Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya kibinadamu Syria iko njia panda, huku watoto wakilipa gharama kubwa:UN

Aprili 3, 2018 nchini Syria, mtoto katika shule ambayo imegeuka kuwa kituo cha uhifadhi katika kijiji cha Zeyarah, kaskazini mwa mji wa Aleppo
UNICEF/UN0207849/Al-Issa
Aprili 3, 2018 nchini Syria, mtoto katika shule ambayo imegeuka kuwa kituo cha uhifadhi katika kijiji cha Zeyarah, kaskazini mwa mji wa Aleppo

Hali ya kibinadamu Syria iko njia panda, huku watoto wakilipa gharama kubwa:UN

Wahamiaji na Wakimbizi

Hali ya kibinadamu nchini Syria imefikia pabaya, mlo ni dhiki, malazi tabu na watoto wanaendelea kulipa gharama kubwa ya vita yameonya leo mashirika ya umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa  (OCHA) nchini Syria Panos Moumtzis, wamezidiwa uwezo katika kukabiliana na changamoto za kibinadamu na hali ni mbaya kwani wamejikuna na mkono umefika mwisho.

(SAUTI YA PANOS MOUMTZIS)

“Tuna kidogo cha kushibisha sasa tu , maghala ni matupu , tunafanya kazi usiku na mchana kwa kila upande, tumekuwa na timu zinazofanya kazi, zinapokea saa tita alfajiri idadi kubwa ya watu, na daima tunajaribu kupata mahali pa kuwahifadhi kwenye jumuiya za wenyeji, kwenye majengo yaliyo tupu, kwenye makambi, tunatumia kila sehemu inayowezekana ya Idlib ili kuweza kuwapokea, kuwahifadhi na kushughulikia mahitaji yao.”

 Nalo shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limesema, watoto nchini humo wameendelea kulipa gharama kubwa ya vita kila uchao. Mkurugenzi wa kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wa shirika hilo Geert Cappeleaere’ amesema wamepokea taarifa kuwa watoto 13 wameuawa siku chache zilizopita katika mashambulio yanayodaiwa kulenga vijiji na katika shambulio la Kijiji cha Zardana Kaskazini Magharibi mwa Idlib maisha ya watoto 9 yamekatiliwa Jumapili .

Amesisitiza  kuwa huu ni ukiukaji mkubwa wa haki za watoto ambao wengi wamesambaratishwa na vita na hawana mahali pengine pa kwenda isipokuwa kupata hifadhi kwenye makambi ya wakimbizi na mashuleni.  Hali hii amesema inadhihirisha kwamba vita dhidi ya watoto Syria havina dalili yoyote ya kumalizika.