Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi kubwa ya wanawake hawana sauti ya maamuzi kuhusu miili yao-UNFPA

Wanawake na uongozi
UN Women/Ryan Brown
Wanawake na uongozi

Idadi kubwa ya wanawake hawana sauti ya maamuzi kuhusu miili yao-UNFPA

Wanawake

Haki za afya ya uzazi na chaguo ni jambo la uhalisi kwa wanawake wengi hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote, imesema ripoti mpya ya shirika la umoja wa mataifa la idadi ya watu, UNFPA kuhusu hali ya idadi ya watu duniani mwaka 2019 iliyotolewa leo Jumatano.

Hata hivyo ripoti hiyo imesema licha ya mafanikio hayo, idadi kubwa ya wanawake kote ulimwenguni hawajawezeshwa kufanya maamuzi hayo muhimu kuhusu miili yao.

Ripoti hiyo ya UNFPA, kwa mara ya kwanza imechapisha takwimu za uwezo wa wanawake kuamua kuhusu masuala matatu ambayo ni kujamiiana na wapenzi wao, matumizi ya huduma za uzazi wa mpango, na afya.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika nchi 51 ambako taarifa hizi zinapatikana ni asilimia57 tu ya wanawake walio ndani ya ndoa au walio na mahusiano ya kingono wanaweza kuamua wenyewe juu ya masuala hayo matatu.

Ripoti hiyo ya UNFPA inaonyesha kwamba maamuzi kuhusu mahusiano ya kingono na afya ya uzazi katika nchi mbili yaani Ufilipino na Ukraine, asilimia 81 ya wanawake wamewezeshwa kufanya maamuzi yao binafsi.

Kwa upande mwingine katika nchi tatu; Mali, Niger na Senegal ni asilimia 7 tu ya wanawake wanaweza kuamua kuhusu kujamiana na wapenzi wao, matumizi ya njia za uzazi wa mpango na afya.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa UNFPA, Dkt.Natalia Kanem amesema, “safari ni ndefu kabla wanawake wote na wasichana wawe na uwezo na njia ya kuamua kuhuzu miili yao na kufanya maamuzo kuhusu afya yao ya uzazi.”

Wanawake wakiuza nyanya katika soko  barani Afrika.
FAO/Cristina Aldehuela
Wanawake wakiuza nyanya katika soko barani Afrika.

Hatua zimepigwa

Licha ya takwimu za kusikitisha, lakini taswira inaonyesha hatua ambazo zimepigwa katika historia ya afya ya uzazi na haki kwa mujibu wa ripoti mpya ikipewa jina, “biashara isiyomalizika:Harakati za haki na maamuzi kwa wote.”

Kwa mujibu wa UNFPA ni mwaka 1968 ambapo viongozi kwa mara ya kwanza katika makubaliano ya kimataifa waliamua kwamba watu binafsi wana haki ya kuamua kwa uhuru idadi ya watoto wanaotaka na miaka ya kusubiri kabla kupata mwingine.

Watu wengi zaidi waliweza kuamua na kufurahia haki ya uzazi wa mpango wakati mbinu hizo zilipatikana kwa watu wengi na hivyo kuimarisha afya na uzima wa kiuchumi wa wanawake wengi.

Kufuatia makubaliano ya kongamano ya kimatifa kuhusu idadi ya watu na maendeleo, ICPD miaka 25 iliyopita ambapo serikali zilikubaliana kwamba afya ya uzazi na haki iwe katikati wa juhudi za maendeleo ambapo tangu wakati huo uzazi wa mpango umeimarika kote ulimwenguni.

Mwaka 1994 ailimia 54 ya wanawake walikuwa wanatumia mbinu za kisasa za mpango wa uzazi ikilinganishwa na asilimia 58 leo.

Upatikanaji wa afya ya uzazi umeimarika kwani wanawake wanaofariki dunia kutokana na changamoto za uja uzito zimepungua kutoka 369 kwa kila watoto laki moja wanaozaliwa mwaka 1994 hadi 216 mwaka 2015.

Licha  ya hatua safari bado ni ndefu

Kwa mujibu wa ripoti ya UNFPA, makundi yaliyotengwa yanakabiliwa na mahitaji mengi zaidi ya huduma za afya ya uzazi ikiwemo jamii za walio wachache, vijana, watu ambao hawajaolewa, wapenzi wa jinsia moja, watu wanaofanya mapenzi na wanaume na wanawake, watu wanoishi na ulemwavu na watu maskini

Kuhusu hilo Dkt. Kanem amesema, “ni lazima tukabiliane na vikwazo vinavyoweza kuturudisha wakati ambapo wanawake walikuwa na sauti ndogo kuhusu maamuzi ya afya ya uzazi au kuhuzu maisha yao kwa ujumla,” ameongeza kuwa, “vita vya haki na maamuzi vinapaswa kuendelea hadi pale itakuwa ni hali halisi kwa wote.”

Kundi la wanawake mjini Mogadishu Somalia.
OCHA
Kundi la wanawake mjini Mogadishu Somalia.

 

Safari kuelekea Nairobi

Mwaka huu ikiwa ni robo karne tangu kupitishwa kwa makubaliano ya ICPD,UNFPA inasema dunia lazima iimarishe juhudi maradufu kwa ajili ya kuhakikisha haki za afya ya uzazi kwa wote.

Kwa mantiki hiyo mwezi Novemba, UNFPA, serikali ya Kenya na ile ya Denmark zitaratibu kongamano mjini Nairobi, Kenya kuhimiza viongozi na serikali na washikadau kuongeza ari ya dhamira ya kufikia haki na maamuzi kwa wote.

“Kongamano la Nairobi litatuwezesha kuchagiza ushirikiano na wadau kwa ajili ya kulinda hatua zilizopigwa na kusongesha mbele ajenda ya ICPD kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma,” amesema Dkt. Kanem.