Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa wajawazito na watoto wanapata tiba ya malaria kuliko wakati mwingine wowote:WHO

Wanawake wengi zaidi katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara wanatumia vyandarua vyenye viuatilifu ili kujikinga dhidi ya Malaria.
©UNICEF/Josh Estey
Wanawake wengi zaidi katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara wanatumia vyandarua vyenye viuatilifu ili kujikinga dhidi ya Malaria.

Sasa wajawazito na watoto wanapata tiba ya malaria kuliko wakati mwingine wowote:WHO

Afya

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la afya ulimwenguni WHO, inaonyesha kwamba wanawake wajawazito na watoto wanapata tiba zaidi ya malaria hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote ingawa juhudi na ufadhili vinahitajika kuchochea zaidi hatua za kimataifa dhidi ya ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya malaria kwa mwaka 2019 idadi ya  wajawazito na watoto wanaolala katika vyandarua vya mbu vilivyopuliziwa dawa na kufaidika na dawa za kuzuia malaria katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara imeongezeka kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni.

Pamoja na mafanikio hayo ripoti inasema hatahivyo “juhudi zaidi zinahitajika ili kupunguza maambukizi na vifo vya ugonjwa huo katika nchi zilizoathirika sana. Mwaka jana malaria iliathiri watu milioni 228 na kukadiriwa kuua watu 405,000 hususan Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara.”

Wajawazito wametajwa kuwa katika hatari zaidi ya kuambukizwa malaria na kuwaweka katika hatari ya magonjwa mengine kama upungufu wa damu na kifo. Pia malaria inaingilia ukuaji wa mtoto tumboni na kuongeza hatari ya kuzaliwa watoto njiti au wenye uzito mdogo ambayo ni moja ya sababu kubwa za vifo vya watoto wachanga.

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt.Tedross Adhamon Ghebreyesus amesema “kina mama wajawazito na watoto ndio walio katika hatari zaidi ya malaria na hatuwezi kupiga hatua dhidi ya ugonjwa huu kama hatutolenga makundi haya mawili. Tunaona dalili za matumaini , lakini mzigo wa maradhi na vifo vitokanavyo na malaria haukubaliki kwa sababu ugonjwa huu unazuilika kwa kiasi kikubwa. Kutokuwepo na mabadiliko makubwa katika idadi ya visa na vifo vya malaria kunasikitisha.”

Hali halisi ya malaria

Kwa mujibu wa ripoti hiyo mwaka 2018 inakadiriwa kwamba wanawake wajawazito milioni 11 waliathirika na malaria katika maeneo yaliyo na kiwango cha wastani au cha juu cha maambukizi kwenye nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Na matokeo yake karibu watoto 900,000 walizaliwa wakiwa na uzito mdogo.

Na ripoti inasema licha ya kuwepo na dalili za matumaini katika matumizi ya nyenzo za kuzuia malaria kwa kina mama wajawazito na watoto , hakukuwa na kuimarika kokote kwa kiwango cha kimataifa cha maambukizi ya malaria kati ya mwaka 2014 hadi 2018 katika nchi zilizoathirika zaidi na ugonjwa huo.

Ripoti imesisitiza kwamba kutokuwepo na ufedha za kutosha kunasalia kuwa kikwazo kikubwa cha kupiga hatua zozote dhidi ya ugonjwa huo siku za usoni. Mwaka 2018 jumla ya fedha zote kwa ajili ya kudhibiti na kutokomeza malaria zilifikia takriban dola bilioni 2.7 ikiwa ni pungufu ya dola bilioni 5 za lengo la mkakati wa kimataifa wa kutokomeza malaria.

Mama akihudumia mtoto anayeumwa malaria katika hospitali nchini Malawi.
WHO/Mark Nieuwenhof
Mama akihudumia mtoto anayeumwa malaria katika hospitali nchini Malawi.

Mzigo mkubwa na athari kubwa

Mwaka jana WHO na ushirika wa RBM wa kutokomeza malaria walizindua mkakati wa “mzigo mkubwa hadi athari kubwa”(HBHI) wenye lengo la kupunguza visa na vifo vya malaria katika nchi zilizoathirika Zaidi. Mkakati huo unongozwa nan chi 11 ambazo zilikuwa na asilimia 70 ya mzingo wa malaria kwa mwaka 2017. Na kufikia Novemba 2019 mkakati huo wa HBHI umeanzishwa katika nchi tisa kati ya hizo 11. Na nchi mbili zimearifu punguzo kubwa la visa vya malaria mwaka 2018 kuliko mwaka uliotangulia, mfano India ilikuwa na visa milioni 2.6 pungufu yam waka uliotangulia na Uganda visa milioni 1.5 pungunfu yam waka uliotangulia.

Kulinda wanawake na watoto

Ripoti inasema inakadiriwa kwamba asilimia 61 ya wanawake wajawazito na watoto walilalia vyandarua vilivyopulizwa dawa ya kujikinga na mbu mwaka 2018 ukilinganisha na asilimia 26 mwaka 2010 Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Miongoni mwa wanawake wajawazito walipopata dozi zote tatu zilizopendekezwa kuzuia malaria (IPTp) katika vituo vya afya iliongezeka kutoa asilimia 22 mwaka 2017 na kufikia asilimia 31 mwaka 2018.

Kwa mujibu wa ripoti bado wanawake wengi hawakuweza kupata dozi zote tatu au hata moja ya IPTp. Na wanawake wengine hawakuweza kupata huduma za afya ya uzazi.

Kwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano wanaosihi Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara WHO inapendekeza mkakati wa msimu wa kuzuia ugonjwa huo (SMC) wakati wa kipindi kikubwa cha maambukizi cha mvua. Mwaka 2018 asilimia 72 ya watoto waliostahili kupewa chanjo walifaidika nayo.