Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yakaribisha msaada wa dola milioni 3.39 kuwanusuru walioathirika na ukame Zambia

WFP wakisambaza mgao wa chakula kwa wakimbizi wa ndani karibu ni makazi ya Murta, Kadugli jimbo la Kordofan Kusini
OCHA/Sari Omer
WFP wakisambaza mgao wa chakula kwa wakimbizi wa ndani karibu ni makazi ya Murta, Kadugli jimbo la Kordofan Kusini

WFP yakaribisha msaada wa dola milioni 3.39 kuwanusuru walioathirika na ukame Zambia

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP, hii leo limekaribisha mchango wa dola milioni 3.39 kutoka mfuko wa Marekani wa maendeleo ya kimataifa USAID kusaidia kutatua hitaji la haraka la chakula kwa watu walioathirika na ukame nchini Zambia. 

Msaada huo wa Marekani ambao ulithibitishwa mwezi uliopita wa Desemba, umekuja katika wakati wa ongezeko la uhitaji baada ya ukame na kipindi kirefu cha kukosekana kwa mvua ambacho kimewaacha watu milioni 2.3 wakiwa hawana chakula na wakiwa katika uhitaji mkubwa wa msaada. Kupitia ufadhili huu, WFP itasambaza tani 2,380 za mahindi, na kuwapatia chakula na lishe  kwa watu 255,000 walioathirika kote nchini.

Akizungumzia mchango huo, Mwakilishi wa WFP nchini Zambia, Jenniffer Bitonde amesema, “WFP inahitaji dola milioni 36 za kimarekani ili kuweza kuisaidia serikali ya Zambia katika kukabiliana na janga. Mchango wa USAID unawakilisha asilimia 10 ya jumla ya hitaji lote na utairuhusu WFP  kuhakikisha watu waliothirika na ukame hawataenda kulala wakiwa na njaa katika kipindi hiki cha mwaka.”

Takribani watu milioni 1.1 wanategemewa kupokea msaada wa WFP wakati watu wengine milioni 1.2 watasaidiwa na serikali na wadau wengine ambao WFP inashirikiana nao.

Serikali ya Marekani ni moja ya wachangiaji wakubwa wa shughuli za WFP katika kuwasaidia wakimbizi kuanzia kule katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC. Kwa mwaka jana wa 2019, WFP imewasaidia takribani wakimbizi 14,000.