Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia imeshindwa kupatia huduma bora za uzazi wajawazito maskini- UNICEF

Mtoto mchanga wa umri wa siku mbili akiwa amelala pembezoni mwa mama yake katika wodi ya wazazi huko Rajasthan India.
UNICEF/Prashanth Vishwanathan
Mtoto mchanga wa umri wa siku mbili akiwa amelala pembezoni mwa mama yake katika wodi ya wazazi huko Rajasthan India.

Dunia imeshindwa kupatia huduma bora za uzazi wajawazito maskini- UNICEF

Afya

Tathmini mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF inaonesha kuwa zaidi ya kaya milioni 5 barani Afrika, Asia na Amerika ya Kusini hutumia zaidi ya asilimia 40 ya matumizi yao yasiyo ya chakula katika huduma za afya ya mama mjamzito kutokana na gharama hizo kuwa za juu.

Tathmini hiyo imo kwenye ripoti ya UNICEF  iliyotolewa leo mjini New York, Marekani na Vancouver, Canada ikisema kuwa takribani theluthi mbili ya kaya hizo zipo barani Asia, milioni 1.9 barani Afrika.

Uchambuzi unaonesha kuwa gharama za huduma kabla ya kujifungua na za kujifungua ni za juu kiasi cha kumzuia mjamzito kutosaka huduma sahihi na hivyo kutishia afya yake na  ya mtoto wake.

Mathalani katika nchi za kusini mwa Asia, wajawazito kutoka kaya tajiri hutembelea kliniki mara nne zaidi kuliko mjamzito kutoka kaya maskini ilihali inapokuja katika kujifungua kwenye kituo cha afya, pengo kati ya maskini na tajiri ni maradufu zaidi katika nchi za Afrika Magharibi na Kati.

Ripoti imegusia pia vifo wakati wa kujifungua ikisema kuwa ni moja ya sababu za vifo vka wasichana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 19 kwa kuwa mara nyingi wanapokuwa wajawazito hawasaki ushauri wa kiafya au hata kujifungua kituo cha afya kama wanawake watu wazima.

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore amesema, pindi familia zinapotafuta njia fupi ya kupunguza gharama za uzazi, maisha ya mama na mtoto yapo hatarini.

Ili kukabili  hali ya sasa, UNICEF kupitia  kampeni yake ya kila mtoto awe hai, ina mapendekezo manne ikiwemo kuwekeza fedha zaidi kweney mifumo ya afya kuanzia ngazi za mashinani.

Pili, kuajiri, kufundisha na kusimamia vyema madaktari, wauguzi na wakunga wenye ujuzi wa masuala ya uzazi na watoto wachanga.

UNICEF pia inataka vituo vya afya viwe na huduma za maji, sabuni na umeme zinazoweza kutumiwa na kila mama na mtoto na pia kuwezesha wasichana barubaru na familia zao kudai na kupata huduma bora za afya.