Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamani tusisahau kuwa dunia ina matarajio makubwa na UN- Balozi Bande

Rais wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa Balozi Tijjani Muhammad-Bande akizungumza na waandishi wa habari jijini New  York, Marekani, Septemba 2019
UN /Mark Garten
Rais wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Balozi Tijjani Muhammad-Bande akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani, Septemba 2019

Jamani tusisahau kuwa dunia ina matarajio makubwa na UN- Balozi Bande

Masuala ya UM

Hatimaye kikao cha kwanza cha mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kimeanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani chini ya uongozi wa Rais wake Balozi Tijjani Muhammad-Bande kutoka Nigeria.

Kikao kilianza kwa Balozi Bande kugonga nyundo hiyo ya kuitisha wajumbe ili waketi tayari kwa shughuli za siku hiyo.

Kisha akatangazia wajumbe wasimame kwa dakika moja, ikiwa ni tamaduni ya kuanza kwa kikao kwa maombi na tafakuri.

Hatua hiyo ikafuatiwa na hotuba ya kwanza kabisa ya Balozi Bande kwa wajumbe ambapo alishukuru wajumbe wa Baraza hilo kwa kumuamini sambamba na kumshukuru Rais wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu, Bi. Maria Fernanda Espinosa.

Amerejelea vipaumbele vyake vinavyolenga utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, hususan kuhusu elimu, kutokomeza umaskini, elimu bora sambamba mabadiliko ya tabianchi.

Halikadhalika amesema atasongesha majukumu anayorithi kutoka vikao vilivyoendelea huku akiomba usaidizi na ushirikiano kutoka kwa wajumbe ambao ni wawakilishi kutoka nchi wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa.

Rais huyo wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu akatoa ombi mahsusi kwa wajumbe akisema, “wakati wa mkutano huu, nasihi wanachama wote wabadilishane uzoefu wao kuhusu utokomezaji wa umaskini hususan jinsi gani mifumo bora ya hifadhi ya jamii inaweza kunufaisha watu walio hatarini zaidi waondokane na umaskini. Nawaombe nyote mjikite kwenye jinsi ya kuboresha vyema mifumo hiyo ili iondoe watu kwenye lindi la umaskini.”

Na kisha Balozi Bande akakumbusha wajumbe kuwa,“katu tusisahau kuwa dunia inaangalia Umoja wa Mataifa kama chombo bora zaidi cha kufanikisha amani na usalama, maendeleo endelevu na haki za binadamu.”

Tijjani Muhammad-Bande (kwenye skrini na kwenye jukwaa) Rais wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la UN akifungua kikao cha kwanza cha mkutano huo. (17 Septemba 2019)
UN /Kim Haughton
Tijjani Muhammad-Bande (kwenye skrini na kwenye jukwaa) Rais wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la UN akifungua kikao cha kwanza cha mkutano huo. (17 Septemba 2019)

Guterres ataka hatua zaidi kumaliza kutokuaminiana baina ya mataifa

Akizungumza kwenye tukio hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amempongeza Balozi Bande kwa vipaumbele alivyotangaza mwezi Juni mwaka huu punde tu baada ya kuchaguliwa.

“Amani na usalama, kutokomeza umaskini, kutokomeza njaa, elimu bora, hatua kwa tabianchi na ujumuishaji wa kila mtu, vyote ni kitovu cha ajenda ya maendeleo endelevu,” amesema Katibu Mkuu.

Halikadhalika amepongeza msisitizo wake kuhusu haki za binadamu na usawa wa jinsia, kuanzia kwenye Umoja wa Mataifa.

Bwana Guterres amekumbusha kuwa watu wana matarajio makubwa kutoka Umoja wa Mataifa hususan kupitia Baraza Kuu na Baraza la  Usalama, hata hivyo akagusia pia hoja aliyotoa Balozi Bande mwezi Juni kuhusu kutoweka kwa kuaminiana baina ya mataifa akisema kuwa, “uwazi, mashauriano na maelewano ni mambo muhimu sana katika kutokomeza ukosefu huo wa kutokuaminiana. Baraza Kuu ni jukwaa la kipekee ambamo kwamo dunia inakutana na kusongesha masuala muhimu. Ni muhimu kwa dunia kuwa na taasisi thabiti za ushirikiano wa kimataifa na muundo ambao kwamo mahusiano ya kimataifa yanazingatia sheria ya kimataifa,” amesema Katibu Mkuu.

Bwana Guterres amekumbusha kuwa ushirikiano wa kimataifa ulio jumuishi na wenye mtandao thabiti, utasaidia kukabiliana na changamoto za zama za sasa ambazo ni za kimataifa na zinaingiliana.