Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko ya tabianchi yazidisha zahma ya utapiamlo na njaa Sudan Kusini:UNICEF/FAO/WFP 

Mama amempeleka mwanye aliyeathirika vibaya na utapiamlo kwenye kituo cha lishe cha WFP Torit nchini Sudan Kusini
© WFP/Eulalia Berlanga
Mama amempeleka mwanye aliyeathirika vibaya na utapiamlo kwenye kituo cha lishe cha WFP Torit nchini Sudan Kusini

Mabadiliko ya tabianchi yazidisha zahma ya utapiamlo na njaa Sudan Kusini:UNICEF/FAO/WFP 

Tabianchi na mazingira

Umoja wa Mataifa umeonya hii leo kuwa njaa na utapiamlo vinaongezeka katika maeneo yote yaliyokumbwa na mafuriko, ukame na mizozo nchini Sudan Kusini huku baadhi ya jamii zikiwa hatarini kukumbwa na njaa iwapo misaada ya kibinadamu haitakuwa endelevu, halikadhalika mikakati ya kukabili madhara ya mabadiliko ya tabianchi haitaimarishwa. 

Onyo hilo limetolewa leo mjini Juba nchini Sudan Kusini na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la chakula na kilimo, FAO, mpango wa chakula duniani, WFP na la kuhudumia watoto UNICEF, yakiongeza kuwa takribani theluthi mbili ya wananchi wa Sudan Kusini wanaweza kukumbwa na uhaba mkubwa wa chakula kati ya nwezi Aprili na Julai mwakani na watoto milioni 1.4 watakabiliwa na utapiamlo. 

Kwa mujibu wa mashirika hayo kiwango cha utapiamlo kiko katika kiwango cha juu zaidi kuwahi kutokea, kupita viwango vilivyoonekana hata wakati wa vita kati yam waka 2013 na 2016.  

Kupungua kwa uhakika wa chakula na kuenea kwa kiwango kikubwa kwa utapiamlo kunahusishwa na mchanganyiko wa migogoro, hali mbaya ya uchumi, majanga ya mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa gharama za chakula na mafuta.  

Wakati huo huo, kumekuwa na kupungua kwa ufadhili wa programu za kibinadamu licha ya kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu nchini humo. 

Wanawake wakisafisha barabara mjini Bentiu Sudan Kusini ambako theluthi mbili ya eneo hilo imeathirika na mafuriko
© UNHCR/Charlotte Hallqvist
Wanawake wakisafisha barabara mjini Bentiu Sudan Kusini ambako theluthi mbili ya eneo hilo imeathirika na mafuriko

WFP yapambana na njaa 

Makena Walker kaimu Mkurugenzi wa WFP nchini Sudan Kusini amesema "Tumekuwa katika hali ya kuzuia njaa mwaka mzima na tumezuia matokeo mabaya zaidi, lakini hii haitoshi. Sudan Kusini iko mstari kwenye mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi na siku baada ya siku familia zinapoteza makazi, ng'ombe, mashamba na matumaini kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Bila msaada wa kibinadamu wa chakula, mamilioni zaidi watajikuta katika hali mbaya zaidi na hawawezi kutimizia familia zao hata chakula cha msingi zaidi.”  

Ameongeza kuwa mafuriko ambayo hayajawahi kushuhudiwa, ya miaka mingi yanayoikumba nchi hiyo yanazidisha viwango vya juu vya njaa vilivyosababishwa na migogoro inayoendelea na mzozo wa chakula duniani.  

Pia amesema maeneo ya kati ya nchi, ambayo yameathiriwa zaidi na mafuriko ya miaka mingi, ni maeneo yenye viwango vya juu vya uhaba wa chakula. 

FAO inawasaidia wakulima kuzalisha tena chakula 

Kwa upande wake mwakilishi wa FAO nchini Sudan Kusini Meshack Malo, amesema "Msaada wa kujikimu kimaisha unahitajika hasa kuwezesha Sudan Kusini kujitegemea katika uzalishaji wa chakula. Tunajua uwezekano upo kwani takriban tani 840,000 za nafaka zilizalishwa mwaka wa 2021, katika mwaka mgumu wa mabadiliko ya tabianchi, mafuriko, migogoro na mambo mengine. Kwa upungufu wa sasa wa nafaka wa tani 541,000, uwekezaji wa haraka katika maisha ya vijijini unahitajika ili kuongeza uzalishaji na kuweza kujitosheleza,”  

Ameendelea kusema kuwa ingawa kumekuwa na uboreshaji mdogo katika uhakika wa chakula katika baadhi ya maeneo ya nchi, changamoto ya lishe kote Sudan Kusini inazidi kuongezeka. Kaunti zote isipokuwa moja zinaonyesha kuzorota kwa hali yao ya lishe hadi Juni 2023, ikijumuisha kaunti 44 ambapo hali hiyo inachukuliwa kuwa mbaya zaidi. 

Mwanamke akimlisha mwanaye katika moja ya vituo vya lishe Sudan Kusini
© WFP/Eulalia Berlanga
Mwanamke akimlisha mwanaye katika moja ya vituo vya lishe Sudan Kusini

Watoto ni miongoni mwa waathirika wakubwa 

Kwa mujibu wa kaimu mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan Kusini Jesper Moller "Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, mafuriko yameathiri kwa kiasi kikubwa idadi inayoongezeka ya watu kote Sudan Kusini. Miongoni mwa walioathiriwa, ni idadi inayoongezeka ya watoto wasio na chakula na utapiamlo, ambayo jumuiya ya kimataifa haiwezi kuipuuza. Ili kuwalinda watoto kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ni lazima tuhakikishe tunawafikia watoto walio katika mazingira magumu zaidi na kmsaada muhimu wa sekta mbalimbali za huduma za kijamii.” 

Naye Sara Beysolow Nyanti, mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu nchini Sudan Kusini amesema "Ripoti ya IPC ni matokeo ya miezi kadhaa ya ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu, iliyotokana na ushiriki kutoka kwa Serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali NGOs, na washirika wengine.” 

Ameongeza kuwa takwimu za ubora kama hizi ni muhimu katika kuandaa mipango ya kukabiliana na misaada ya kibinadamu ili kusaidia kukidhi mahitaji ya watu nchini humo, na takwimu hizi zinaonyesha watu wa Sudan Kusini wanahitaji msaada zaidi sasa kuliko hapo awali.  

Hivyo amesisitiza kuwa “Ni muhimu kupokea ahadi kutoka kwa wafadhili kwa ajili ya 2023 ili tuweze kuzuia kuzorota kwa hali ya kibinadamu kote nchini." 

Rasilimali kwa ajili ya hatua za misaada ya kibinadamu wa mwaka 2023 nchini Sudan Kusini zinahitajika kwa haraka ndani ya miezi michache ijayo au mashirika yatashindwa kuwasilisha misaada ya kibinadamu kwa wakati kwa mwaka ujao, na kuacha mamilioni ya familia katika hatari kubwa kutokana na kuongezeka kwa njaa.