Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia lazima iwekeze katika mifumo ya afya kwa ajili ya sasa na vizazi vijavyo

Huduma za afya ya msingi ni pamoja na chanjo kama inavyoonekana pichani mtoto akipatiwa chanjo kwenye kituo cha afya cha kijiji cha Kombaka nchini Mali.
UNICEF/Seyba Keïta
Huduma za afya ya msingi ni pamoja na chanjo kama inavyoonekana pichani mtoto akipatiwa chanjo kwenye kituo cha afya cha kijiji cha Kombaka nchini Mali.

Dunia lazima iwekeze katika mifumo ya afya kwa ajili ya sasa na vizazi vijavyo

Afya

Dunia imetakiwa kuwekeza katika mifumo imara ya afya ambayo itaweza kumlinda kila mtu sasa na vizazi vijavyo.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake kuhusu siku ya kimataifa ya huduma za afya kwa wote (UHC) inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 12 Desemba.

Katika ujumbe huo Guterres amesiositiza kwamba“Janga la corona au COVID-19 limedhihirisha ni jinsi gani ilivyo muhimu kwa nchi zote kuwa na mifumo imara ya afya ambayo inaweza kutoa hudumua bora kwa watu wote wakati watakaozihitaji huduma hizo.”

Ameongeza kuwa kwa mantiki hiyoKwa siku hii ya kimataifa ya huduma za afya kwa wote hebu tuahidi kumaliza mgogoro hu una kujenga mustakabali salama na wenye afya kwa kuwekeza katika mifumo ya afya ambayo itatulinda sote sasa. Janga la COVID-19 limetuonyesha kwamba hakuna aliye salama hadi pale wote tutakapokuwa salama.”

Pia Bwana. Guterres amesisitiza kwamba mwaka 2020 dunia imeshuhudia janga ambalo limevamia wakati mifumo ya afya imezidiwa uwezo na magonjwa mapya ya mlipuko ambayo mara nyingi hukatili maisha ya watu wengi.

Afisa wa huduma za afya Indonesia  akichunguza damu kuchunguza homa ya mafua makali
UN/maktaba
Afisa wa huduma za afya Indonesia akichunguza damu kuchunguza homa ya mafua makali

COVID-19 imeongeza zahma

Ameongeza kuwa mlipuko wa corona umedhihirisha nini kinachoweza kutokea wakati juhudi za kushughulikia majanga kwenye mifumo ya afya ambayo imeshalemewa kwamba inashindwa kutoa huduma zingine muhimu kama za vipimo na matibabu ya saratani, chanjo na huduma kwa kina mama na watoto.

“Ni lazina tuongeze juhudi endapo tunataka kufikia lengo la huduma za afya kwa wote ifikapo mwaka 2030” amesema Guterres akikumbusha makubaliano yaliyoafikiwa nan chi wanachama wa Umoja wa Mataifa Septemba 2019 miei michache tu kabla ya kuzuka kwa janga la COVID-19.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kufikia lengo hili kunamaanisha sio tu kuongeza matumizi katika masuala ya afya lakini pia kutumia vyema fedha za sekta hiyo kuanzia kuwalinda wahudumu wa afya na kuimarisha miundombinu hadi kuzuia magonjwa na kutoa huduma za afya karibu na nyumbani kwenye jamii.

“Kuwekeza katika mifumo ya afya pia kunaimarisha uwezo wan chi katika kujiandaa na kukabiliana na dharura za afya zitakazojitiokeza siku zijazo”ameeleza Katibu Mkuu.

Mwanamke azingatia mapendekezo ya afya bora kwa kuvaa barakoa kazini kwenye mgahawa nchini Indonesia.
ILO/Feri Latief
Mwanamke azingatia mapendekezo ya afya bora kwa kuvaa barakoa kazini kwenye mgahawa nchini Indonesia.

Waliotengwa na wasiojiweza ndio waathirika wakubwa.

Dharura za afya zimewaathiri kwa kiasi kikubwa watu waliotengwa na wasiojiweza ameendelea kusema Bwana. Guterres akisistiza kwamba wakati chanjo mpya za COVID-19, vipimo na matibabu vitakapopatikana ni lazima viwafikie wote ambao wanavihitaji.

“Katika kukabiliana na janga la COVID-19tumeshuhudia ubunifu wa hali ya juu na wa haraka katika kufikisha huduma za afya na miundo ya kutoa huduma na pia katika maandalizi. Ni lazima tujifunze kutoka katika uzoefu huu.”

Haki ya afya

Naye mkurugenzi mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO Dkt. Tendross Adhanom Ghebreyesus amesema dunia imeadhimisha siku ya haki za binadamu siku chache zilizopita  na siku hizi mbilizinakuja karibu Pamoja mwishoni mwa mwaka huu mgumu , na ni kumbusho kwamba wakati tukijikwamua na janga la COVID-19 ni lazima tufanye hivyo kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu ikiwemo haki ya afya.”

Huu ni wakati muafaka wa kuwekeza katika afya -WHO Dkt. Tedros

Bwana Tedros ameongeza kuwa “mwaka 2020 umetukumbusha kwamba afya ni bidhaa muhimu sana duniani. Wakati wa COVID-19 nchi nyingi zimetoa huduma za upimaji na matibabu ya COVID-19 bure kwa watu wao. Wametambua kwamba uwezo wa kulipia gharama za afya haupaswi kuwa ni tofauti kati ya ugonjwa na afya, kati ya maisha na kifo.”

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus akizungumza katika moja ya taarifa za WHO kuhusu janga la COVID-19
UN Photo/Evan Schneider
Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus akizungumza katika moja ya taarifa za WHO kuhusu janga la COVID-19

Dkt. Tedros ameongeza kuwa kwa upande wake WHO inazindua mikakati miwili ya kusaidia na kusongesha safari za nchi kuelekea huduma za afya kwa wote.
Mosi Dkt. Tedros amesema mosi ni mpango wa kimataifa wa kuimarisha huduma za afya ya msingi, kuziwezesha nchi kuweza kuzuia na kushughulikia dharura za aina zote kuanzia matatizo binafsi ya shinikizo la moyo hadi milipuko ya virusi vipya vinavyokatli Maisha ya watu wengi. 
Na pili ni ujumuishwaji mpya wa UHC ulioandaliwa kuzisaidia nchi kuandaa mafungu ya huduma yanazozihitaji kukidhi mahitaji ya kiafua ya watu wao.