Mradi wa uzazi wa mpango wa UNFPA kisiwani Unguja umeboresha hata mapenzi kati yetu-Othman Vuai

2 Oktoba 2019

Na sasa tuelekee Kwarara Unguja, Zanzibar nchini Tanzania ambako shirika la idadi ya watu duniani, UNFPA limefadhili mradi wa ushirikishaji wa wanaume katika elimu ya afya ya Uzazi.

Afisa Mawasiliano mkuu wa UNFPA Tanzania, Warren Bright katika kukagua miradi hiyo kuangazia miaka 25 ya mafanikio ya mkutano wa kimataifa kuhusu idadi ya watu na maendeleo, ICPD uliofanyika Cairo, Misri mwaka 1994, amezungumza na Mwalimu Othman Maulid Vuai na mkewe Nargis Nassor ambao ni wanufaika wa mradi huo.

 

 

Bwana Vuai akiwa ameketi na mke wake, anaanza kwa kueleza alivyoipokea taarifa ya kushiriki mafunzo yatakayomuhitaji kuambatana na mkewe, "mimi sikuwa na pingamizi olote kwasababu uzazi wa mpango ni jambo zuri  una faida nyingi kuliko hasara, na mimi nilishiriki na mke wangu tukapewa mafunzo mazuri kabisa.

Akijibu swali la ni mafunzo gani waliyoyapata na wanaona yana umuhimu gani katika familia, Bi Nargis anasema, “ni mafanikio mengi sana, kwanza kushirikishwa, kwasababu nilikuwa sielewi kabisa haya masuala ya uzazi wa mpango na pia nimepata kujijua na kujitambua.”

Naye mumewe, Bwana Vuai anaongeza kwa kusisitiza, “na hivi ninavyokwambia siku ya Ijumaa tunaenda kumpeleka mtoto wetu, na hayo yote tumeyapata siku ambayo tulipewa mafunzo ya uzazi wa mpango.  Kwa maana uzazi wa mpango ni njia moja ya kuboresha mapenzi ndani ya ndoa.”         

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud