Watu 350,000 wanakabiliwa na baa la njaa Tigray, msaada wahitajika haraka kunusuru maisha:UN

10 Juni 2021

Takwimu mpya na za kusikitisha zilizotolewa leo zimethibitisha ukubwa wa dharura ya njaa inayolighubika jimbo la Tigray nchini Ethiopia ambako watu milioni 4 wanakabiliwa na njaa kali na wengine 350,000 tayari wanakubwa na baa la njaa.

Takwimu hizo zilizopo kwenye tathimini ya kiwango cha chakula IPC zinasema kupitia taarifa ya pamoja ya mashirika ya Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, la chakula na kilimo FAO na la kuhudumia Watoto UNICEF kuwa ukosefu wa taarifa kuhusu hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula unaowakabili watu Magharibi mwa Tigray pia inatia hofu kubwa.
WFP kwa upande wake imeongeza operesheni zake za msaada wa dharura wa chakula ikipeleka wafanyakazi 180 na kupanua wigo wa mgao ambao sasa unalenga kuwafikia watu milioni 1.4, hata hivyo shirika hilo linasema idadi haifiki hata nusu ya watu wanaopaswa kufikiwa.
Mashirika mengine nayo yanahaha kuwafikia watu wengine waliosalia ambao wanakabiliwa na njaa kali jimboni Tigray.

Maelfu ya wakimbizi wamevuka mpaka kutoka Ethiopia kuingia Sudan wakikimbia mgogoro katika eneo la Tigray nchini Ethiopia.
© WFP/Leni Kinzli
Maelfu ya wakimbizi wamevuka mpaka kutoka Ethiopia kuingia Sudan wakikimbia mgogoro katika eneo la Tigray nchini Ethiopia.

Wito wa hatua za msaada wa haraka

Mashirika hayo matatu ya Umoja wa Mataifa yametoa wito wa kuchukuliwa hatua haraka kushughulikia tatizo kubwa la kutokuwa na uhakika wa chakula Kaskazini mwa Ethiopia. Yameonya kuwa baa la njaa haliepukiki endapo hatua za haraka hazitochukuliwa kutoa msaada wa chakula, kuokoa maisha na misaada mingine ya kibinadamu ambayo ni ya lazima , na pia kuhakikisha fursa za kuwafikia bila vikwazo watu wenye uhitaji.
IPC ni mkakati wa kimataifa unaohusisha wadau mbalimbali yakiwemo mashirika 15 ya Umoja wa Mataifa, mashirika ya kikanda na unatathimini viwango vya njaa na kuviweka katika madaraja tofauti.
Tathimini hiyo ya IPC inasema katika jimbo la Tigray watu hao 350,000 wako katika janga la daraja la 5 la ukosefu wa chakula ambalo ni baa la njaa na hiyo ni idfadi kubwa zaidi kuorodheshwa katika nchi moja katika muda wa muongo mmoja uliopita.
Tathmini imeongeza kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watu ambao ni watu zaidi ya milioni 5.5 wanakabiliwa na kiwango cha juu cha ukosefu wa chakula daraja la 3-5 katika majimbo ya Tigray, Amhara na Afar.
Na watu milioni 2 kati ya hao wako katika kiwango cha dharuracha daraja la 4 la kutokuwa na uhakika wa chakula yaani njaa kali.

Hofu kubwa ya Umoja wa Mataifa

Mama ambaye amefurushwa kutoka ukanda wa Magharibi wa Tigray nchini Ethipia akizungumza na mfanyakazi wa UNICEF mjini Mekelle
UNICEF/Esiey Leul Kinfu
Mama ambaye amefurushwa kutoka ukanda wa Magharibi wa Tigray nchini Ethipia akizungumza na mfanyakazi wa UNICEF mjini Mekelle

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasema hofu yao kubwa hasa ni hatari ya njaa huko Tigray ikiwa mizozo itaongezeka na usaidizi wa kibinadamu umezuiliwa sana. “Jamii za vijijini kaskazini mwa Ethiopia zimeathiriwa sana na mzozo huo. Mashamba mengi yameharibiwa narasilimali za uzalishaji kama vile mbegu na mifugo imepotea. Ni muhimu kwamba tusaidie jamii hizi kulinda familia zao kwa lishe, na kusaidia uzalishaji wa chakula wa ndani, tukiweka njia za kujimwamua haraka. Lakini kuwasaidia watu walio kwenyehatihati ya njaa, tunahitaji rasilimali na ufikiaji  na ambayo vyote ni shida. " Amesema mkurugenzi mkuu wa FAO QU Dongyu.

Mkurugenzi mkuu wa WFP, David Beasely kwa upande wake amesema "Ukweli ulio bayana kwa wafanyikazi wetu huko Tigray ni kwamba kwa kila familia tunayoifikia na chakula cha kuokoa maisha, kuna mengi zaidi, haswa katika maeneo ya vijijini, ambao hatuwezi kufikia. Tumeomba fursa za ufikiaji wa kibinadamu lakini bado tunazuiliwa na vikundi vyenye silaha. Uwezo wa watu katika jimbo la Tigray kupata huduma muhimu na kwa WFP kuwafikia na msaada wa chakula ni muhimu ili kuepuka janga kubwa zaidi. Ufikiaji lazima upanuliwe zaidi ya miji mikubwa kufikia watu wanaohitaji sana msaada popote walipo, na kwa msaada wa kutosha na bila kuchelewa.

 Naye mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema "UNICEF ina wasiwasi sana juu ya hali kote Tigray hasa tunapoona watoto na watoto wachanga zaidi na zaidi wakiongezeka karibu na magonjwa na uwezekano wa kufa kutokana na utapiamlo. Tunashirikiana na wenzetu kutoa lishe, huduma za afya na msaada wa maji safi. Lkini, bila ufikiaji wa msaada wa kibinadamu kuongeza haraka katika maeneo yasiyofika inakadiriwa watoto elfu tatu wenye utapiamlo katika maeneo yasiyofikika kwa sasa huko Tigray wako katika hatari kubwa ya kifo. Ulimwengu hauwezi kuruhusu jambo hilo kutokea. ”

Wakimbizi kutoka Tigray wanaokimbia machafuko.
OCHA/Gabriela Vivacqua
Wakimbizi kutoka Tigray wanaokimbia machafuko.

Fedha zinazohitajika

• WFP inahitaji dola milioni 203 ili kuendelea kuongeza operesheni zake huko Tigray kuokoa maisha na uwezo wa kuishi hadi mwisho wa mwaka.
• FAO inahitaji haraka  dola milioni 30 kuweza kufikia watu milioni 1.4 kaskazini mwa Ethiopia katika miezi sita ijayo, na kwa jumla inahitaji dola milioni 77 kwa shughuli zilizopangwa hadi mwisho wa 2022. Hadi sasa, hakuna fedha yoyote ambayo imepatikana.
• Nayo UNICEF inahitaji dola milioni 10.7 kutoa msaada wa chakula cha matibabu kwa watoto wa Tigray na maeneo yaliyoathiriwa kwenye jimbo la Amhara na Afar. 
Fedha hiyo pia itawezesha UNICEF na washirika wake kutoa dawa za kawaida na kuongeza matibabu ya kuokoa maisha kwa watoto na ushauri wa akina mama na walezi juu ya njia zinazopendekezwa za kulisha watoto wachanga na Watoto wadogo.
 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter