Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 61 ya watu Sudan Kusini kukabiliwa na janga la chakula:WFP/FAO/UNICEF

Mgao wa chakula huko Peri nchini Sudan Kusini ambako WFP inasaidia watu 29,000 kati yao 6,600 ni watoto wenye umri wa chini  ya miaka mitano. (Picha  5 Februari 2019)
WFP/Gabriela Vivacqua
Mgao wa chakula huko Peri nchini Sudan Kusini ambako WFP inasaidia watu 29,000 kati yao 6,600 ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano. (Picha 5 Februari 2019)

Asilimia 61 ya watu Sudan Kusini kukabiliwa na janga la chakula:WFP/FAO/UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Mamilioni ya watu nchini Sudan Kusini kukabiliwa na janga kubwa la ukosefu wa chakula kuwahi kutokea nchini humo yameonya leo mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa yakihimiza hatua kuchukuliwa haraka.

Kwa mujibu wa ripoti  ya tathimini ya viwango vya chakula (IPC) iliyotolewa leo na  mashirika hayo matatu  lile la mpango wa chakula duniani WFP, la chakula na kilimo FAO na la kuhudumia Watoto UNICEF, kwa pamoja na serikali ya Sudan Kusini  inakadiria kwamba takriban watu milioni 6.1 nchini humo sawa na asilimia 61 ya watu wote  watakumbwa na viwango vya juu au zaidi vya kutokuwa na uhakika wa chakula ifikapo mwisho wa mwezi Julai mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis hii leo msemaji wa WFP amesema IPC ripoti inagawanyisha tatizo hilo la chakula katika ngazi tano ngazi ya 1 ikiwa ni tatizo dogo huku ngazi ya 5 ikiwa ni janga kubwa ambapo amesema, “watu wapatao 21,000 huwenda wakakabiliwa na janga kubwa la ukosefu wa chakula ngazi ya 5 huku wengine milioni 1.82 wakikumbwa na dharura ya chakula au ngazi ya 4 na watu wengine milioni 5.12 watakuwa katika mgogoro wa chakula au ngazi ya 3 ya kutokuwa na uhakia wa chakula.”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ukilinganisha makadirio ya Januari yaliyoelezea hali ya Mei hadi Julai mwaka huu watu wengine 81, 000 watakumbwa na mgogoro wa chakula ngazi ya 3 au mbaya zaidi hususan katika maeneo ya Jonglei, Lakes, na majimbo ya Unity.

Ripoti inasema hali hii ya kutokuwepo na uhakika wa chakula imechangiwa na kaya nyingi kutokuwa na chakula cha kutosha katika msimu huu wa muambo lakini kumechochewa na kuchelewa kwa mvua matatizo sugu ya kiuchumi, watu kutawanywa na hali dunia ya maisha kutokana na kuendelea kwa vita, ambapo sababu zote hizi zimeendelea kuathiri uwezo wa kaya nyingi kupata chaula cha kutosha katika msimu huu wa muambo unaoendelea.

Chakula kikisambazwa kwa washiriki wa programu ya chakula ya WFP katika jimbo la Warrap, Sudan Kusini. Hivi sasa WFP inawasaidia watu 200,000 chini ya mpango huo.
WFP/Gabriela Vivacqua
Chakula kikisambazwa kwa washiriki wa programu ya chakula ya WFP katika jimbo la Warrap, Sudan Kusini. Hivi sasa WFP inawasaidia watu 200,000 chini ya mpango huo.

Mashirika hayo ya WFP, FAO na UNICEF yamesema sababbu nyingine kubwa zinazochangia hali mbaya ya uhakika wa chakula nchini Sudan Kusini ni bei ya juu ya chakula iliyosababishwa na mavuno hafifu lakini pia barabara mbovu zinazoathiri usambazaji wa vyakula masokoni.

Hata hivyo yamsema utekelezaji wa makubaliano ya amani na utulivu wa kisiasa Sudan Kusini vinapaswa kuruhusu msaada wa haraka wa kibinadamu ili kunusuru maisha ya watu na kuinua uzalishaji wa kilimo nchini nzima na kuokoa maisha ya watu. Verhoosel amesema kwa wakati huu “WFP inasaidia watu milioni 2.77 Sudan Kusini ,na ikiwa na mpango wa kuongeza msaada wake na kufikia watu milioni  5.1 million ifikapo Disemba 2019 katika kukabiliana na kuongezeka kwa mahitaji.”

Ameongeza kuwa hatua hizo za msaada zitakuwa ni pamoja na kugawa chakula na fedha taslim katika maeneo ambayo masoko yanafanya kazi, kugawa chakula kama ujira kwa watakaofanya kazi katika ujenzi, kusambaza mlo mashuleni, na lishe maalum ya kukabiliana na utapiamlo kwa Watoto na kina mama wajawazito na wanaonyonyesha.

Kwa upande wake shirika la FAO limesema linafanya kazi na wakulima wanaorejea ili kuwasaidia kujumuika tena katika jamii na katika kilimo lakini pia kukabiliana na changamioto za upatikanaji wa mvua.

Pia inagawa mbegu na kutoa mafunzo ambayo yatawasaidia wakulima kupunguza hasara zitokanazo na ukame na mafuriko. Mbali ya kusaidia kaya 800,000 za wakulima, wafugaji na wavuvi FAO inatoa chanjo na huduma kwa wafugaji kuwasaidia kulinda mifugo yao.

Limeongeza kuwa pamoja na jitihada zote zilizopo bado kuna kibarua hasa cha kuongeza uwezo wa wakulima hao kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kama ukame na ukosefu wa mvua katika njia ambayo ni endelevu.

Nalo shirika la UNICEF limesema licha ya changamoto ya uhakika wa chakula utulivu uliopo nchini humo hivi sasa umewasaidia kuwatibu Watoto 100,000 waliokuwa na utapiamlo uliokithiri katika miezi mitano ya mwanzo wa mwaka hu una Zaidi ya asilimia 90 ya Watoto hao wamepona.

Lakini shirika hilo limeonya kwamba kiwango cha utapiamlo bado kikubwa na kibaya katika maeneo mengi na hofu yao ni kwamba njanga hili la kutokuwa na uhakika wa chakula kitafanya hali kuwa mbaya  zaidi katika miezi ijayo.