda watoto na kuruhusu uingizaji wa misaada ya kibinadamu bila vikwazo.

Taarifa iliyotolewa leo na mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore inasema “mgogoro wa Kaskazini Magharibi mwa Syria unageuka kuwa zahma kubwa isiyoelezeka ya ulinzi kwa watoto. Machafuko ya wiki iliyopita yamewalazimisha watoto 6500 kukimbia kila siku na kufanya idadi ya watoto waliotawanywa na machafuko katika eneo hilo kufikia zaidi ya 300,000 tangu mapema mwezi Desemba mwaka jana.”

UNICEF inakadiria kwamba watoto watoto milioni 1.2 wanahitaji msaada haraka. Maji, chakula na madawa ni haba, watoto na familia zao wanasaka hifadhi katika maeneo ya umma ikiwemo mashuleni, misikitini, kwenye majengo ambayo hayajakamilika na kwenye maduka.

Hospitali ya wanawake na watoto jimbo la Idlib nchini Syria, ambayo ilishambuliwa kufuatia mashambulio ya anga yaliyofanyika mapema asubuhi.
© UNICEF
Hospitali ya wanawake na watoto jimbo la Idlib nchini Syria, ambayo ilishambuliwa kufuatia mashambulio ya anga yaliyofanyika mapema asubuhi.

Shirika hilo limeongeza kuwa wengi wanaishi katika maeneo ya wazi ikiwemo kwenye bustani za kupumzikia huku kukiwa na mvua kubwa na baridi kali. Na fursa ya kupata huduma za msingi kama za afya, maji au usafi ni ndogo sana ama haipo kabisa. “mjini Idlib ambako robo tatu ya wanaohitaji msaada ni wanawake na watoto, familia nyingi zimeathirika na kutawanywa mara kadhaa na sasa wako katika hali ya taharuki bila kuwa na njia salama ya kukimbia machafuko yanayoendelea.”

Bi. Fore amesema mgogoro wa Syria unawabebesha gharama kubwa watoto, watoto 900 wameuawa nchini Syria mwaka jana pekee kutokana na vita vinavyoendelea na asilimia 75 ya watoto hao walikuwa Kaskazini Magharibi huku mji wa Idlib ukiongoza kwa idadi kubwa ya vifo na majeruhi.

watoto wakipumzika chini ya mti nchini Syria.Familia zao zimeweka mahema katika kambi ya wakimbizi kwenye kijiji cha Aqrabat , kilimeta 45 kutoka mjini Idlib karibu na mpaka na Uturuki
© UNICEF/Aaref Watad
watoto wakipumzika chini ya mti nchini Syria.Familia zao zimeweka mahema katika kambi ya wakimbizi kwenye kijiji cha Aqrabat , kilimeta 45 kutoka mjini Idlib karibu na mpaka na Uturuki

Hata hivyo UNICEF inasema kupitia washirika wake katika eneo hilo inaendelea kufikisha msaada kwa familia zenye mahitaji ikiwemo zilizotawanywa hivi karibuni.” Msaada huu unajumuisha vifaa vya usafi na kujisafi, maji salama , chanjo kwa watoto dhidi ya magonjwa, vipimo na matibabu kwa watoto wanaoumwa.”

Fore amesisitiza kwamba msaada wa kuokoa maisha ni muhimu na ni lazima uendelee lakini amesema hata hivyo hautomazima madhila yanayowakabili watoto hao. Hivyo ametoa wito kwambaMachafuko lazima yakome kwa ajili ya kuwanusuru watoto. Pande zote kinzani katika mzozo lazima sitishe uhasama mara moja na kuruhusu watoto na familia zao kukimbia machafuko hayo, ili misaada ya kibinadamu na huduma za msingi vianze tena na kuruhusu bila vikwazo ufikishami wa misaada ya kibinadamu kwa kila mtoto.