Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi 12 Barani Afrika kuanza kutoa chanjo ya Malaria

Mwanamke akipokea dawa ya kuzuia malaria katika kituo cha afya nchini Uganda
© UNICEF/Maria Wamala
Mwanamke akipokea dawa ya kuzuia malaria katika kituo cha afya nchini Uganda

Nchi 12 Barani Afrika kuanza kutoa chanjo ya Malaria

Afya

Nchi 12 katika barani Afrika zinatazamiwa kupokea dozi milioni 18 za chanjo ya kwanza ya malaria katika kipindi cha miaka miwili ijayo imeeleza leo taarifa ya pamoja iliyotolewa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la Afya ulimwenguni WHO na linaloshughulika na watoto UNICEF huku wakishirikiana na Ubia wa chanjo duniani, GAVI. 

Tangu mwaka 2019 nchi tatu barani Afrika ambazo ni Ghana, Kenya na Malawi zilikuwa zikitoa chanjo hiyo kupitia Mpango wa Utekelezaji wa Chanjo ya Malaria (MVIP) na sasa nchi 9 ambazo ni Benin, Burkina Faso, Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, Liberia, Niger, Sierra Leone na Uganda, ambazo zitaendea kuanzisha utoaji wa chanjo hiyo ya malaria katika programu zao za kawaida za chanjo kwa mara ya kwanza.

“Chanjo hii ina uwezo wa kuwaleta matokeo makubwa chanya katika vita dhidi ya malaria, na inapojumuishwa pamoja na afua zingine, inaweza kuzuia makumi ya maelfu ya vifo vya siku zijazo," amesema Thabani Maphosa, Mkurugenzi Mkuu wa programu wa GAVI. 

Mhudumu wa afya akiwa ameshika sindano ya chanjo ya malaria nchini Ghana wakati wa kampeni ya chanjo kwa wingi. (Maktaba)
WHO
Mhudumu wa afya akiwa ameshika sindano ya chanjo ya malaria nchini Ghana wakati wa kampeni ya chanjo kwa wingi. (Maktaba)

Chanjo zitaanza kutolewa lini?

Maphosa amesema wakiwa na jukumu la kuhakikisha usambazaji wanatarajia kufanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa "Wakati tunafanya kazi na watengenezaji kusaidia kuongeza usambazaji, tunahitaji kuhakikisha kuwa dozi tulizo nazo zinatumika kwa ufanisi iwezekanavyo, ambayo inamaanisha kutumia mafunzo yote kutoka kwa programu zetu za majaribio tunapopanua usambazaji hadi kufikia nchi 12.”

Dozi za kwanza za chanjo hiyo zinatarajiwa kuwasili katika nchi hizo katika robo ya mwisho ya mwaka huu 2023, huku nchi zikianza kuzisambaza mapema 2024.

Mpango huo wa utoaji chanjo unaoratibiwa na WHO na kufadhiliwa na Gavi, Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria, pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la kufanikisha upatikanaji wa dawa na tiba kwa gharama nafuu UNITAID. 

Malaria na vifo vya watoto

Malaria inasalia kuwa moja ya magonjwa hatari zaidi barani Afrika, na kuua karibu watoto nusu milioni kila mwaka wenye umri chini ya miaka 5, na kuchangia takriban 95% ya visa vya malaria duniani na 96% ya vifo kwa mwaka 2021.

Katika kipindi cha miaka mitatu ya majaribio, chanjo hiyo ya Malaria inayotwa RTS,S/AS01 imetolewa kwa zaidi ya watoto milioni 1.7 nchini Ghana, Kenya na Malawi na imeonekana kuwa salama na yenye ufanisi, na hivyo kusababisha kupungua kwa malaria kali na kupungua kwa vifo vya watoto. 

Clara Magalasi kutoka maeneo ya kijijini ya mji mkuu wa Malawi, Lilongwe alitembea kilometa 4 kuhakikisha mtoto wake Grace mwenye umri wa miezi 22 anapata dozi yake ya nne na ya mwisho ya chanjo ya Malaria.
WHO Malawi
Clara Magalasi kutoka maeneo ya kijijini ya mji mkuu wa Malawi, Lilongwe alitembea kilometa 4 kuhakikisha mtoto wake Grace mwenye umri wa miezi 22 anapata dozi yake ya nne na ya mwisho ya chanjo ya Malaria.

“Karibu kila dakika, mtoto mwenye umri chini ya miaka 5 hufa kwa malaria," alisema Mkurugenzi Mshiriki wa UNICEF wa Kinga Ephrem T Lemango na kuongeza kuwa kwa muda mrefu, vifo hivyo vimekuwa vikizuilika na kutibika. 

Ephrem amesema kuanza kutolewa kwa chanjo hii kutawapa watoto, hasa barani Afrika, nafasi nzuri zaidi ya kunusurika, kuokoa maisha. “Chanjo ya malaria ni mafanikio ya kuboresha afya ya mtoto, maisha ya mtoto na familia kwa jumuiya, kwa haki, wanataka chanjo hii ifikie kila mtoto.”

Takriban mataifa 28 ya Afrika yameonesha nia ya kupokea chanjo ya malaria.

Ugawaji wa kwanza wa dozi za chanjo ya malaria unapewa kipaumbele kwa watoto walio katika hatari kubwa ya kufa kutokana na malaria alisema Dk Kate O’Brien, Mkurugenzi wa Kinga, Chanjo na Biolojia wa WHO. "Mahitaji makubwa ya chanjo na ufikiaji mkubwa wa chanjo ya watoto itaongeza usawa katika upatikanaji wa kuzuia malaria na kuokoa maisha ya vijana wengi. Tutafanya kazi bila kuchoka ili kuongeza usambazaji hadi watoto wote walio katika hatari wapate ufikiaji.”

Kusoma zaidi juu ya mpango wa ugawaji wa chanjo hizo bofya hapa.