Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tutumie vikao vya wiki ijayo kuonesha watu tunawajali badala ya kuja na kauli zilizorembwa- Guterres

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres akizungumza na wanahabari kuashiria kuanza kwa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la UN
UN Photo/Cia Pak
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres akizungumza na wanahabari kuashiria kuanza kwa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la UN

Tutumie vikao vya wiki ijayo kuonesha watu tunawajali badala ya kuja na kauli zilizorembwa- Guterres

Masuala ya UM

Kufuatia kuanza kwa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA74,  jijini New York, Marekani, Katibu Mkuu wa umoja huo Antonio Guterres leo amekutana na waandishi wa habari kuzungumzia matarajio yake ya vikao muhimu vya wiki ijayo ambapo pia amejibu maswali kadhaa kutoka kwa wanahabari hao.

Katibu Mkuu amesema matarajio yake ni kwamba viongozi wa serikali na nchi watatumia vikao hivyo kuonesha kuwa wanajali wakazi wa sayari ya dunia na kushughulikia changamoto kubwa zinazokabili ulimwengu hivi sasa.

Amesema dunia hivi sasa iko katika hali tete katika maeneo kadhaa, kuanzia dharura ya tabianchi, kuongezeka kwa pengo la ukosefu wa usawa, ongezeko la chuki na ukosefu wa stahmala sambamba na changamoto za usalama na amani huku mivutano ikiongezeka kila kona.

Tweet URL

 

Bwana Guterres amesema ni kwa mantiki hiyo bila shaka dunia inahitaji ushirikiano wa kimataifa kuliko wakati wowote ule lakini, “kusema tu haitafanikisha,” kwa hiyo amesema, “changamoto kubwa inayokabili viongozi na taasisi ni kuonesha kuwa wanajali na kuhamasisha suluhu ambazo zinajibu shaka na shuku za watu. Wiki ijayo ya vikao vya juu imetengwa kufanikisha hilo. Kwa kuzingatia idadi kubwa ya viongozi wanaokuja Umoja wa Mataifa, tuna fursa ya kusongesha diplomasia ya amani. Nimesisitiza kuwa wiki ijayo ya vikao vya ngazi ya juu isiwe mijadala ya kitaalam na kauli zilizorembwa.”

SUDAN SASA ISAIDIWE LA SIVYO MAFANIKIO YATATOWEKA

Waandishi wa habari walipata fursa ya kuuliza maswali ambapo mojawapo ni mtazamo wake kuhusu kile kinachoendelea nchini Sudan ambapo  baada ya vuguvugu na maandamano hivi sasa kuna kipindi cha mpito.

Akijibu swali hilo, Bwana Guterres amesema kinachoendelea Sudan ni matumaini makubwa na anaamini kuwa kile kilichowezekana nchini humo kupitia mazungumzo ni kiashiria kuwa mizozo yote ya kisiasa inaweza kutatuliwa kwa mazungumzo pindi kuna utashi wa kisiasa na hilo ni funzo kwa kila mtu.

Hata hivyo amesema huu ni wakati wa jamii  ya kimataifa kusaidia Sudan kwa kuwa, “Sudan iko katika hali mbaya zaidi ya kiuchumi, natumai kuwa vikwazo vyote vilivyowekewa Sudan, ikiwemo kutengwa kama nchi inayounga mkono ugaidi vitaondolewa haraka na natumaini kutakuwepo na uhamasishaji wa rasilimali ili kuweza kusaidia Sudan kukabiliana na hali ngumu ya uchumi ambayo inakabiliwa sasa kwa sababu iwapo hili lisipofanyika bila shaka tunahatarisha kupoteza mafanikio ya kidemokrasia, haki za binadamu na kisiasa yaliyopatikana.”

Melen, eneo la makazi duni katikati ya mji mkuu wa Cameroon, Yaoundé
© UN-Habitat/Kirsten Milhahn
Melen, eneo la makazi duni katikati ya mji mkuu wa Cameroon, Yaoundé

MIJI NI SULUHISHO LA MABADILIKO YA TABIANCHI

Alipoulizwa kuhusu mtazamo wake juu ya taarifa ya kwamba Rais wa Marekani pamoja na mamlaka ya mazingira nchini Marekani watafuta uamuzi wa serikali ya jimbo la California wa kuweka udhibiti mkali wa uchafuzi wa hewa utokanao na magari, Katibu Mkuu amesema, “ninaunga mkono sana mchakato wa ugatuzi wa hatua kama hizo na ninapinga sana ubinyaji wa hatua hizo nadhani ni muhimu na ni dhahiri kwa nchi nyingi duniani ya kwamba miji, majiji na majimbo yana uwezo wa kutunga kanuni chanya juu ya hatua kwa tabianchi.”

IRAN NA ZIMBABWE

Kuhusu tangazo ya kwamba viongozi wa baadhi ya nchi ikiwemo Iran hawajapata vibali vya kuingia Marekani ili kuweza kuhudhuria mjadala wa wiki ijayo ambapo Katibu Mkuu amesema tayari wapo kwenye mazungumzo na mwenyeji Marekani ili kushughulikia changamoto hiyo iliyojitokeza kwa siyo tu Iran bali pia na makundi mengine.

Waandishi wa habari wakataka kufahamu msimamo wa Katibu Mkuu kuhusu ongezeko la ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Zimbabwe na athari zake kimataifa, Katibu Mkuu amesema marekebisho  ya dhati ya kiuchumi na kisiasa yanatekelezwa kusongesha wananchi wake na pia kupata msaada ambao unahitaji lakini suala la haki za binadamu lazima liwe sehemu yake.