Ukatili dhidi ya watoto umefurutu ada Mashariki ya Kati :UNICEF

2 Agosti 2019

Wiki hii imekuwa ni wiki nyingine ya majonzi na ukatili kwa watoto wanaoshi kwenye maeneo ya vita hususan Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini huku mauaji na vitendo vingine vya kikatili vikiwaandama kila uchao. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF iliyotolewa leo kwenye mjadala wa wazi wa Baraza la Usalama kuhusu watoto na migogoro ya silaha.

Mkurugenzi Mtendaji huyo Henrietta Fore amesema, “tangu Jumamosi iliyopita machafuko yamekuwa jinamizi kwa watoto wa eneo hilo, shule mbili na hospital vzimeshambuliwa mjini Tripoli, Libya, takriban watoto 4 wa sekondari walipigwa risasi wakati wa maandamano jimbo la Kordofan Kaskazini nchini Sudan, na watoto wanne wameuawa na wengine 14 kujeruhiwa katika shambulio lililofanyika sokoni jimboni Sa’dah nchini Yemen.”

Ameongeza kuwa wakati huohuo machafuko yaliyoua au kujeruhi watoto 359 tangu mwanzoni mwa mwaka huu yanaendelea Kaskazini Magharibi mwa Syria.

Mkurugenzi huyo mtendaji wa UNICEFpia wiki hii  amesema watoto kadhaa kwenye eneo la Palestina walijeruhiwa katika matukio ya kikatili na kuifanya jumla ya watoto waliojeruhiwa katika eneo la Wapalestina tangu mwanzoi wa mwaka huu wa 2019 kufikia 477.

“Wanaotekeleza ukatili huu wanawaangusha watoto na wameshindwa kutimiza wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za kuhakikisha watoto wanalindwa. Hali hii ni zaidi ya kusitikitisha ni ya kughadhibisha”, amesema Bi. Fore.

Bi. Fore amesisitiza kwamba “hali ya kutojali maisha ya watoto kulikodhihirika wiki hii ni lazima ikome. Pande zote katika mzozo na wale walio na ushawishi na pande hizo wanawajibika na usalama wa watoto popote walipo katika kanda hiyo.”

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter