Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 54 ya watu Sudan Kusini hawana uhakika wa chakula:FAO/UNICEF/WFP

Wanawake wa Yei nchini Sudan Kusini wakati walisimama kuzungumza na walinda amani wa UNMISS ambao walikuwa wanapiga doria eneo hilo
UNMISS/Isaac Billy
Wanawake wa Yei nchini Sudan Kusini wakati walisimama kuzungumza na walinda amani wa UNMISS ambao walikuwa wanapiga doria eneo hilo

Asilimia 54 ya watu Sudan Kusini hawana uhakika wa chakula:FAO/UNICEF/WFP

Msaada wa Kibinadamu

Zaidi ya nusu ya watu wote nchini Sudan Kusini hawana uhakika wa chakula licha ya juhudi ha hatua zilizopigwa yamesema mashirika ya Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, la mpango wa chakula WFP na la chakula na kilimo FAO.

Kwa mujibu wa ripoti ya leo ya hali ya uhakika wa chakula na mgawanyo wake IPC, licha ya kuimarika kwa hali ya uhakika wa chakula tangu Juni mwaka 2019 bado zaidi ya nusu ya watu nchini humo ambao ni milioni 6.35 hawajui mlo wao utakaofuata utatoka wapi.

Taarifa hiyo ya IPC iliyotolewa kwa pamoja na serikali ya Sudan Kusini imeonya kwamba asilimia 54 ya watu wa taifa hilo changa kabisa barani Afrika hawana uhakika wa chakula na wanahaha kutimiza mahitaji ya mlo ya kila siku.

Ripoti inakadiria kwamba watu 10,000 wako katika hali mbaya zaidi ya daraja la 5 na wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula huku wengine milioni 1.7 wako katika hali ya dharura ya daraja la 4 na wengine milioni 4.6 wako katika kiwango cha mgogoro wa chakula daraja la 3.

Eneo lililoathirika zaidi kwa mujibu wa UNICEF, FAO na WFP  ni jimbo la Greater Nile likifuatiwa na jimbo la Bahr el Ghazal na majimbo yaliyo katika zahma ni Yirol Mashariki ambao linahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu ili kuokoa maisha.

Ingawa hali ya uhakika wa chakula bado ni mbaya  IPC inasema kumekuwa na mabadiliko kidogo ya kuboresha hali yaliyotokana na hatua kubwa katika kufufua makubaliano ya amani yaliyotiwa saini Septemba mwaka 2018. Kupungua kwa vita kumewahamasisha wakulima wengi kurejea nyumbani , pia kumeongeza fursa za maisha na kuimarisha masoko.

Utulivu wa kisiasa pia umeruhusu ufikishaji wa misaada ya kibinadamu kwa watu waliokuwa katika uhitaji mkubwa. Ripoiti ya IPC inasema “Kukiwa na utulivu wa kisiasa na amani endelevu basi Sudan Kusini itaweza kuondokana haraka na mgogoro wa vita na kuinua kiwango cha uzalishaji wa chakula. Na hilo linaonyesha kwamba kufufuliwa kwa muafaka wa amani kumeanza kuzaa matunda na utekelezaji wa mkataba huo ni muhimu sana kwa mustakabali wa taifa hilo ”

Pia imeelezwa kuwa utapia mlo uliokithiri umesalia kuwa changamoto kubwa hasa kwa watoto wa umri wa chini ya miaka 5.