Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mustakabali ni wa wazalendo na si wakumbatia utandawazi- Trump

Rais Donald Trump wa Marekani akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (24 Septemba 2019)
UN Photo/Cia Pak
Rais Donald Trump wa Marekani akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (24 Septemba 2019)

Mustakabali ni wa wazalendo na si wakumbatia utandawazi- Trump

Amani na Usalama

Rais Donald Trump wa Marekani amehutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akipigia chepuo uzawa badala ya  utandawazi.

Katika hotuba yake ya dakika 38 ikiangazia masuala ya biashara, uchumi, usalama, afya na maendeleo, Rais Trump amesema mataifa huru ni lazima yakumbatie misingi ya kitaifa na  katu yasijaribu kuyafuta au kuyabadilisha, “iwapo unataka uhuru jivunie nchi  yako, ukipenda demokrasia zingatia uhuru wako na ukitaka amani penda taifa lako.”

Amekumbusha kuwa mwelekeo sasa ni kuweka kipaumbele kwa taifa na wananchi akisema kuwa, Marekani hivi sasa iko kwenye kipindi cha ufufuko na kwamba,

“viongozi wenye busara kila wakati wanaweka mbele maslahi ya wananchi na taifa lao kwanza. Mustakabali si kwa wapenda utandawazi bali, mustakabali ni wa wazalendo.”

Amesema ndio maana kila wafanyacho Marekani ni kuwezesha raia wake akitetea será za ukuaji wa uchumi zinazozingatia ukuaji wa ndani akisema zimesaidia kuongeza idadi ya ajira.

TUMEJIZATITI KUONDOKANA NA MFUMO WA BIASHARA KANDAMIZI

Kuhusu biashara, Rais Trump amesema wakati wa baadhi ya mataifa kujinufaisha na biashara umekishwa. “kwa miongozo kadhaa mfumo wa biashara duniani umekuwa ukitumiwa vibaya na mataifa machache, kazi zikipelekwa nje huku watu wa kada ya kati wakihaha.”

Amesema hivi sasa Marekani hivi sasa imeamua kuchukua hatua kuhakikisha kuwa biashara ya kimataifa inakuwa ya mizania na inafaisha pande zote akitolea mfano wa mikataba mipya na Canada na Mexico na kesho watakuwa na mkataba mpya na Japan.

Kuhusu urafiki amesema kuwa Marekani iko tayari kujenga urafiki na wale wote wanaosaka amani na heshima kwa dhati akisema wale walio marafiki wa Marekani kwa kuwa Marekani haiamini suala la kuwa na adui wa kudumu.

Amekumbusha mtu yeyote anaweza kuanzisha vita lakini ni wachache majasiri ambao wanaweza kusaka amani.

HAKI ZA KUJIELEZA, WANAWAKE NA LGBTQ

Kuhusu haki amezungumzia mitandao ya kijamii akisema watahakikisha kuwa mitandao hiyo haibinyi haki ya wananchi kuwa huru kujieleza kupitia mitandao ya kijamii.

Akizungumzia pia haki za wapenzi wa jinsia moja na mashoga, Rais Trump amesema wako na mshikamano na watu hao na katu hawatokubali kuona haki zao zinakandamizwa popote pale duniani.

Kuhusu wanawake, Rais Trump amesema kuwa Marekani inajitahidi kuhakikisha kuwa duniani kote wanawake wana haki sawa na wanaume ya kumiliki mali, kusafiri huru na kupata mikopo.