Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lishe bora inaweza kuokoa maisha ya watu milioni 3.7 ifikapo mwaka 2025- WHO

Mlo wa shuleni ukiandaliwa na akina mama wanoajitolea ambao wamesomea masuala ya lishe, kwa maana ya mandalizi kwa kuzingatia vigezo vya usafi na stadi zingine.
©Pep Bonet/NOOR for FAO
Mlo wa shuleni ukiandaliwa na akina mama wanoajitolea ambao wamesomea masuala ya lishe, kwa maana ya mandalizi kwa kuzingatia vigezo vya usafi na stadi zingine.

Lishe bora inaweza kuokoa maisha ya watu milioni 3.7 ifikapo mwaka 2025- WHO

Afya

Huduma za afya zinapaswa kujikita zaidi katika kuhakikisha kila mtu anapata lishe bora wakati wote wa maisha yake, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la afya ulimwenguni, WHO.

Ripoti hiyo inakadiria kuwa uwekezaji bora kwenye lishe unaweza kuokoa maisha ya watu milioni 3.7 ifikapo mwaka 2025.

“Ili kutoa huduma bora za afya na kufanikisha huduma ya afya kwa wote, UHC, lishe inapaswa kuwa kitovu cha mipango yote kuhusu afya,” amesema Dkt. Naoko Yamamoto, Mkurugenzi Msaidizi wa WHO akiongeza kuwa, “tunahitaji pia kuwa na mazingira bora ya chakula ya kuwezesha watu kula mlo wenye lishe.


Ripoti hiyo inasema kuwa mipango muhimu ya afya inahitaji kujumuisha vipengele vyote vya lishe lakini kila nchi inapaswa kuamua ni hatua gani ya kuchukua ili kuunga mkono sera za kitaifa za afya, mikakati na mipango.


Hatua muhimu za kuchukua kwa mujibu wa WHO ni pamoja na kuhakikisha wajawazito wanapatiwa madini ya chuma na foliki, kuchelewa kukata kitovu cha mtoto ili kuhakikisha mtoto anapata virutubisho bora baada ya kuzaliwa, kuendeleza na kuunga mkono unyonyeshaji watoto wachanga maziwa ya mama, kutoa ushauri kuhusu lishe bora kwa watu wazima na watoto ili kupunguza ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi na hatimaye kusaidia kuepusha magonjwa ya moyo na kiharusi.

Watoto wa Cambodia wakipata mlo. Watoto kukosa lishe bora husababisha unyafuzi
World Bank/Masaru Goto
Watoto wa Cambodia wakipata mlo. Watoto kukosa lishe bora husababisha unyafuzi

 

Ripoti hiyo inasema kuwa, “uwekezaji kwenye lishe kunaweza kusaidia nchi kufikia lengo la huduma ya afya kwa wote na malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. Unaweza pia kusaidia uchumi kwa kuwa kwa kila dola moja inayotumiwa kwenye miradi ya lishe hurejesha dola 16 kwenye uchumi.”


Mafanikio ambayo yamepatikana kutokana na lishe ni pamoja na kupungua kwa udumavu wa watoto kwa kutoka asilimia 39.2 mwaka 1990 hadi asilimia 21.9 mwaka 2018, ingawa yaelezwa kuwa kasi imekuwa ndogo kwa mataifa ya Afrika na Kusini-Mashariki mwa Asia.


Hata hivyo utipwatipwa unaongezeka, imesema ripoti hiyo, iwe kwa watoto na watu wazima ikielezwa kuwa utipwatipwa ni kihatarishi kikubwa cha magonjwa kama vile kisukari, moyo na baadhi ya saratani.