Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

watoto wanaendelea kubeba gharama za machafuko Syria:UNICEF

watoto wakipumzika chini ya mti nchini Syria.Familia zao zimeweka mahema katika kambi ya wakimbizi kwenye kijiji cha Aqrabat , kilimeta 45 kutoka mjini Idlib karibu na mpaka na Uturuki
© UNICEF/Aaref Watad
watoto wakipumzika chini ya mti nchini Syria.Familia zao zimeweka mahema katika kambi ya wakimbizi kwenye kijiji cha Aqrabat , kilimeta 45 kutoka mjini Idlib karibu na mpaka na Uturuki

watoto wanaendelea kubeba gharama za machafuko Syria:UNICEF

Amani na Usalama

Watoto wanaendelea kubeba gharama kubwa za machafuko yanayoshika kasi Kaskazini Magharibi mwa Syria limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Kupitia tarifa ya Ted Chaiban mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini “zaidi ya watoto 500 wamejeruhiwa au kuuawa katika miezi tisa ya mwanzo wa mwaka 2019 na takriban watoto 65 wameuawa au kujeruhiwa katika mwezi wa Desemba pekee.”

Taarifa yake imeongeza kuwa machafuko yaliyoshika kasi hivi karibuni katika eneo lenye watu wengi la Ma’arat An-Mu’man Kusini mwa jimbo la Idlib yamezilazimisha maelfu ya familia kufungasha virago na kukimbia eneo hilo.

“tangu tarehe 11 Desemba zaidi ya watu 130,000 wakiwemo watoto 60,000 wametawanywa kutoka Kusini mwa Idlib, Kaskazini mwa Hama na Magharibi mwa Aleppo kwa sababu ya kuongezeka kwa mapigano.”

Watoto daima wanapaswa kulindwa ikiwemo wakati wa vita, huu ni wajibu w apande zote katika mzozo na si chaguo. Hivyo tunazitaka pande zote katika mzozo kusitisha uhasama na kuwapa kipaumbele watoto wakati wote-UNICEF

UNICEF inasema kutawanywa huku kunaongeza shinikizo kwa jamii karimu zinazowahifadhi na pia katika makambi ya wakimbizi ambayo yamefurika.

Familia nyingi bado hazina malazi kabisa na zina lala nje katika maeneo ya wazi. Shirika hilo limeonya kwamba ongezeko la machafuko limekuja wakati mbaya ambapo msimu wa baridi Kali umeanza kwenye ukanda huo ukiambatana na mvua zinazoleta mafuriko na baridi.

“Watoto wanaoishi makambini au katika makazi mengine ambayo hayajengwa vizuri wamechoka kutokana na kutawanywa mara kadhaa na hususan kuishi katika mazingira yenye baridi Kali, maradhi na kushuhudia vifo vingi.”

UNICEF imetoa wito wa kuhakikisha kwamba fursa za kufikisha misaada ya kibinadamu zinaendelea ili kunusuru maisha ya maelfu ya watoto kila mahali kwenye majimbo ya Kaskazini Magharibi na sehemu zingine za Syria.

 Shirika hilo limesisitiza kwamba “Miaka tisa katika vita hivyo watoto wanaendelea kukumbana na ukatili wa hali ya juu, kiwewe na madhila mengine makubwa.

Katibu Mkuu

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesisitiza kwamba machafuko hayo yanayoendelea Syria yamesababisha madhila makubwa kwa raia na kuwatawanya jumla ya 80,000 wakiwemo 30,000 waliotawanywa wiki iliyopita pekee.

Katibu mkuu kupitia taarifa yake iliyotolewa usiku wa kuamkia leo ameongeza kuwa “Fursa endelevu , isiyo na vikwazo na salama kwa wahudumu wa binadamu ni muhimu kuweza kuwafikia raia wakiwemo wa ,pakani na inapaswa kutolewa ili kuruhusu Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada ya kibinadamu kuendelea kufanya kazi yao ya muhimu katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.”

Guterres amerejelea kauli yake kwamba “hakuna suluhu ya vita katika mzozo wa Syria na kwamba suluhu pekee nay a kuaminika ni mchakato wa kisiasa unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa kwa kuzingatia azimio la Baraza la Usalama namba 2254 la 2015 ambalo linatoa wito wa usitishaji uhasama na kusaka suluhu ya kisiasa.”

Miji imesambaratishwa

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA imesisitiza kuwa hali ni mbaya sana kwa watu milioni 4 wanawake, Watoto na wanaume huko Kaskazini Magharibi mwa Syria ambako mapigano, uvurumishaji makombora na mashambulizi ya anga vimesababisha athari kubwa kwa wat una miumbombinu muhimu ya raia. "Miji yote na vijiji vimesambaratishwa, wakati jamii kadhaa zimekatwa na mawasiliano kabisa", limeongeza shjirika la OCHA.

"Wakazi katika maeneo yanayodhibitiwa na Serikali wameathiriwa na mashambulizi yasiyo ya ubaguzi katika maeneo yao".

Na kufanya mambo kuwa mbaya zaidi, msimu wa baridi unashika kasi baadhi ya siku nyuzi joto zinashuka hadi chini ya sufuri , lakini pia uhaba wa mafuta umeibuka kama changamoto kubwa, ukiongezea na mvua kubwa ambazo zinazidisha hatari ya ulinzi, afya na hatari zingine.