Skip to main content

Baa la njaa liko mlangoni Somalia na leo tunapokea onyo la mwisho:Griffiths

Mwanzoni mwa mwaka 2017 watu milioni 6.2 walihitaji msaada wa kibinadamu Somalia , lakini sasa idfadi imeongezeka zaidi : Kutoka maktaba:OCHA
@UNOCHA Somalia
Mwanzoni mwa mwaka 2017 watu milioni 6.2 walihitaji msaada wa kibinadamu Somalia , lakini sasa idfadi imeongezeka zaidi : Kutoka maktaba:OCHA

Baa la njaa liko mlangoni Somalia na leo tunapokea onyo la mwisho:Griffiths

Tabianchi na mazingira

Mratibu mkuu wa masuala ya kibinadamu na misaada yad harira wa Umoja wa Mataifa Martin Griffith ameshtushwa sana na kiwango cha machungu na madhila wanayopitia watu wa Somalia kutokana na hali ya ukame ambao sasa umeikaribisha njaa mlangoni.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo mjini Moghadishu ambako amekuwa ziarani tangu mwishoni mwa wiki Griffiths amesisitiza kuwa “Baa la njaa liko mlangoni na leo tunapokea onyo la mwisho”

Ripoti ya uchambuzi wa uhakika wa chakula na lishe ya Somalia, inayotolewa leo, inaonyesha dalili za uhakika kwamba baa la njaa litatokea katika maeneo mawili kwenye jimbo la Bay  ambayo ni wilaya za Baidoa na Burhakaba Kusini-Kati mwa Somalia kati ya mwezi Oktoba na Desemba mwaka huu.

Bwana Griffiths amesema “Narudia tena hili ni onyo la mwisho kwetu sote. Hali na mwenendo unafanana na ule ulioonekana mwaka 2010-2011, katika mgogoro huo. Ila wa sasa ni mbaya zaidi. Kushindwa kusiko na kifani kwa misimu minne ya mvua mfululizo, miongo ya migogoro, kutawanywa kwa watu wengi, na masuala makubwa ya kiuchumi yanawasukuma watu wengi kwenye ukingo huo wa baa la njaa. Na hali hii inaweza kudumu hadi angalau Machi 2023.”

Sijashangazwa na matokeo haya 

Kituo cha kusambaza maji maeneo yaliyo na ukame Somalia.
© IOM Somalia 2022/ Ismail Osma
Kituo cha kusambaza maji maeneo yaliyo na ukame Somalia.

Mkuu huyo wa masuala ya kibinadamu ameendelea kusema kwamba “Ninasikitika kusema kwamba sishangazwi na matokeo haya. Nilikuwa Baidoa siku ya Jumamosi. Ni kitovu cha mzozo wa kibinadamu nchini Somalia. Sio mahali pekee penye mahitaji, lakini ni moja wapo ya maeneo. Katika kambi za watu wakimbizi wa ndani, tumeshuhudia njaa kali. Katika hospitali ya Baidoa, tumepata fursa ya kushuhudia watoto wakiwa na utapiamlo mkali kiasi kwamba hawakuweza hata kuzungumza. Upatikanaji wa huduma za msingi huko ni mdogo. Na hii ni hali ya Baidoa. Familia iwe zimekuwa kambini kwa siku kadhaa au kwa miaka -wengi wao wametuambia hawana matumaini ya kurejea nyumbani na baadhi yao wamekuwa katika moja ya maeneo hayo kwa miaka minane hadi tisa.”

Ameongeza kuwa mkasa kama huo unatokea pia Banadir, sio mbali na Mogadishu. “Nilitembelea hospitali ya mtaani nikiwa na wahudumu wa afya wa kipekee, wa Serikali na wasio wa serikali, na timu hizi za wataalam wa matibabu zinajitahidi kukabiliana na msongamano wa watoto waliodhoofika wanaotafuta matibabu. Na wao ndio wenye bahati, ndio wanaofanikiwa huko. Mmoja wa madaktari aliniambia kwamba wanaona ongezeko la asilimia 40-50 zaidi la watoto kuliko walivyofanya wiki chache zilizopita. Hakuna hata mtoto mmoja kati ya niliowaona katika kituo cha matibabu cha hospitali ya Banadir aliyeweza kutabasamu. Wachache sana waliweza kulia. Na tulipogundua tulipotoka, tulipata bahati ya kusikia mtoto akilia, na tuliambiwa kwamba mtoto akilia, kuna nafasi ya kuishi. Watoto ambao hawalii ndio tunapaswa kuwa na wasiwasi nao. Na mtoto huyu, akilia kwa wasiwasi mbele yetu mama yake alitabasamu.”

Daktari akihudumia mtoto mwenye utapiamlo katika hospitali ya Dolow Somalia
© UNICEF/Ismail Taxta
Daktari akihudumia mtoto mwenye utapiamlo katika hospitali ya Dolow Somalia

Watoto zaidi ya milioni 1 kukabiliwa na unyafuzi

Kwa mujibu wa Griffiths watoto milioni moja na nusu kote nchini Somalia watakabiliwa na utapiamlo wa hali ya juu au unyafuzi ifikapo Oktoba ikiwa tutabaki kwenye hali na mwenendo wa sasa.

“Bila shaka, mashirika ya jumuiya ya kibinadamu ya Kisomali, jumuiya za Kisomali, zimekuwa zikiitikia kile tunachosikia leo na kile ambacho tumekuwa tukiona katika miezi hii. Kujitahidi wawezavyo kwa rasilimali walizonazo. Ninataka kushukuru kwa ukarimu wa serikali nyingi na wafadhili waliotoa msaada. Watu wamekuwa wakichukua hatua. Wanajua wao ni akina nani, na tunawashukuru kwa mshikamano wao na watu wa Somalia. Bila shaka, hii inasaidia kuokoa maisha. Hao watoto mahospitalini, tunatarajia maisha yao yataokolewa.”

Kuokoa maisha tu haitoshi.

Bwana Griffith amesisitiza kuwa kuokoa maisha tu haitoshi kwani ukame, mbaya zaidi katika miongo minne, unatabiriwa kuendelea. Hii ni, katika maneno hayo yanayotumiwa mara nyingi, na ukweli ni kwamba janga la kibinadamu litaendelea na mahitaji yataongezeka.

“Ujumbe tunaousikia kutoka kwenye ripoti hii na tunaouona katika nchi hii na tunaoshuhudia katika hospitali na maeneo ya watu waliotawanywa bila shaka ni mbaya zaidi katika maeneo ya asili ya wale waliotawanywa, ujumbe huu ni wa dharura.”

Amesisitiza masuala kadhaa ya msingi: Kwanza kabisa, kwa mashirika ya kibinadamu ambayo nina bahati ya kufanya kazi nayo, lazima tupate ufikiaji wa haraka na salama wa watu wote wanaohitaji msaada, sio tu wale wanaochukua uamuzi mbaya wa kutembea kutoka kwenye makazi yao, vijiji na jamii hadi kufikia maeneo ya makazi na kufikia huduma, bali kwa watu wote wanaohitaji msaada tunahitaji kuwafikia na kwa salama.

Pili, nilitaja ukarimu wa wafadhili, na hawatashangaa kujua kwamba bado tunaomba zaidi. Tunahitaji ufadhili zaidi, hasa kwa mashirika ya Somalia. 

Kwa sababu ni mashirika ya Kisomali, kama ilivyo katika nchi nyingi, ambao wana wajibu wa mstari wa mbele, wajibu wa kwanza, ambao wanahatarisha, maisha yao ambao kufikisha msaada kwa msaada wa mashirika mengine mengi ya kijasiri na ya kibinadamu. Kwa hivyo tunahitaji ufadhili zaidi.

Mwanamke akienda kusaka maji kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Kabasa huko Dolow nchini Somalia
© UNICEF/Ismail Taxta
Mwanamke akienda kusaka maji kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Kabasa huko Dolow nchini Somalia

Tatu ni lazima tuwekeze licha ya hitaji la dharura la usaidizi wa kuokoa maisha kwa watu tunaowaona leo, na tutaona zaidi ya kesho na kuizungumza juu na kuchunguza na kupata msaada kwa ajili ya ufumbuzi endelevu ili tusijipate tena katika hali sawa na hii ni mara ya tatu katika miaka kumi iliyopita, na labda wakati huo itakuwa mbaya zaidi ikiwa hatuna bahati. 

“Hii ina maana ya kupeleka huduma za afya mahali watu walipo, kurudi kwenye maeneo ambayo ni magumu kufikiwa. Inamaanisha muundombinu bora ya maji na usafi wa mazingira. Huduma bora ya afya za msingi. Daktari katika hospitali ya Banadir alituambia jana kuwa huduma ya afya ya msingi ambayo ni njia muhimu ya kuzia magonjwa na kuokoa maisha, ni nadra kupatikana katika maeneo ya pembezoni na tunahitaji kuwekeza rasilimali.”

Tuko katika dakika za majeruhi

Akihitimisha mkutano wake na wanahabari Griffith amesema “Tunahitaji kutafuta vyanzo vya mapato mapya kwa watu wote ambao wanahitaji msaada lakini kwa sasa leo, tuko katika dakika za majeruhi za kuokoa maisha. Saa zinakimbia, na hivi karibuni zitaisha. Lakini hofu haiwasaidii wale wanaohitaji na wanastahili msaada wetu. Somalia inajua, kwa bahati mbaya, kuhusu njaa, Wasomali wanajua kuhusu majanga ya njaa. Na mwaka wa 2016 na 2017, watu wa Somalia na Serikali yao, wakisaidiwa na mashirika ya kibinadamu, walizuia njaa na lazima tuwe na matumaini kwamba tutaona hili tena sasa.”

Ameendelea kusema  kuwa onyo hili ni kusaidia kukomesha baa hilo la njaa kutokea.”Tunayo nafasi, lakini tuna wakati mdogo sana. Na ninarudi kwenye ile picha, ambayo nitakaa nayo, ya daktari aliyeniambia jana juu ya mtoto aliyelia, na akasema, vizuri, hiyo ni habari njema, hiyo ni ishara nzuri, ikiwa mtoto analia, tunaweza kuokoa maisha ya watoto hao wanaokuja hospitalini kwetu.”