Chonde chonde acheni kuongeza machafuko:Guterres

8 Januari 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amerejelea wito wake wa Jumatatu wa kudumisha amani kwa viongozi wa dunia akitaka kukomeshwa kwa uhasama na kujizuia na ongezeko la machafuko

Katika tarifa yake kufuatia mvutano unaoendelea Mashariki ya Kati baina ya Iran, Marekani na Iraq Katibu Mkuu amesihi kila upande kujizuia na vitendo vyovyote vitakavyoongeza zahma na kuanza tena majadiliano.

Pia amesisitiza ushirikiano wa kimataifa akisema kama ilivyokuwa muhimu Jumatatu bado ni muhimu hii leo.

Kwa upande wa jukumu lake Katibu Mkuu amesema ataendelea kuwasiliana na wadao wote kwani “Ni wajibu wetu wa pamoja kufanya kila juhudi kuepuka vita katika eneo la Ghuba vita ambavyo dunia haiwezi kuvimudu. Tunapaswa kutosahau madhila makubwa yanayosababishwa na vita na kama ada raia ndio wanaolipa gharama kubwa.”

Nao mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq UNAMi kupitia ukurasa wake wa Twitter umesema “Mashambulizi ya karibuni ya makombora katika majimbo ya Erbil na Anbar ni ya kuchochea machafuko na yanakiuka uhuru wa Iraq. Vurugu zisizo na maana zina athari zinazotabirika. Tunatoa mwito wa kujizuia haraka na kuanza tena kwa mazungumzo. Iraq haipaswi kulipa gharama ya mashindano ya watu wa nje. "

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud