Shambulio huko Tikrit linachukiza- Kubis

19 Novemba 2018

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, Ján Kubiš amelaani shambulio la bomu lilitokea huko Tirkit kaskazini mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Katika taarifa iliyotolewa leo mjini Baghdad, mji mkuu wa Iraq, Bwana Kubiš ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, UNAMI, amesema tukio hilo ni baya ambalo linawalenga raia wa kawaida.

Bw. Kubis amesema “shambulio hili nje ya mgahawa mmoja  katikati ya mji wa Tikrit ni baya. Halina lengo lolote lile zaidi ya kuwaua bure  raia wa kawaida na pia kujaribu kuharibu juhudi za Iraq za kurejea katika hali ya utulivu na amani baada ya mgororo ambao umechukua miaka kadhaa sasa.Lakini lengo la magaidi la kuvuruga usalama hususan katika maeneo ambayo yanarejea utulivu kutoka katika shughuli za magaidi litashindwa kutokana na amani na umoja miongoni mwa  raia wa Iraq na vilevile  na utayari wa vikosi vya usalama vya nchi hiyo.”

Mwakilishi huyo maalum ametoa wito kwa wakuu nchini humo kuzidisha juhudi za kukabiliana na magaidi ili kuzuia mashambulio mengine dhidi ya raia.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud