Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 1 zahitajika kusaidia watu milioni 3 mwaka 2020 Somalia:UNSOM

Mfugaji kaskazini mwa Somalia katika jimbo lililokumbwa na ukame, alipoteza takribani nusu ya kondoo wake ambao walikuwa wamefikia 70.
Photo: UNICEF/Sebastian Rich
Mfugaji kaskazini mwa Somalia katika jimbo lililokumbwa na ukame, alipoteza takribani nusu ya kondoo wake ambao walikuwa wamefikia 70.

Dola bilioni 1 zahitajika kusaidia watu milioni 3 mwaka 2020 Somalia:UNSOM

Msaada wa Kibinadamu

Serikali ya shirikisho ya Somalia na washirika wa kimataifa wamezindua mpango unaohitaji zaidi ya dola bilioni moja ili kuweza kutoa msaada wa kibidamu unaohitajika nchini humo. Flora Nducha na taarifa zaidi

Kwa mujibu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia UNSOM fedha hizo ni za kuwasaidia watu zaidi ya milioni 3 kwa mahitaji ya msingi ya kibinadamu mwaka huu wa 2020.

Na mara baada ya uzinduzi wa mpango huo uliofanyika mjini Moghadishu Somalia mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini humo Adam Abdelmoula amesema

(SAUTI YA ADAM ABDELMOULA)

“Wakati tunazindua mpango huu lazima tukumbuke aina ya madhila ya kibinadamu ambayo Somalia inaendelea kukabiliwa nayo. Miezi michache tu iliyopita watu zaidi ya nusu milioni waliathirika na mafuriko ambayo yalikumba sehemu kubwa ya nchi, wakati wengi walioathirika wameweza kurejea nyumbani wengine wengi wanaendelea kuhaha kujenga upya maisha yao.”

Uzinduzi huo  wa mpango wa kukabiliana na masuala ya kibinadamu (HRP) wa jumla ya dola bilioni 1.03 umehudhuriwa pia na waziri wa Somalia wa masuala ya kibinadamu na udhibiti wa majanga Hamza Said Hamza aliyesema mpango huu unadhihirisha dhamira ya serikali ya Somalia ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kibinadamu na msaada wa dharura OCHA, mashirika yasiyo ya kiserikali NGO’s na jumuiya ya kimataifa katika kuwasaidia watu wa Somalia.

Ameongeza kuwa mgogoro wa kibinadamu Somalia unachangiwa na vita vya miaka mingi, ukame wa muda mrefu , na bila shaka mafuriko yaliyoshuhudiwa mwaka 2019.

Fedha hizo za mpango wa HPR zitasaidia watu milioni 3 wakiwemo milioni 1.7 waliotawanywa na vita, kutokuwepo usalama, kuhamishwa kwa nguvu, ukame na mafuriko na msaada utakuwa katika mfumo wa mgao wa chakula , elimu, huduma za afya, maji safi na salama na pia ulinzi kwa walio katika hatari ya ukatili wa kijinsia.

Akizungumza kwa niaba ya mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Somalia mkurugenzi wa muungano wa NGO Nasra Ismail amesema kuna mambo mawili ambayo yako bayana

(SAUTI YA NASRA ISMAIL)

“Kwamba bila kuwa na mfumo wa msaada wa kibinadamu wenye wadau mbalimbali kuanzia Umoja wa Mataifa, NGO’s na mashirika ya serikali watu wa Somalia wangekuwa katika hali mbaya zaidi na pili kama mwenendo wa miaka mitano iliyopita unavyoonyesha ni lazima tuendelee na kiwango hiki cha dharura na ahadi ya kuhakikisha kwamba hatua zilizopatikana tangu mwaka 2015 zinalindwa.”

UNSOM imesema mwaka huu mahitaji ya ufadhili ya mpango wa usaidizi wa kibinadamu yamepungua kwa asilimia 11 kutoka dola bilioni 1.08 hadi dola bilioni 1.03.